• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:50 AM
Auntie Jemimah: Nilishika mimba nyingine miezi mitatu baada ya kupoteza ujauzito

Auntie Jemimah: Nilishika mimba nyingine miezi mitatu baada ya kupoteza ujauzito

Na MWANDISHI WETU

MTANGAZAJI na mwigizaji Mercy Nguri almaarufu Auntie Jemimah amesema kuwa alishika mimba miezi mitatu baada ya kumpoteza mwanawe.

Akizungumza kwenye mahojiano, Jemimah alisema kuwa siku ya kusherehekea kina mama duniani, Mei 14, ilikuwa spesheli sana kwake.

Anakumbuka 2021, alimpoteza mwanawe aliyefariki akiwa tumboni mwake na siku kama hiyo mwaka jana, 2022 ilikuwa imegubikwa na huzuni mwingi sana kwake.

“Niliwaona wengi wakisherehekea lakini bado nilikuwa na huzuni nyingi sababu ya kifo cha mtoto wangu. Hata hivyo, mwaka huu nimejazwa na furaha sana kwani niliweza kusherehekea pamoja na mtoto wangu,” akafichua.

Jemimah anasema kuwa wakati mwingine anamwangalia mtoto wake anafurahia sana na haamini kuwa yeye ni malaika wake.

“Nilikaa miezi mitatu kabla sijashika mimba tena. Kama daktari amekushauri kujaribu tena tafadhali jaribu,” akasema.

Hata ingawa alijifungua mtoto wake akiwa mfu, Jemimah anasema kuwa hawakupata jibu haswa ni kwa nini lakini anashuku ugonjwa wa kisukari cha mimba (gestational diabetes) kwani alikuwa na ugonjwa uo huo alipokuwa na mimba ya mtoto wake.

“Hatukufanya uchunguzi mwingi wakati huo. Ukiwa na ujauzito wa aina hiyo, unaweza jifungua mtoto mkubwa sana, afie tumboni au ukishajifungua mtoto aage dunia,” akaeleza.

Isitoshe, Jemimah anasema kuwa kina mama hawana maarifa ya kutosha wanaposhika mimba huku watoto wao wakifariki.

“Watu waliongea vibaya sana baada ya kumpoteza mtoto wangu huku wakisema kuwa picha nilizokuwa nimeposti mtandaoni ndizo zilivutia macho mabaya,” anakumbuka.

Hata hivyo, Jemimah anasema kuwa kuna sababu zingine nyingi zinazomfanya mwanamke kupoteza mimba yake na Wakenya wanapaswa kuwa na maarifa ya sababu hizo pia.

“Nilimwambia tunayefanya kazi naye kuwa nitachukua likizo fupi ili niweze kujifungua. Nilipoenda nyumbani nilikula chajio na nilipokuwa nikitulia nikahisi maji yakinitoka. Nilimpigia daktari wangu akanieleza nifike hospitalini haraka iwezekanavyo,” anasema.

Anaendelea, “Madaktari walijaribu kuhisi moyo wa mtoto wangu ukidunda bila mafanikio. Kufichua kutosikia moyo wa mtoto wangu kuliniumiza sana. Nilirudishwa kwenye wodi mpaka siku iliyofuata hadi pale nilipoweza kujifungua. Hakuna kitu cha uchungu kama kujifungua mtoto aliyefariki.”

 

  • Tags

You can share this post!

Zingatia mambo haya uishi na watu vizuri

Akaunti 30 za pasta Ezekiel Odero kufungwa kwa siku 30,...

T L