• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 5:55 PM
Mtaalamu wa IT auza biskuti akiendelea kusaka ajira

Mtaalamu wa IT auza biskuti akiendelea kusaka ajira

NA TOBBIE WEKESA

MSIMU huu ambapo Wakenya wanajiunga na ulimwengu kusherehekea Krismasi na kuendelea na shamrashamra za kuukaribisha Mwaka Mpya, wanafanya hivyo kwa kujumuika na familia zao.

Lakini Samuel Mbuthia,35, haoni haja ya kuenda nyumbani kujiunga na familia yake isipokuwa kuwasukumia kidogo alichoweka kama akiba na kuwaombea dua njema.

Isitoshe, anasema kuna majukumu mengi yanayomkodolea macho.

Mkazi huyu wa Bahati katika Kaunti ya Nakuru anasema licha ya kutunukwa shahada mbalimbali alizojizolea katika vyuo vikuu na taasisi mbalimbali, hali imemlazimu kuchuuza bidhaa mjini Nakuru.

Akilimali ilikumbana naye akiuza biskuti.

“Mimi nilifanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne mwaka 2007 na nikapata alama ya B+. Nina digrii ya Teknolojia ya Habari almaarufu IT kutoka Chuo Kikuu cha Dedan Kimathi,” alieleza Bw Mbuthia.

Baada ya kufuzu kwa digrii, Bw Mbuthia anasema alianza kukanyaga lami kusaka kazi lakini milango ya kazi haijawahi kumfungukia.

Ingawa hivyo, Bw Mbuthia hakufa moyo. Ndiposa aliamua kujiunga na taasisi nyingine, mojawapo ikiwa ni Taasisi ya Sensei kusomea uendeshaji wa matingatinga ya kuunda barabara. Juhudi zake za kupata kazi katika sekta ya ujenzi wa barabara zingali hai, akisema ni mwingi wa subira.

Bw Mbuthia ni baba wa watoto wawili na kwa sasa anasema biashara ya kuchuuza biskuti na maji jijini Nakuru inamfaa pakubwa akisubiri na kutumai kwamba ipo siku ambayo itakuja na baraka za kazi kuhusu maswala aliyosomea.

“Kwa siku mimi huunda Sh300. Ingawaje mahitaji ni mengi, ninaMshukuru Mungu. Inashinda kukaa bure. Pesa hizi husaidia kukidhi mahitaji ya familia yangu. Shida tu nahofia kesho yangu na ya familia yangu,” alieleza Bw Mbuthia.

  • Tags

You can share this post!

Mama aliyejeruhi wanawe aliambia kanisa ‘kuna...

Hakikisha raia wana noti mfukoni, Rais aambiwa

T L