• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Utalipia kupata huduma katika Huduma Center, Waziri mpya wa Utumishi wa Umma atangaza

Utalipia kupata huduma katika Huduma Center, Waziri mpya wa Utumishi wa Umma atangaza

NA LABAAN SHABAAN

WAKENYA watazidi kuchimba mifukoni kutoa pesa zaidi serikali ikitangaza misururu ya malipo kwa huduma za serikali katika vituo vya Huduma Center.

Waziri mpya wa Utumishi wa Umma Moses Kuria, akipokea mikoba ya uongozi kutoka kwa Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa, alipasua mbarika ya mzigo zaidi kwa mlipaushuru.

Bw Kuria alisema matozo hayo yatatumiwa kuendesha shughuli za kutoa huduma za serikali.

“Kwa muda mrefu, Wakenya wamekuwa wakifurahia huduma hizi bila kulipia. Sasa, hakuna cha bure, lazima ulipie,” alisema akieleza jukwaa dijitali la biashara litahitaji kujisimamia.

Kwa mujibu wa aliyekuwa waziri wa hivi punde zaidi wa biashara, hatua hii itapunguza shinikizo za uhitaji wa pesa kutoka kwa Wizara ya Fedha.

Miongoni mwa huduma zitakazotozwa ada ni usajili upya wa leseni za udereva, nakala ya kitambulisho cha kitaifa, na Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).

Si hizo tu, pia huduma ya usajili wa Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF), Mkopo wa Karo ya Elimu ya Juu (HELB), usajili wa makundi, fomu za thibitisho kutoka kwa polisi (police abstracts) na kadhalika.

Mtaalamu wa Uchumi na Masuala ya Fedha Eliud Mutwiri anasema serikali hutoza wananchi ushuru ili iweze kutoa huduma hizi bila kupokea ada zaidi kutoka kwa mlipaushuru.

“Mlipaushuru ana malimbikizo ya kodi nyingi ambayo anang’ang’ana nazo na kama serikali inaendelea kuwatoza pesa, utakuwa mzigo mkubwa watakaoshindwa kumudu,” Bw Mutwiri alisema akitaja Sheria ya Fedha ya 2023 ambayo imezidisha viwango vya ushuru kwa wananchi ambao wanateta kuhusu hali ngumu ya uchumi.

Kadhalika, Bw Mutwiri ametaja kuwa mlipaushuru tayari amelipia huduma hizi kupitia matozo mbalimbali katika shughuli za biashara zikiwemo kodi ya kuongeza thamani (VAT) na ushuru katika mishahara.

“Kumtoza Mkenya fedha zaidi hapa ni kumfanya kulipia huduma mara mbili,” alieleza.

Programu ya Huduma Kenya ilianzishwa 2013 ili kuwezesha utoaji wa huduma mbalimbali za serikali katika kitengo kimoja maarufu ‘Huduma Center.’

  • Tags

You can share this post!

Vidosho kutoka Uganda, Tanzania wafurika Rift Valley...

Pasta Ng’ang’a asema hawezi kupitisha gari lake la...

T L