• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Hakikisha raia wana noti mfukoni, Rais aambiwa

Hakikisha raia wana noti mfukoni, Rais aambiwa

NA TITUS OMINDE

VIONGOZI wa kidini kutoka North Rift wametoa wito kwa Wakenya kuendelea kuwa na mshikamano na umoja licha ya hali ngumu ya kiuchumi huku wakimtaka Rais William Ruto kutumia Mwaka Mpya 2024 kama mwaka wa kuangazia ufufuaji wa uchumi.

Wakizungumza wakati wa ibada za Krismasi katika makanisa mbalimbali North Rift, viongozi hao wa kiroho pamoja na waumini waliofika maabadani walisema wangependa kuona Rais Ruto akitafuta hekima kutoka kwa Mungu ampe mawazo ya jinsi ambavyo anaweza kusimamia mchakato wa kisera na kiutawala kukabiliana na changamoto za nyakati ngumu za kiuchumi.

Walisema wangependa kuona raia nchini wakiwa na pesa mfukoni mwaka 2024.

Askofu Wilson Kurui, mlezi wa wahudumu wa injili Uasin Gishu alisema rais Ruto anahitaji mazingira ya amani ili kufufua uchumi.

Askofu Kurui alitoa changamoto kwa Rais Ruto kujiepusha na siasa za kulipiza kisasi badala yake azingatie mahitaji ya raia wa kawaida.

“Kama Kanisa tunasali ili Rais wetu aongoze Wakenya katika mazingira ya amani na ushauri wangu kwake ni kuachana na siasa za utengano. Ajikusuru kutumikia nchi kama mtumishi wa Mungu kwa kuzingatia sana ufufuaji wa uchumi,” alisema Askofu Kurui.

Alitoa changamoto kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuanza kufanya kazi na Rais Ruto kwa manufaa ya nchi.

“Kiongozi wa upinzani, Bw Odinga asahau yaliyopita na akubali kumpa sapoti Rais Ruto kwa ustawi wa nchi yetu,” akaongeza Askofu Kurui.

Kwa upande wake Askofu Zablon Malema wa Kanisa la Hallelujah mjini Eldoret, aliwaomba Wakenya wote kuendelea kumtakia mafanikio Rais Ruto ili kuishi maisha ya amani ambayo yataleta maendeleo.

Askofu Malema alitoa ushauri kwa kiongozi wa nchi kwamba aongoze bila ukabila, hasa katika uteuzi wa maafisa wa serikali kwa kubuni nafasi za ajira kwa Wakenya kutoka jamii zote.

“Rais Ruto lazima awe macho ili kuhakikisha kuwa kuna usawa katika uajiri ili kuhakikisha sekta za ajira zinaonyesha sura ya Kenya na kuepuka ukabila katika ajira,” alisema Askofu Malema.

  • Tags

You can share this post!

Mtaalamu wa IT auza biskuti akiendelea kusaka ajira

Usifakamie mlo tu kujaza tumbo – mtaalamu

T L