• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 12:03 PM
AKILIMALI: Mkulima hodari wa blueberries ajikakamua kuziba pengo la uhaba wa matunda hayo

AKILIMALI: Mkulima hodari wa blueberries ajikakamua kuziba pengo la uhaba wa matunda hayo

Na SAMMY WAWERU

BLUEBERRIES ni matunda yenye virutubisho tele vya Vitamin C na Potassium, na yenye chembechembe zinazosafisha damu na mishipa.

Ni matunda adimu hapa nchini Kenya, yakipatikana katika maduka ya jumla hususan yaliyoko mitaa ya kifahari jijini Nairobi kama vile Lavington, Karen na Runda.

Maduka yanayoyauza, kilo moja inagharimu kati ya Sh3,000 – Sh4,000.

Upungufu hasa unatokana na idadi ya chini mno ya wakulima wanaoyakuza nchini.

California ni miongoni mwa majimbo yanayofahamika kuyakuza Magharibi mwa Amerika, na linaloongoza katika uzalishaji ulimwenguni.

Uholanzi katika Bara Ulaya pia hukuza blueberries, ingawa kwa uchache.

Kutopatikana kwa mbegu au miche ya matunda haya kunatajwa kama kizingiti kikuu kwa wakulima kuyakuza.

Orodha ya wakulima wachache nchini waliojituma kuangazia pengo lililopo la upungufu wa blueberries ikitolewa, Wilson Ndung’u hatakosa kujumuishwa.

Huyakuzia katika Kaunti ya Kiambu, eneo la Limuru na mtaa wa Lavington jijini Nairobi.

Aliingilia kilimo cha blueberries mwaka wa 2019, na anasema ni matunda asilia yenye mapato ya kuridhisha.

Licha ya upungufu wa matunda haya kuwepo nchini, Ndung’u anasema Kenya ina hali bora ya anga kuyazalisha.

“Mengi ya matunda haya tunayouziwa yametoka nje ya nchi. Kenya tuna uwezo kuyakuza. Yanastawi katika mazingira yenye joto na yanayopokea mvua ya kutosha,” aelezea.

Mbali na kuyapanda Nairobi na Kiambu, mkulima huyu wa haiba yake pia amezindua mradi mwingine Malindi, Kaunti ya Kilifi.

“Humo ninapania kuyalima kwenye ekari moja,” Ndung’u asema.

Lavington, ana kiunga cha miche, eneo la Limuru akiwa na kivungulio cha neti kuyazalisha.

Mbinu za upanzi

Huku kero ya ukosefu wa mbegu na miche ikizuia wenye ari kuyakuza, Ndung’u anasema kilimo cha blueberries ni rahisi.

Anaorodhesha mbinu kadha wa kadha katika mchakato mzima kufanikisha upanzi.

“Unaweza ukapanda mbegu, ambazo ni za kununua kutoka nje ya nchi. Huchukua muda wa hadi miaka mitano kukomaa na kuzalisha matunda.

“Njia nyingine, ni ya kuyapandikiza (grafting), ambapo matawi ya yanayoendelea kukua hutumika. Huchukua kipindi cha miaka miwili kuanza kuzaa matunda,” afafanua.

Ndung’u amekumbatia mfumo wa air layering.

“Hii ni mbinu ya kutumia matawi. Hufungwa kwa kutumia Sphagnum moss, na kuyatunza kwenye vyungu,” aelezea, akiongeza yanapochipuka yanapaswa kuhamishiwa eneo la upanzi mara moja.

Sphagnum moss, ni mfumo wa matumizi ya malighafi asilia unaosaidia kuhifadhi maji kwenye vyungu.

Akisifia mfumo anaotumia, mkulima huyu anasema huanza kuchana maua na kutunda miezi minne baada ya upanzi.

“Kwa kutumia mbinu ya air layering, mimea haishuhudii msongo wakati wa kuihamishia eneo la kuitunzia,” asema.

Mfumo mwingine ni wa miche, Ndung’u akidokeza mwamba anashirikiana kwa karibu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mimea na Uimarishaji Mifugo (Karlo) kuizalisha.

“Karlo inanisaidia kujamiisha na kuzidisha,” asema.

Lengo lake ni kupata karibu miche laki moja (100,000).

Huku kikwazo kwa wakulima wengi kikiwa ukosefu wa mbegu na miche, Vincent Ochieng kutoka Karlo anasema wenye nia kuyakuza wanaweza kupata miche kwa taasisi hiyo.

Mtaalamu Ochieng aidha anashauri wakulima kupata mbegu na miche kutoka kwa asasi au wapandaji walioidhinishwa.

“Mbali na Karlo, pia wanaweza kuzipata kutoka kwa Taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis) au wazalishaji walioidhinishwa,” mwanasanyansi huyu ahimiza.

Anasema vigezo bora vya udongo vikiafikiwa kilimo cha blueberries ni rahisi, hakihitaji matunzo ya hali ya juu na matunda haya yanastahimili athari za wadudu na magonjwa.

Wilson Ndung’u akiendelea kujibidiisha kusaidia kuziba pengo la uhaba wa matunda haya nchini, anasema changamoto inayomzingira kwa sasa ni ukosefu wa maji safi na ya kutosha.

“Ombi langu kwa serikali na wadau husika katika sekta ya kilimo, wanisadie kupata maji,” anasema.

Mkulima huyu hutegemea maji ya mvua, ambapo huyavuna kwa kutumia matangi.

You can share this post!

Wanaraga Kabras Sugar moto balaa ligini Kenya Cup

Wanavoliboli wa Kenya Prisons wakanyaga DCI ligi ya kina...