• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Vidosho kutoka Uganda, Tanzania wafurika Rift Valley kukamua wazee bonasi ya chai

Vidosho kutoka Uganda, Tanzania wafurika Rift Valley kukamua wazee bonasi ya chai

NA RICHARD MAOSI

UTAPELI wa kimapenzi, ndiyo picha ya hali halisi katika kaunti za Bomet, Kericho, Kisii, Nandi na Mlima Elgon wakulima wa majanichai wakianza kupokea bonasi kuanzia wiki hii.

Vidosho wanaendelea kumiminika mjini Kericho tayari kutafuna jasho la wakulima hao.

Mikahawa ambayo kwa muda haijakuwa ikipokea wateja wengi, kwa sasa imefurika huku magari ya uchukuzi katika barabara za kuelekea Kisii na Kericho zikiwa zimepandisha nauli.

Kwa wakazi hapa, hii ni hali ya kawaida ambapo wanakiri kuwa warembo kutoka nchi jirani za Tanzania na Uganda, vilevile, wamekuwa wakijumuika na wenzao wa Kenya kuvuna.

Kwa upande mwingine, wakazi wa eneo la Konoin, Kaunti ya Bomet wameungama kuingiwa na tumbojoto, wakidai makahaba wanatumia mitego mingi kuwanasa na kuwaibia wanaume.

“Badala ya kukodisha vyumba vya malazi mbali na mji, wanapangisha karibu na ploti zetu ili kuwadhibiti wanaume kwa muda mrefu, kuhakikisha wanawakamua kila kitu,” anasema Bi Ann Chebet muuzaji wa mananasi eneo la Ngoina Road.

Aidha, kituo cha kibiashara cha Mogosiek, muda kama huu vyumba vya kulala huwa vimejaa na kuwalazimu baadhi ya walevi kutumia vichaka.

“Makahaba wachanga na wale wenye umri mkubwa hufika hapa mapema na kukodisha vyumba ambapo huwapeleka wateja wao,” anasema Robert Kipkemoi mkazi wa Mogogosiek.

Isitoshe, wamiliki wa baa na mikahawa wameongeza mtaji kutokana na mazingira mazuri ya kufanyia bishara na wanatarajia idadi kubwa ya wateja.

Kipkemboi anasema ni jambo ambalo limekuwa likirudisha familia nyingi nyuma kimaisha.

Ikumbukwe kuwa Konoin ni eneo linalopatikana katika Kaunti ya Bomet ambapo idadi kubwa ya wakulima wa majani chai huwa wanatoka.

  • Tags

You can share this post!

Huyu rafiki ataniambukiza tabia za usagaji?

Utalipia kupata huduma katika Huduma Center, Waziri mpya wa...

T L