• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 10:55 AM
Polisi watano wakamatwa na maafisa wa EACC kwa kuitisha hongo kutoka kwa madereva

Polisi watano wakamatwa na maafisa wa EACC kwa kuitisha hongo kutoka kwa madereva

NA SIAGO CECE

MAAFISA watano wa polisi akiwemo Inspekta wa Polisi wamekamatwa huku maafisa kutoka kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) wakiimarisha msako dhidi ya polisi wa trafiki wanaoogelea kwa ufisadi kwenye barabara kuu humu nchini.

Katika taarifa mnamo Jumanne, EACC ilisema imemkamata Inspekta wa Polisi Joash Rotich Koriese wa kituo cha polisi cha Kisumu Central ambaye alikuwa akiitisha hongo ya Sh500,000 ili kuondoa mashtaka dhidi ya mwendeshaji wa lori la trela na kuachilia bidhaa zake alizozuilia.

“Alijaribu kukataa kukamatwa na maafisa wa EACC,” tume hiyo ikasema kwenye chapisho kwa mtandao wa X (zamani Twitter).

Maafisa wa tume hiyo pia waliwafumania polisi wanne katika Kaunti ya Machakos akiwemo Debora Ngila, (Naibu Kamanda), Rosemary Nyokabi, Robert Kabiru na Christine Chebon wakiitisha pesa kutoka kwa madereva katika Barabara Kuu ya Thika-Garissa.

Kukamatwa kwa watu hao kumeibuka baada ya EACC kuanzisha msako dhidi ya maafisa wafisadi katika kitengo cha polisi wa trafiki nchini.

Afisa mkuu wa EACC Twalib Mbarak alikuwa ameonya kwamba tume hiyo hivi karibuni inakabiliana na polisi wanaochukua hongo kutoka kwa madereva, akidai kuwa vizuizi vingi vimekuwa vituo vya kutoa hongo bila kuficha.

“Tunaomba udhibiti wa sheria za trafiki ufanyike kielektroniki kama hatua ya mageuzi, kwani ufisadi katika barabara za Kenya, ambao sasa umebadilika kutoka hongo hadi tamaa, unadhoofisha sura ya nchi na unapaswa kukoma,” Bw Mbarak alionya.

Alisema operesheni hiyo itaendelea, akiwataka madereva kuzingatia sheria na kanuni za trafiki na kuripoti kesi zozote za madai ya hongo kwa EACC kupitia laini ya bure ya 1551.

Hata hivyo, hatua ya EACC kuwakamata maafisa wa polisi imekabiliwa na hisia tofauti huku baadhi ya Wakenya wakisema tume hiyo badala yake inafaa kuwatafuta samaki wakubwa wa ufisadi nchini.

Wakenya wengine wameorodhesha vizuizi kadhaa kwenye barabara kuu wakiomba tume hiyo ichukue hatua dhidi ya polisi wanaokusanya hongo.

Hapo awali Bw Mbarak alisema Wakenya wanaotoa hongo wanakwepa taratibu ndefu za mahakama na wangependelea kulipa kiasi kidogo cha pesa kwa kuvunja sheria za trafiki.

  • Tags

You can share this post!

Waziri Soipan Tuya aomba mahakama iagize mume wake kutoa...

Wataalam waonya kuhusu athari za tabianchi kwa kilimo na...

T L