• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Pesa zipo katika mimea ya mafuta, asema mmiliki wa kiwanda

Pesa zipo katika mimea ya mafuta, asema mmiliki wa kiwanda

NA PETER CHANGTOEK

PAUL Mwangi ni mhandisi wa masuala ya zaraa, ambaye alihudumu katika Shirika la Ustawishaji wa Kilimo (ADC) kwa muda mrefu, kabla kustaafu 2019.

Mwangi, ambaye pia ni mkuzaji wa mimea ya soya na alizeti, katika eneo la Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia, amekuwa akiongeza thamani kwa mimea ya alizeti, soya na canola, kwa kutengeneza mafuta ya kupikia.

Mkulima huyo anasema kwamba, mkewe alikuwa na shida ya kupata lishe za kuku zilizo bora, na wakaamua kujitengenezea lishe wenyewe. Hivyo basi, ikawalazimu kutumia alizeti kuzitengeneza lishe hizo.

Katika harakati za kuzitengeneza lishe hizo, wakagundua kuwa kulikuwa na mafuta mengi yaliyokuwa yakitoka kwa alizeti, na hivyo, wakaamua kuinunua mashine ya kutengeneza mafuta.

“Hapo awali tulikuwa na mashine tuliyonunua kwa Sh20,000, iliyokuwa ikichakata kilo 60 tu. Kwa sasa, tuna kiwanda kizima,” asema Mwangi, akiongeza kuwa, uwekezaji wote ni wa kima cha Sh16 milioni.

Anaongeza kuwa wao huchakata tani 90 za canola, soya na alizeti kwa mwaka mmoja.

Mhandisi Paul Njuguna Mwangi akionyesha jinsi mashine huchakata mafuta ya kupikia. PICHA | PETER CHANGTOEK

Ananuia kuchakata tani 300.

Hata hivyo, yeye huikuza mimea ya alizeti na soya kwa shamba ekari kumi tu, na hununua malighafi kutoka kwa wakulima wengine.

Anadokeza kuwa, ana wakulima takriban 100 aliowapa kandarasi ili wawe wakimuuzia alizeti, canola na soya.

Kwa msimu uliopita, alikuwa akiwalipa wakulima wa alizeti Sh36-Sh40 kwa kilo moja ya zao hilo, huku akiwalipa wale wanaozalisha soya Sh50 kwa kilo na Sh60 kwa kilo moja ya canola.

Kwa mujibu wa Mwangi ni kuwa, wakulima wanaozalisha alizeti ni wengi, ikilinganishwa na wale wanaozalisha canola na soya.

Anasema kuwa, hununua alizeti kutoka kwa wakulima walioko katika maeneo ya Teso Kaskazini, Bungoma na Trans Nzoia.

Aidha, hununua soya kutoka maeneo ya Kitale na Bungoma. Pia, hununua canola kutoka maeneo ya Uasin Gishu na Mau Narok.

Kampuni yake inajulikana kama Elgon Fine Enterprises Limited, na hutengeneza bidhaa zenye nembo Elsun.

Pia, mjasiriamali huyo, mwenye umri wa miaka 63, hutengeneza lishe aina tofauti tofauti za kuku, na kuuza kilo moja kwa Sh40 na Sh45.

Huziuza bidhaa zake kwa madukakuu kama vile; Transmart Supermarket (Kitale), Transmart Supermarket (Eldoret), Woolmart Supermarket (Nakuru) na Hygienic Supermarket (Nakuru).

Mwangi, ambaye ni baba wa watoto watatu wakubwa, hutengeneza mafuta na kupakia kwa vitoma vya lita moja, lita mbili na lita tano.

Huuza lita moja ya mafuta ya canola kwa Sh300 na lita tano kwa Sh1,500. Vilevile, huuza lita moja ya mafuta ya alizeti kwa Sh300 na lita tano kwa Sh1,400.

“Huuza lita moja ya mafuta ya soya kwa Sh280, na lita tano kwa Sh1,300,” aongeza Mwangi, ambaye ana wafanyakazi saba.Hata hivyo, kuna baadhi ya changamoto ambazo amewahi kuzipitia, kama vile kupanda kwa gharama ya umeme na “ushuru mwingi unaotozwa na serikali.”

Mwangi anawashauri wale ambao wangependa kujitosa kwa biashara kama hiyo kuwa na uvumilivu na kutoogopa kuwekeza.“Si lazima uanze kwa kutumia pesa nyingi, bali unaweza kuanza kwa pesa kidogo.

Mipango yetu ya baadaye ni kupanua na kushindana na kampuni kubwa vilivyo,” aongeza.

Anawashauri wakulima waikuze mimea inayotumika kutengeneza mafuta, ili iwasaidie kuongeza riziki, badala ya kutegemea mahindi pekee.

Anaoongeza kuwa, mimea kama hiyo hutia nitrojeni kwa udongo.

  • Tags

You can share this post!

UDA yaondoa ada ya uteuzi kwa wanaoishi na ulemavu

UFUGAJI: Mtandao waimarisha soko la nguruwe wake

T L