• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Pasta Ng’ang’a asema hawezi kupitisha gari lake la kifahari barabara ya Luthuli

Pasta Ng’ang’a asema hawezi kupitisha gari lake la kifahari barabara ya Luthuli

SAMMY WAWERU

PASTA mtatanishi James Maina Ng’ang’a kwa mara nyingine amekuwa gumzo la mitandao ya kijamii, kufuatia matamshi yake kuhusu barabara tajika ya Luthuli, Jijini Nairobi.

Kwenye video inayosambaa mitandaoni, Mhubiri huyo wa Kanisa la Neno Evangelism amesema kamwe hawezi kupitia Luthuli Avenue na gari lake la kifahari kwa kile ametaja kama ‘kujaa vituko na uhuni’.

Video hiyo ya sekunde 24, Bw Ng’ang’a anasikika akidai barabara ya Luthuli itasababisha gari lake la hadhi kukwaruzwa na matatu.

Isitoshe, pasta huyo ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akirusha cheche kali za maneno kwa serikali, umma na wafuasi wake, amesema anahofia mikokoteni kumharibia gari.

“Luthuli…Luthuli hata siwezi kupita hapo na gari langu kwa sababu litakwaruzwa na matatu na hizo mikokoteni iko hapo,” anasema.

Mchungaji Ng’ang’a anasikika akitoa ushuhuda wake wa hapo awali wa barabara hiyo ya jijini iliyo na shughuli nyingi akisema aliwahi kupitia hapo na gari lake aina ya Mercedes na mmoja wa askari akamuonya dhidi ya mazingira hayo.

Anafichua kwamba licha ya kuwa na gari la bei ghali, liligongwa na matatu zinazobebea Luthuli Avenue.

“Nilipitia hapo zamani na Mercedes ikagongwa, hata Inspekta aliniuliza; sasa hii unakuja nayo hapa ya nini?” anasimulia.

Anaongeza, “Wahubiri wanakunywa chai hapo na mandazi kubwa kama masikio ya ndovu.”

Majuzi, Pasta Ng’ang’a alinukuliwa kupitia video akikashifu mmoja wa waumini wake aliyetoa sadaka ya Sh500 akitaka aombewe.

“Mwingine jana alinipa Sh500 akaniambia nikumbuke watoto wake, nikumbuke wajukuu wake…500…Hata nitawakumbuka namna gani mimi sasa…500…Hata hakuna mafuta ya gari ya 500, hiyo labda ya watu wa pikipiki. Hiyo ni ibada gani sasa?” alielezea kushangazwa kwake na mchango huo wa sadaka.

Aidha, Ng’ang’a alisema ibada ya Sh500 inafanywa na waganga wa Nairobi, akimaanisha wahubiri, wanaoitisha mbegu – sadaka ili kuombewa.

Pasta huyo katika kisa tofauti alitangaza kwamba hataki kwenye kanisa lake washirika wenye Digrii, akihoji ndio wamechangia ulimwengu kuwa na matatizo kutokana na uvumbuzi wa teknolojia za kisasa.

Kauli zake zinazidi kukosolewa mitandaoni.

  • Tags

You can share this post!

Utalipia kupata huduma katika Huduma Center, Waziri mpya wa...

Waraibu wa asali wanavyouziwa mchanganyiko wa sukari na...

T L