• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 3:28 PM
Kwa mara ya kwanza akina mama wa Kibajuni kisiwani Pate wajihusisha na ufugaji wa nyuki

Kwa mara ya kwanza akina mama wa Kibajuni kisiwani Pate wajihusisha na ufugaji wa nyuki

NA KALUME KAZUNGU

TANGU JADI, jamii ya Waswahili wa asili ya Kibajuni katika Kaunti ya Lamu haijakuwa ikiwapa kipaumbele wanawake kujiendeleza au kujisimamia maishani.

Kimsingi, mwamamke Mbajuni kazi zake nyingi zilihusisha sana masuala ya jioni, kuzaa, kulea, kuchunga na kuipamba nyumba ilhali mwanamume akichanika mpinini kulisaka tonge kwa udi na uvumba, iwe ni kwa kheri au kwa shari.

Cha msingi kwa mwanamume Mswahili wa asili ya Kibajuni ni kuhakikisha familia,mke na watoto wake anawakimu vyema kimahitaji.

Hulka hiyo ilichangia sana ubaguzi na ukaguzi wa majukumu, ambapo kazi zimekuwa zikipangwa mafungu kwamba hizi ni za jinsia ya kiume ilhali nyingine chache zikikubalika kutekelezwa na jinsia ya kike.

Katika ulimwengu wa sasa aidha jamii ya Waswahili Wabajuni imekengeuka kiasi kwamba hakuna tena ubaguzi wa ni kazi ipi iachiwe mwanamume na ipi ya mwanamke.

Hali hiyo inadhihirishwa wazi na wanachama wa kundi la akina mama la Pate-Kisiwani Self-Help Group kutoka kijiji cha Mtangawanda kilichoko kaunti ndogo ya Lamu Mashariki, ambao kwa karibu mwaka mmoja sasa, wamejitosa kwenye shughuli ya ufugaji nyuki na ambayo wanasema inafanya vyema.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa
kundi hilo Bi Fatima Hassan, madhumuni ya kuanzisha ufugaji wa nyuki ni katika harakati za kuidhihirishia jamii ya Waswahili Wabajuni kwamba akifahamucho na kukitekeleza mwanamume, pia mwanamke anaweza kukifanya hicho hicho kwa ubora zaidi.

Bi Hassan anasema walianza harakati zao za kufuga nyuki takriban mwaka mmoja uliopita kupitia ufadhili wa kundi la kijamii la Save Lamu na lile la Uhifadhi wa mazingira na viumbe hai la Northern Rangeland Trust (NRT).

Anasema walipokea mizinga minne kutoka kwa shirika hilo, ambapo baada ya kuitega kwenye mikoko, ni mitatu pekee iliyofaulu kuingiwa na nyuki na kuanza kuzalisha asali.
Bi Hassan anasema mizinga yao huitega kwenye msitu wa mikoko,ambapo asali hutokana na michanganyiko ya maua kutoka kwa miti hiyo.

“Awali tulikuwa tukitekeleza kazi ya kuhifadhi mazingira, hasa kupanda mikoko. Wageni na wafadhili wengi waliokuwa wakitembelea mradi wetu wa kuhifadhi mikoko wakawa wanatuuliza kila wakati kuhusu ni wapi wangepata asali ya mikoko. Hapo ndipo tukaibuka na wazo la kufuga nyuki na kuzalisha asali kutoka mikokoni. Twajivunia kwamba sisi ndio wanawake wa kwanza Wabajuni kufuga nyuki hapa Lamu. Twahisi mradi umebadili vilivyo akina mama,kiasi cha kuinua hadhi yetu zaidi kama jinsia ya kike,”akasema Bi Hassan.

Bi Tima Shebwana ambaye ni mmoja wa wanachama wa Pate-Kisiwani Self-Help Group, alisema waume wao wamekuwa kiungo muhimu katika kufaulisha mradi huo wa kuzalisha asali kupitia kuzitambua na kuzikubali juhudi zao sufufu.

Bi Shebwana anasisitiza kuwa ni kupitia ufugaji wa nyuki ambapo akina mama hao wameweza kujisimamia wenyewe kimahitaji kinyume na awali ambapo kila kitu walitegemea waume wao.

“Angalau waume wetu wanapumzika. Fedha kidogo tupatazo kupitia kilimo cha nyuki zinatusaidia kukidhi mahitaji yetu badala ya kila kitu kupewa na waume wetu. Tunaweza kujisimamia kwa mengi sasa na hili limezidisha upendo kwa ndoa zetu,” akasema Bi Shebwana.

Kwa upande wake, Bi Zulfa Hassan, mmoja wa wanachama, pia aliweka wazi kwamba bidii walizodhihirisha kama wanawake kwamba wanaweza zimesaidia kupunguza migogoro kwa familia zao kinyume na awali.

Bi Hassan alishauri wanawake kujizatiti maishani kwa kuibukia kazi mbalimbali ili kuwasaidia mabwana zao bila kubagua kazi,iwe ni za kike au kiume.

Aliisifu jamii ya Mtangawanda na kisiwa cha Pate kwa ujumla kwa kuwakubali wanawake kufanya kazi za kila aina na kujiendeleza maishani.

“Huu si wakati wa wanawake kubagua kazi. Kazi ni kazi na lile mwamamume aweza kufanya pia mwanamke hulitekeleza kwa ubora zaidi. Wanawake tunaweza,” akasema Bi Hassan.

Bi Halima Chuo aliomba wafadhili zaidi kujitokeza kuwafadhili kwa mizinga itakayowawezesha kuzalisha asali kwa wingi,kupanua shughuli zaidi na kugeuza kilimo cha nyuki wanachoendeleza kwa sasa kuwa cha kibiashara.

“Twashukuru shirika la Save Lamu na NRT kwa kutufadhili,iwe ni harakati zetu za kuhifadhi mikoko au kufuga nyuki. Twahitaji wafadhili zaidi kupanua shughuli zetu,” akasema Bi Chuo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Lamu Women Alliance (LAWA), Bi Raya Famau aliwapongeza wanawake wa Lamu, hasa wale Waswahili wa asili ya Wabajuni kwa kuibuka na miradi ya kujiendeleza maishani,ikiwemo kilimo cha nyuki na uhifadhi wa mikoko.
Bi Famau aliahidi ushirikiano wake katika kuona kwamba wanawake wengi zaidi Lamu wanaibukia miradi ya kuwawezesha kujitegemea maishani.

“Twashukuru. Miaka ya hivi punde tumejionea akina mama Waswahili Wabajuni wakijitoa jikoni na kusaidia waume wao majukumu. Tukijituma sawa na waume wetu tutawaondolea msongo wa mawazo unaotokana na kung’ang’ana kwao kuzikimu familia zetu peke yao. Tuwajibike. Tukifanya hivyo waume wetu watatuheshimu hata zaidi,hivyo mapenzi kunoga majumbani mwetu,” akasema Bi Famau.

  • Tags

You can share this post!

Kindiki sasa abatilisha notisi zilizopandisha ada za...

Polo atoweka kazini ghafla kukwepa bosi wa kumtupia mistari...

T L