• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Wanavoliboli wa Kenya Prisons wakanyaga DCI ligi ya kina dada kusalia kileleni

Wanavoliboli wa Kenya Prisons wakanyaga DCI ligi ya kina dada kusalia kileleni

Na AGNES MAKHANDIA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya voliboli ya kinadada Kenya Prisons waliandikisha ushindi wao wa tano mfululizo baada ya kuzima maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwa seti 3-1 katika uwanja wa magereza ya Kamiti jijini Nairobi mnamo Agosti 14.

Prisons walijipata mashakani katika seti ya kwanza waliyopoteza kwa alama 25-16 kabla ya kuamka kutoka usingizini na kuzoa seti tatu zilizofuata kwa alama 25-17, 25-21 na 25-21, mtawalia.

Vipusa wa kocha Josp Barasa watakamilisha msimu wa kawaida dhidi ya wanajeshi wa KDF mnamo Agosti 15. Wamezoa alama 15 baada ya kujibwaga uwanjani mara tano.

Naibu kocha wa Kenya Prisons, Azenga Mavisi alikiri kuwa walianza vibaya na kutumia muda mwingi kutulia, lakini anafurahia kutia kapuni alama tatu.

Wakati huo huo, washiriki wapya Nairobi Prisons walizoa ushindi wao wa kwanza msimu huu kwa kuduwaza wazoefu KDF 3-0 (25-23, 25-18, 25-14). Kocha Salome Wanjala alieleza kufurahishwa na ushindi wa timu yake.

Alisema, “Ukuta tulioweka pamoja na kupokea mipira vyema ndizo idara zilizotusaidia kutwaa ushindi huu. Mashambulizi yetu hayakuwa mazuri. Natumai tutakamilisha ligi kwa kishindo tutakapokutana na Nairobi Water hapo Jumapili. Water ni timu nzuri, lakini lengo letu ni kupata alama tatu katika mechi hiyo.”

Nairobi Prisons ina alama tatu baada ya kujibwaga uwanjani mara tano nayo Water inavuta mkia bila ushindi.

Katika mechi nyingine zilizochezewa Kamiti, nambari mbili KCB ilifunga msimu kwa kuzima Water 3-0 (25-14, 25-11, 25-18) nao mabingwa wa zamani Kenya Pipeline wakapepeta KDF 3-0 (25-16,25-12, 25-14) na kufikia DCI iliyo na alama tisa.

DCI na Pipeline watamenyana Agosti 15 katika mechi itakayoamua nani kati yao atamaliza katika nafasi ya tatu.

Mwisho wa msimu wa kawaida hapo Agosti 15, timu nne za kwanza zitajikatia tiketi ya kushiriki mechi za muondoano za kuamua bingwa wa mwaka 2021. Awamu ya muondoano itaandaliwa Agosti 26-29 katika ukumbi wa KPA Makande katika kaunti ya Mombasa.

Ratiba ya Agosti 15: Nairobi Prisons vs Nairobi Water (10am), KDF vs Kenya Prisons (12pm), Kenya Pipeline vs DCI (2pm).

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

You can share this post!

AKILIMALI: Mkulima hodari wa blueberries ajikakamua kuziba...

Man-United wamtwaa rasmi beki Raphael Varane kutoka Real...