• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wakulima kutozwa ushuru wawasilishapo mazao kwa vyama vya ushirika

Wakulima kutozwa ushuru wawasilishapo mazao kwa vyama vya ushirika

NA CHARLES WASONGA

WAKULIMA na wafugaji sasa ndio tabaka la Wakenya ambao wataathiriwa na mzigo mzito wa kutozwa ushuru baada ya serikali kupendekeza ushuru kwa mazao watakayowasilisha kwa vyama vya ushirika au asasi nyingine zilizosajiliwa.

Hii ni kulingana na Taarifa kuhusu Sera ya Bajeti (BPS) ya mwaka wa 2024 iliyochapishwa na serikali kupitia Wizara ya Fedha mnamo Desemba 18, 2023.

Kulingana na BPS hiyo, inayopatikana katika wavuti wa hazina ya kitaifa wa www.treasury.go.ke, hatua hiyo inalenga kuisaidia serikali kukusanya pesa zaidi za kuiwezesha kufadhili Ajenda yake ya Kiuchumi almaarufu, Bottom Up Economic Transformation (Beta).

Ushuru huu unaojulikana kwa Kimombo kama ‘Withholding Tax’ utakatwa na vyama vya ushirika kutoka kwa malipo ya wakulima walioviuzia mazao hayo kabla wao (wakulima) kupokea pesa hizo. Hali ni hivyo kwa wafugaji watakaowasilisha bidhaa kutokana na mifugo hasa maziwa.

Ushuru huo unatarajiwa kuwaongezea wakulima na wafugaji mzigo ikizingatiwa kuwa wao hutozwa ada mbalimbali na vyama hivyo vya ushirika, kampuni za kusindika mazao ya shambani pamoja na serikali husika za kaunti.

“Hazina ya Kitaifa inatalii njia bora za kukusanya ushuru kutoka kwa sekta ya kilimo, kama vile kupitia kuanzishwa ushuru maalum wa malipo kwa mazao yatakayowasilishwa kwa vyama vya ushirika au makundi mengine yaliyosajiliwa,” inaeleza taarifa hiyo ya BPS.

Kulingana na stakabadhi hiyo, sekta ya kilimo ni miongoni mwa zile ambazo ni vigumu kutoza ushuru (yaani Hard to Tax Sector) sawa na zile ya Juakali na Biashara za Mitandaoni.

Endapo pendekezo hili la serikali litapitishwa na bunge, ina maana kwa wakulima wa mazao kama vile kahawa, majanichai, pareto, mahindi, wafugaji wa ng’ombe wa maziwa, miongoni mwa wengine ambao huuza mazao yao na bidhaa kupitia vyama vya ushirika, wataathirika na ushuru huu mpya kuanzia mwaka wa kifedha wa 2024-2025.

Hata hivyo, Wizara ya Fedha inayoongozwa na Profesa Njuguna Ndung’u imewahakikisha wakulima kuwa “hatua zitachukuliwa kuwakinga wale wenye mapato ya chini.”

Kulingana na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) ‘withholding tax’ ni mtindo wa ukusanyaji ushuru ambapo anayelipa mapato fulani hukata ushuru anapowalipa wale waliopaswa kuyapokea.

Kisha mlipaji mapato hayo huwasilisha ushuru uliokatwa kwa Idara ya Ushuru zinazokusanywa nchini (Domestic Taxes Department) ndani ya siku tano baada ya kuukata.

  • Tags

You can share this post!

Maskwota 3,500 hatarini kuanza mwaka mpya bila makazi

Ruto, Gachagua wapata ‘D’ na ‘E’...

T L