• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 3:13 PM
UFUGAJI: Kuku wa kienyeji bado smaku sokoni

UFUGAJI: Kuku wa kienyeji bado smaku sokoni

Na PAULINE ONGAJI

LICHA ya kuwa amesomea masuala ya uhalifu na usalama chuoni, mbali na kuwa kwa sasa anajihusisha na biashara ya kuuza spea za magari, ameamua kujitosa katika nyanja ya ufugaji wa ndege.

Raphael Mbugua, 29, mkazi wa eneo la Tinganga, Kaunti ya Kiambu, anaendesha shughuli hii katika ardhi ya ekari robo tatu, inayomilikiwa na wazazi wake.

Anajihusisha na ufugaji wa ndege wa nyama, mayai na mapambo. Baadhi ya ndege anaowafuga ni pamoja na kuku wa kienyeji na wa nyama, bata na bata bukini na kanga. Na japo amekuwa akijihusisha na ufugaji kwa kipindi cha mwaka mmoja pekee, tayari anavuna vinono.

“Kwa kawaida mimi hupata kati ya mayai 80 na 120 kila siku. Kwa mwezi, 2400 na 3000. Kwa upande mwingine, mimi huuza kati ya jogoo 10 na 15 kila mwezi,” aeleza, huku akidokeza kwamba wateja wake ni maduka na hoteli za mtaani, vile vile marafiki.

Kinachomtofautisha na wafugaji wengine wa ndege, ni kwamba hatumii chakula cha ndege kilichoundwa kwa kemikali.

“Hasa mimi hutumia bidhaa kama vile mahindi, ngano na mchele, masalio ya mbegu za alizeti baada ya mafuta kuondolewa, shayiri, omena na magugu miongoni mwa bidhaa zingine za kiasili,” aeleza.

Kwa kawaida yeye hupata bidhaa hizi kutoka mashambani na madukani.

Raphael Mbugua akionyesha kuku anaowafuga. PICHA | EVANS HABIL

“Kwa upande wa mchele na ngano zilizovunjwavunjwa, mimi huziunua kutoka viwandani, ilhali magugu mimi huyapata shambani,” adokeza.

Mbugua asema kinachomsukuma kuwapa ndege wake chakula cha kiasili, ni ili kuhamasisha watu umuhimu wa kudumisha afya njema kupitia chakula wanachokula.

“Kumekuwa na visa vya matatizo ya kiafya kama vile uzani mzito kupindukia na maradhi mengine yanayosababishwa na mtindo wa kimaisha, matatizo ambayo yamekuwa yakihusishwa na aina ya chakula tunachokula,” aeleza.

Kulingana na Alvine Ochiel kutoka Idara ya Sayansi ya Wanyama katika Chuo Kikuu cha Egerton, ni rahisi kuunda vyakula vya ndege wako kwani viungo vinapatikana kwa urahisi mtaani au vijijini.

Hata hivyo, asema kwamba, mbinu hii pia ina udhaifu kwani ni vigumu kutimiza viwango vinavyohitajika vya virutubisho kuambatana na umri wa ndege wako.

Safari yake Mbugua katika ufugaji wa ndege ilianza 2020. Alianza kwa kuatamisha trei nne za mayai alizokuwa amenunua kutoka kwa rafikiye mkulima.

“Baada ya shughuli hii nilipokea vifaranga 89. Aidha, nilinunua ndege 40 waliokomaa kutoka kwa wakulima hapa mtaani,” aeleza. Mwanzoni asema, ilikuwa shughuli ya kupitisha muda.

“Hata hivyo, baada ya kurejea nyumbani kutoka ng’ambo na kukumbana ‘lockdown’ ya Covid-19, niliamua kujihusisha kikamilifu,” aeleza.

Muda ulivyozidi kusonga, marafiki zake na waliokuwa wakimfahamu walianza kuagiza nyama na mayai kutoka kwake. Hii asema ilimpa ari ya utaka kujihusisha zaidi na ufugaji.

Ni suala lililomsukuma kujituma zaidi na kuanza kuchunguza jinsi angeweza kuendeleza biashara yake kwa kutambua fursa ambazo zingemletea mapato zaidi kama vile uuzaji wa mbolea na vifaranga, vile vile kutoa huduma za kuatamiza.

Hata hivyo, asema, mambo hayajakuwa rahisi kwani kama biashara ingine ile, amelazimika kukabiliana na changamoto za hapa na pale, kama vile mauzo duni na gharama ya juu ya kujiundia vyakula vya ndege. “Kuna wakati ambapo nalazimika kutembea tembea katika mashamba na viwanda ili kupata bidhaa zinazotumika kuunda vyakula hivi.”

Katika upande mwingine, asema, ukosefu wa baadhi ya bidhaa shambani mwake kutokana na sababu tofauti kama vile mabadiliko ya hali ya anga. “Hii bil ashaka huathiri viwango vya uanguaji. Hatimaye, hii inaathiri idadi ya ndege wanaokomaa hadi kiwango cha ukomavu.”

Lakini licha ya changamoto hizi, Bw Mbugua asema sasa amelenga kupanua biashara yake na kuhusisha kuzalisha viaranga na mayai kwa viwango vikubwa, kuanzisha kituo cha mafunzo ya utafiti, na kuuza bidhaa zake ng’ambo.

Ushauri wake kwa yeyote anayetaka kujitosa katika ufugaji wa aina hii ni “fanya utafiti wa kutosha, kuwa subira na soma vya kutosha ili ujifunze.”

You can share this post!

ZARAA: Amegundua siri ya kukuza matunda yanayosakwa mno

Mtambo wa kuangua mayai wawaletea tuzo

T L