• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
AKILIMALI: Hakujua sabuni, mafuta kutoka kwa maziwa ya mbuzi yana wateja wengi

AKILIMALI: Hakujua sabuni, mafuta kutoka kwa maziwa ya mbuzi yana wateja wengi

Na MARY WANGARI

TOM Kiragu, 40, alipoanzisha kampuni yake kwa jina Cleo Nature, takriban miaka mitano iliyopita, alichotaka tu ni kupata tiba kwa mwanawe aliyekuwa amehangaishwa na maradhi ya chunusi tangu utotoni mwake.

Mhitimu huyo aliyefuzu na Shahada katika Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Hertfordshire, Uingereza, sasa anamiliki kampuni inayounda bidhaa za aina yake za sabuni na mafuta kwa kutumia maziwa ya mbuzi kama malighafi.

Alichukua hatua ya kufungua Cleo Nature mnamo 2017, na tangu hapo, hajawahi kutazama nyuma.

Akilimali ilipomtembelea afisini mwake eneo la Kenya Industrial Estate, Kaunti ya Embu, tulimpata amezama katika shughuli ya kupakia katoni za sabuni na mafuta ya kiasilia tayari kusafirishwa kwa wateja waliokuwa wameagiza.

Huku akitabasamu, anatufahamisha kwamba, jina la kampuni yake Cleo Nature, linatokana na simulizi ya malkia wa mwisho wa Egypt, Cleopatra, aliyejizolea umaarufu kwa kuwa “mwanamke mrembo zaidi kuwahi kutembea kwenye changarawe ya jangwa hilo.”

Yote haya yalianza kama juhudi za kupata suluhisho la kudumu kwa matatizo ya chunusi yaliyokuwa yamehangaisha familia yake kwa muda mrefu, huku wakilazimika kwenda hospitali moja baada ya nyingine, bila mafanikio.

Alianza kufanya utafiti kuhusu maradhi ya ngozi ikiwemo njia bora ya kuyatibu.

Hapo ndipo waligundua manufaa chungu nzima ya sabuni na mafuta yaliyotengezwa kwa kutumia malighafi ya kiasilia kwenye ngozi.

Cleo Nature ilianza kimchezomchezo tu kutokana na jamaa yetu aliyekuwa amehangaishwa na chunusi tangu alipozaliwa. Tulizuru hospitali nyingi, tukapatiwa dawa na mafuta ya kila aina kudhibiti ugonjwa huo bila mafanikio,” akaeleza.

Sabuni na mafuta ya kiasilia yanasheheni manufaa tele ikiwemo kutumika kama virutubishi vya ngozi, kudhibiti ngozi yenye mafuta mengi na kulinda ngozi iliyokauka, jinsi anavyotufahamisha.

Furaha yao kufuatia uvumbuzi huo ilikatizwa ghafla walipogundua hawangeweza kupata bidhaa hizo katika soko nchini.

Tom Kiragu, 40, ambaye hutengeza sabuni kwa kutumia maziwa ya mbuzi anayosema yanasheheni manufaa tele kwa ngozi. Picha/ George Munene

Akiwa mfanyabiashara mbunifu jinsi alivyo huku akiwa amechoshwa na kero ya chunusi, alikata kauli ya kuanza kujiundia bidhaa hizo kwa matumizi ya nyumbani, kwa kutumia maarifa aliyokuwa amepata kupitia utafiti wake.

“Ilichukua muda kukusanya vifaa vyote vilivyohitajika. Tulianza kwa kuunda sabuni ya nazi kwenye roshani ya nyumba yetu. Tulitumia sabuni hiyo kumwogesha mtoto na tulishangaa sana ilipomponya,” anaeleza.

Akaongeza: “Tuliwapa bidhaa hizo baadhi ya watu tuliofahamu walikuwa wanasumbuliwa na chunusi na matokeo yalikuwa ya kutia moyo. Watu walianza kuagiza bidhaa hizo. Jioni moja tulipokuwa tukitengeza sabuni tulipata wazo la kuanzisha biashara ya kuunda sabuni na hivyo ndivyo Cleo Nature ilivyoanza mnamo 2017.”

Kabla ya kujitosa kwenye ulingo wa biashara, Kiragu aliwekeza pakubwa katika utafiti na kuwashirikisha wataalam kutoka nyanja ya Matibabu na Afya ya Ngozi ili kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa zake kwa wateja, kama anavyoeleza.

“Wataalam tuliowashirikisha walitufahamisha kuhusu manufaa tele ya kemikali za Hydroxyl Acids (AHAS) na Caprylic Acid zinazopatikana kwa wingi katika maziwa ya mbuzi. Kemikali hizi zinafahamika kwa uwezo wake wa kuondoa seli za ngozi zilizokufa na kuruhusu mwonekano wa ngozi changa zaidi,” anasema.

Pia anasema maziwa yana madini chungu nzima.

“Maziwa ya mbuzi pia yanasheheni kiasi kikubwa cha madini aina ya Selenium yanayowezesha ukuaji wa ngozi yenye afya,” anafafanua.

Anaeleza kuwa bidhaa zake za sabuni huundwa kwa kutumia mchakato wa baridi kuunganisha mafuta ya kiasilia.

“Mchakato huo huifanya sabuni na mafuta hayo kuwa na manufaa kwa watu wenye ngozi inayoathirika upesi, ngozi iliyoharibika pamoja na watu wanaotaka kudumisha ngozi changa,” anasema.

Kuhudhuria warsha kadhaa kuhusu uundaji wa sabuni vilevile kulimsaidia Kiragu kutia makali ujuzi wake na kujihami vilivyo kwa maarifa.

Alianzisha biashara yake kwa kutumia mtaji wa Sh1 milioni alizokopa kwenye benki.

Aidha, Cleo Nature hukuza mmea wa castor viungani mwa mji wa Embu na kiwanda cha kuunda mafuta ya castor yanayochanganywa na mafuta mengineyo ya kiasilia kama vile Jamaican Oil, tea tree na rosemary, ambayo yamethibitishwa kisayansi kuwa na manufaa tele kwa ngozi na nywele.

“Castor Oil inasheheni Ricinocleic acid na Omega 6 zinazoimarisha ukuaji wa nywele ndefu, na kuzuia nywele kukatika,” anasema.

Hata hivyo, hakuna kilichomwandaa kwa changamoto tele zilizomsubiri katika sekta ya biashara chipukizi SME.

“Tulipata changamoto hasa kuhusu nafasi ya kuweka biashara yetu kwa sababu wapangaji wengi walikuwa wanaitisha kodi ya miezi sita kabla ya kuturuhusu kutumia majengo yao. Tulibahatika kupata sehemu ya kuanzisha biashara yetu na kujikuza mjini Embu ambapo tunajiendeleza hadi leo hii,” anaeleza.

Masharti makali ya serikali kuhusu kupata kibali cha kuanzisha biashara ni changamoto nyingine iliyomkosesha usingizi.

Jinsi anavyofafanua, ilijumuisha malipo ya hadi Sh300,000, kiasi ambacho, kwa hakika, ni ghali mno kwa biashara yoyote chipukizi.

Anasema kuwa wateja anaolenga hasa ni “watu wanaotamani kudumisha mtindo wa maisha unaozingatia afya bora kwa kutumia bidhaa zisizokuwa na kemikali, pamoja na watu wanaokabiliwa na matatizo ya ngozi kama vile chunusi na upele.

Kwa bei ya jumla, bei ya sabuni ni kati ya Sh130 na 400 huku mafuta yakiwa kati ya Sh350 na 1050.

Huuza sabuni kati ya Sh350 na Sh600 (retail) nayo mafuta kati ya Sh250 na Sh1550.

Tasnia ya mitandao ya kijamii, matangazo kwa njia ya mdomo na wateja walioridhika ndizo mbinu kuu anazotumia kutangaza biashara na kuwavutia wateja zaidi.

“Tulianza biashara hii tukiwa wawili lakini tumekua na kufikia timu ya watu 15 kwa sasa. Tunatumai kufikia watu 20 kufikia mwisho wa mwaka huu,” anaeleza.

Sawa na biashara nyingine yoyote, Kiragu amekumbana na pandashuka anuai, jinsi anavyotupasha.

“Tatizo kuu linalotukabili kwa sasa ni kuhusu jinsi ya kusambaza bidhaa zetu katika kila sehemu kote nchini. Tunahitaji kuongeza kiwango cha uzalishaji hatua inayohitaji kuongeza kiasi cha mtaji jambo ambalo ni ngumu hasa wakati huu ambapo benki zinakataa kufadhili SME kutokana na janga la Covid-19,” anaeleza.

Licha ya changamoto hizo, hajakata tamaa huku akitumai katika siku za usoni kumiliki “Kampuni Nambari moja ya kuunda Sabuni na Bidhaa Asilia za Nywele Barani Afrika kwa kupanua mipaka yake nje ya Kenya.”

“Bidhaa za Cleo Nature zinapatikana katika maduka maarufu ya kuuzia dawa na bidhaa za urembo nchini,” anasema.

[email protected]

You can share this post!

AKILIMALI: Mwalimu mwenye bidii ya mchwa ashauri vijana...

Ruto atawezana?