• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 7:50 AM
BAHARI YA MAPENZI: Mume, mke hawawezi ‘urafiki wa kawaida’

BAHARI YA MAPENZI: Mume, mke hawawezi ‘urafiki wa kawaida’

SIZARINA HAMISI Na BENSON MATHEKA

KWAMBA wanandoa wanaweza kuwa huru kwenda kuvinjari na marafiki zao wa jinsia tofauti wakiwa peke yao ni jambo lenye utata kiasi.

Wengi wanasema suala hili ni zito kwani mwanaume ama mwanamke anaweza kujidanganya kwamba hawezi kupata mvuto wa kimapenzi kwa huyo rafiki, lakini binadamu tumeumbwa tofauti.

Ni kawaida kwa mwanamke ama mwanaume kuvutiwa na mtu wa jinsia nyingine na wakati mwingine kuwepo na msukumo wa ziada wa tamaa ya kuchangamsha mwili.

Tafiti nyingi duniani zimegundua kuwepo na msukumo na mhemko wa tamaa za ngono kwa wanaume. Majibu kadha wa kadha ya tafiti hizo yamekuwa yakitoa majibu sawa, ikiwemo suala la maumbile ya mwanamume na namna anavyompokea mwanamke yoyote machoni pake.

Wanasema uaminifu katika ndoa ni kipawa, kwani wakati mwingine wanandoa wanaweza kujiamini kwamba watakuwa waaminifu, lakini hali huwa tofauti pale anapojikuta katikati ya hali ya kutoa uamuzi wa kuonja ama kuacha.

Wengi wanasema uhusiano wa kirafiki kwa wanandoa huwa ni sawa na bahati nasibu ya pata potea. Mwanaume ama mwanamke anaweza kujikuta anajidanganya mwenyewe, anadanganya mwenzake na kudanganya wengine na hatimaye kujipata kwenye shida. Hili la kudai kuwa inawezekana kwa mwanaume na mwanamke wasio katika mapenzi au wasio katika mchakato wa kuanza mapenzi kuwa marafiki wa karibu, wasiri na wa ndani, ni jambo lenye ukakasi.

Wapo akina kaka ambao wameniambia kwamba hawawezi kukubali kamwe wake zao kutoka na marafiki wanaume kiholela. Kwani wanasema wanajuana kama wanaume, suala la urafiki tena kwa mwanamke ambaye ni mrembo huwa ni mara chache sana kubakia katika huo urafiki.

Tena wanaelewa tabia ya uwindaji waliyo nayo wanaume wenzao kiasi kwamba ni vigumu kuwaamini kuwa pekee na wake zao.

Kwa upande mwingine akina dada pia wanasema haitakuwa rahisi kukubali kwamba waume zao watoke na marafiki zao wanawake bila wao kuwepo. Nao pia wanaeleza kwamba sababu kubwa ni kwamba hawana imani na waume zao, sababu lolote linaweza kutokea.

Wanaume wana kawaida ya kutongoza wanawake waliowazoea wakiwemo rafiki za wake zao kwa kuwa huwawia rahisi wakati wa kujieleza. Inaelezwa kwamba ni mara chache sana mwanamume kutongoza mwanamke anayekutana naye kwa mara ya kwanza.

Waume wengi hawana kawaida hiyo hasa waliooa, kwanza hufikiria mtu anayetongoza hamfahamu kiundani huenda anaweza kuwa ndugu au mtu wa karibu na mkewe, huona afadhali kwa mtu anayemjua au anayefanya naye kazi ofisi moja.

[email protected]

URAFIKI ni kitu kizuri lakini unafaa kuwa na mipaka hasa kwa masuala ya mahusiano. Mtu anafaa kuheshimu mke au mume wa rafiki yake na hapo ndipo urafiki wa dhati unapoanzia.

Inafaa kueleweka kuwa urafiki huwa wa mtu na mwingine lakini sio kwa wake au waume zao. Hivyo basi, mtu anaporuhusu mke au mumewe kuzoeana na rafiki yake huwa anajiweka katika hatari kubwa.

Hatari ninayozungumzia hapa ni uwezekano wa mkeo au mumeo kuchepuka na mtu unayedhani ni rafiki unayemwamini.

Hatari hii, huwa inaongezeka mazoea hayo yanapogeuka kuwa vikao katika maeneo ya burudani. Unapata mtu akikubali mkewe kuketi na mwanamume rafiki yake kilabuni wakiteremsha pombe, siku moja, ya pili, ya tatu halafu aamini kwamba, pamoja na hisia na vituko vinavyoandamana na ulevi, hakuna kitakachotokea kati yao.

Hapa ninazungumzia mtu kusalitiwa na rafiki anayemwamini kwa dhati kiasi cha kumwacha azoeane na mume au mkewe hadi wawe wakivinjari. Ni sawa na yule jamaa mpumbavu aliyeacha chui na mbuzi wake katika zizi moja.

Bila shaka njaa ikimkeketa matumbo chui atageuza mbuzi kuwa kitoweo. Mtu akitaka heshima idumu kati yake na rafiki yake, huwa anaweka mchumba wake mbali naye, hili naweza kusisitiza milele.

Kuna watu wanaojifanya marafiki huku wakimezea mate wake au waume wao. Wiki jana, nilishuhudia kisa cha mwanamume aliyeachwa na mkewe wa miaka sita akaolewa na rafiki yake wa miaka kumi aliyekuwa amempa uhuru wa kutangamana naye bila mipaka.

Visa vya wanawake kulia wakipokonywa waume na marafiki wao vimekuwa vikiripotiwa kote, ikiwemo katika makanisa ambapo mapasta wamekuwa wakizini na wake wa waumini wao wanaowaamini kama viongozi wa kiroho.

Ikiwa hali kama hii inatokea kanisani ambapo kinywaji cha pekee kinachokubaliwa ni divai takatifu, je itakuwaje mtu akiruhusu mume au mke wake kujivinjari na rafiki yake katika kilabu au eneo lingine la burudani wakiwa wawili tu ambako kuna mvinyo na pombe kali inayofanya mwili kuwaka kwa hisia?

Sisemi kwamba watu hawafai kuwatambulisha wake au waume zao kwa marafiki wao. Ni vyema kufanya hivyo lakini waweke mipaka ili kuepuka mazoea. Udhaifu mkubwa wa binadamu ni kutumbukia katika majaribu.

Ni watu wachache wanaoweza kujidhibiti na kustahimili majaribu ya kutumbuizana wakiwa wamelewa. Tumeona yakifanyika kwa watu na yanaweza kufanyika unapozoea kuruhusu mkeo au mumeo kujivinjari na rafiki.

Ukiona ukuruba umeota kati ya mtu wako na rafiki yako, gutuka mapema kwa sababu ni muda tu ubaini huyo rafiki amekuwa akikusaliti kwa kuchovya asali yako.

Ilinde asali yako kwa kuweka mipaka kati ya mtu wako na marafiki wako la sivyo utajuta.

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Inauma kukataliwa lakini heri kujiondoa

Nottingham Forest wazamisha chombo cha Liverpool katika EPL

T L