• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Mtambo wa kuangua mayai wawaletea tuzo

Mtambo wa kuangua mayai wawaletea tuzo

Na RICHARD MAOSI

MIAKA mitatu iliyopita, vijana Samwel Mwangi na Peter Mwangi kutoka eneo la Posta Njoro, Kaunti ya Nakuru walipata pigo baada ya kupoteza vifaranga wapatao 60 kutokana na hali mbaya ya hewa.

Ndiposa wakaja na uvumbuzi wa kifaa ambacho kinaweza kuangua na kulea vifaranga katika mazingira mazuri yenye kiwango cha kadri katika hatua ya kuendeleza kilimo biashara mashinani.

Ni kifaa ambacho kimefanya wawili hao kutuzwa Shirika la Young African Enterprenuers Innovators Organisation kutokana na juhudi zao kuangazia matatizo yanayowakumba wafugaji.

Kifaa chenyewe wamekipatia jina la Incubrooder kwani kinaweza kufanya majukumu mawili kwa wakati mmoja, ikiwa ni kuangua mayai , pamoja na kulea vifaranya.

Hiki ni kifaa ambacho kinaweza kupima joto na kiasi cha unyevu (humidity) ikizingatiwa kuwa sehemu mbalimbali zimewekewa kipepeta hewa, huku zikiwekewa trei zinazotumika kama mahali pa kutotolesha mayai.

Aliongezea kuwa mashine hii ni rahisi kutumia kwani imegawika katika sehemu tatu, ya kwanza ikiwa ni ile ya kutotolesha vifaranga, kulea na ile ya kukusanya mabaki ya lishe.

Peter aliambia Akilimali kuwa ni uvumbuzi ambao hatimaye umewatengenezea ajira, mbali na kuwasaidia wakulima wengi mashinani ambao hawajakuwa na mbinu mwafaka ya kutunza vifaranga.

Hatimaye, walitengeneza kiwanda cha Plotus Technology ambacho kinashughulika na utengenezaji na usambazaji wa mitambo hii ambayo inaendelea kupata umaarufu.

Samwel anakumbuka namna safari yao ilianza akiwa mwanafunzi wa mwaka wa tano kutoka Chuo Kikuu cha Moi alipokuwa akisomea taaluma ya uhandisi.

Samwel Mwangi (kushoto) na Peter Mwangi kutoka eneo la Posta Njoro, Kaunti ya Nakuru, wakionyesha mtambo wa kutotolesha na kulea vifaranga. PICHA | RICHARD MAOSI

Mara tu baada ya kufuzu alirejea kwao nyumbani kusaka ajira lakini alipokosa kufanikiwa, aliamua kuwekeza kwenye mradi wa kufuga kuku ambapo alinunua vifaranya 60 kutoka Shirika la Kenya Agricultural Research Institute.

Mradi haukufanya vyema kwani vifaranga wake wote waliaga, ndiposa akaamua kumsaka rafiki yake wa utotoni, Peter ambaye pia alikuwa amefuzu kutoka Tecnical University of Kenya, ila hakuwa amebahatika kupata kazi.

“Tulishirikiana katika hatua ya kwanza kubadilishana mawazo kabla ya kuungana na CoElib ambayo inapatikana ndani ya Chuo Kikuu cha Egerton, na chini ya kipindi cha mwaka mmoja tulipokea mafunzo ya kutosha kubuni kifaa hiki,” akasema.

Mnamo 2020 walizindua kifaa chao kwa mara ya kwanza kwa umma na kumuuzia mkulima kwa Sh10,000 ambaye alisifia utendakazi wa kifaa chenyewe na hata kuwaelekeza wakulima wengine.

Peter anasema ni kifaa ambacho kimeundwa kwa namna ya kipekee kwani kinaweza kuangua aina mbalimbali ya mayai kama vile kanga, kuku, bata na hata bata bukini.

Pili kinaweza kusawazisha kiwango cha joto na unyevu kwa mujibu wa operesheni za kisayansi.

Aidha, kinyume na aina nyingine ya mitambo ambapo humlazimu mkulima kugeuza mayai kila wakati ili kila sehemu iweze kupata joto, kifaa hiki ni tofauti kwani kina uwezo wa kuyageuza mayai chenyewe.

Huja na kimo tofauti ili kukidhi mahitaji ya wakulima wote. Kinaweza kubeba kati ya mayai 98 hadi 700 na kimeboreshwa kutunza vifaranga kuhakikisha wanabakia kuwa hai kwa asilimia 99.

Ni mtambo ambao Peter anasema huuzwa kati ya Sh45,000-120,000 kulingana na mahitaji ya mkulima mara nyingi wakilenga wakulima wadogowadogo ambao wanapata changamoto za kulea vifaranga.

Aidha anasisitiza kuwa mradi wa kulea vifaranga unahitaji mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwalisha vyema, ambapo chakula chao huendana na umri ili wawe na maendeleo mazuri ya ukuaji.

You can share this post!

UFUGAJI: Kuku wa kienyeji bado smaku sokoni

NJENJE: Pakistan yaibuka mtumizi bora wa chai ya Kenya,...

T L