• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 9:17 PM
BAHARI YA MAPENZI: Nafasi ya wazazi katika ndoa ya wanao

BAHARI YA MAPENZI: Nafasi ya wazazi katika ndoa ya wanao

SIZARINA HAMISI Na BENSON MATHEKA

NI ukweli usiopingika kwamba wazazi wana nafasi na mchango katika maisha ya watoto wao hasa kwenye suala la mahusiano na hatimaye ndoa.

Wazazi wetu wanajua mengi na wamepitia mengi, kwani wao wametangulia kuona ulimwengu kabla yetu sisi.

Hivyo wana uzoefu wa kutosha katika maisha na uhusiano kwa ujumla.

Mara nyingi wachumba wanapokuwa katika hatua za awali za matayarisho ya ndoa, ni kawaida kuwashirikisha wazazi katika mipango, matarajio na hata hatua za awali za maisha ya ndoa.

Hata hivyo wanandoa wanapoanza maisha ya pamoja, wanakuwa na vipaumbele vyao na yale waliyopanga kuyatekeleza kama mke na mume. Wakati huu kama wanaingiliwa katika kupanga na kuamua inawezekana kuleta mvutano na wale wanaoingilia utaratibu waliojiwekea.

Kwa upande mwingine, tumeshuhudia wazazi wakisababisha tafrani kwa wapendanao. Wapo wanathubutu kuzuia ndoa na kuwapangia vijana wao maisha na mengine ambayo kwa kiasi kikubwa huwa hayawahusu. Inapotokea mvutano wa wazazi katika suala la ndoa, tatizo linakuwa kubwa zaidi kwa wanandoa. Kwani huwa wanayumbishwa na mwisho wa siku wanakosa kitu cha kufanya.

Watakubali kuoana halafu mmoja wao atengwe au ndoa ivunjike. Wataathirika kwa sababu wao wanaweza kuwa wamekubaliana kwa hali yoyote lakini wazazi wa upande mmoja kwa sababu wanazozijua wao, wanaweka pingamizi na ndoa inasuasua kuanzia hapo.

Wazazi ni muhimu katika maisha ya watoto wao, lakini pale wanapofikia muda wa kuanza maisha na wenzao, hawana budi kuwapatia nafasi. Nafasi kubwa ya wazazi ipo katika mwongozo wakati wa matayarisho ya ndoa, na kutoa maelekezo ya unapaswa kufanyaje kumpata mchumba ambaye anaweza kuwa nawe kwa muda mrefu kutokana na mwenendo na tabia na imani pia.

Imani na miongozo mbalimbali ya kiimani inasema kwamba mwanamume na mwanamke wataacha wazazi wao na kuanza maisha yao pamoja, hivyo msichana na kijana wanapoamua kufunga ndoa, nafasi ya wazazi haitakiwi kuwa kubwa katika maisha ya wanandoa hawa.

Hata hivyo inaweza kuwa vigumu kwa baadhi ya wazazi kukubali na kuzoea mabadiliko, kwamba binti ama kijana ameondoka nyumbani na kuanza maisha yake.

Wapo wazazi wanaodai wapatiwe hiki ama kile bila kutambua kwamba sasa nao wana jukumu la kutunza na kukuza boma lao.

Na pale wanandoa wanapokataa kusaidia hiki ama kile inakuwa ni mvutano na wazazi ukifuatiwa na lawama tele.Inaweza pia ikawa ni vigumu kuwa na wakwe wa upande wa pili wa wanandoa, kwani pia muunganiko wa wazazi wa pande hizi mbili unaweza kuwa ni changamoto nyingine kwa wanandoa.

Katika uhalisia, huwa inasikitisha pale ambapo inajulikana wanandoa wenyewe hawana shida yoyote, isipokuwa mzazi ama wazazi ndio wamekuwa mwiba unaodunga ndoa ya wahusika. Kwamba wao ndio wanakuwa waanzilishi wa nyufa kwenye ndoa ya watoto wao.

Muhimu kwa wanandoa ni kuwa makini, kwani zipo ndoa zilizoporomoka sababu ya kuendekeza matakwa na mahitaji ya wazazi.

[email protected]

WAZAZI wa pande zote mbili yaani, upande wa mke na wa mume, ni muhimu sana kwa wanandoa.

Kama haingekuwa wao, mtu hangepata mume au mke. Hata hivyo, kumekuwa na vilio vingi watu wakilalamika kwamba wazazi au wakwe zao huwa wanageuka mwiba kwa ndoa zao.

Wanawake wamelia kwamba waume zao wamekuwa wakipokea maagizo kuhusu jinsi ya kuendesha familia zao kutoka kwa wazazi wao, na hasa mama zao huku wanaume wakililamika kuwa wake zao wamekuwa wakiwaasi kufuatia ushauri au maagizo wanayopata kutoka kwa wazazi na hapa tena, mama zao. Matokeo ya kupokea maagizo kutoka kwa wazazi kuhusu masuala muhimu ya ndoa ni chanzo cha kuporomoka kwa uhusiano wa mume na mkewe.

Ushauri wa wazazi ni muhimu sana lakini ni juu ya mtu kufanya uamuzi unaofaa kwa ndoa yake. Mwanamume anayemwambia mkewe kila wakati kwamba “mama amesema” , huwa ni mwanamume kasoro mume wa mtu.

Vile vile, mwanamke anayefanya anayoambiwa na baba yake bila kujali athari zake kwa ndoa yake, ni mwanamke kasoro mke wa mtu.

Kabla ya kuachia mzazi wako kukuelekeza, unafaa kukumbuka kuwa ndoa ni kati ya watu wawili walio na umri wa miaka 18 na zaidi waliokutana kwa hiari na ambao inachukuliwa wanafaa kufanya maamuzi peke yao.

Watu wanapokutana, kujuana na kuanza safari ya mapenzi hadi ndoa huwa wako wawili na wazazi huja kwa picha wakati wa posa kukamilisha mipango ya ndoa.

Wale wanaoingiza wazazi wao katika maamuzi kuhusu ndoa zao huwa wamepoteza dira na ikipotea, chombo huenda mrama.

Inashangaza kama sio kuchekesha kuona mwanamume akiamuliwa na mama yake idadi ya watoto ambao mkewe anapaswa kuzaa au akiambiwa na baba yake asikubali mkewe aendelee na kuajiriwa ilhali alimuoa akiwa kazini. Baadhi ya wanawake pia wamekuwa wakiamuliwa na mama zao kuhusu idadi ya watoto wanaofaa kuzaa na waume zao au hata wakati wa kupata mimba.

Nikubalieni niseme kwamba hali kama hii imekuwa ikizua mzozo katika ndoa, chanzo kikiwa ni ukosefu wa hekima na busara kwa kuruhusu wazazi kutawala ndoa ya watu wawili waliokutana wakiwa wazima na kukubaliana wao wenyewe kuishi pamoja.

Kufanyiwa maamuzi na wazazi ni sawa na kufanya ndoa kuwa chombo kinachoendeshwa na mtu aliye nje asiyefahamu joto au baridi iliyoko ndani yake.

Nasisitiza kuwa mchango wa wazazi katika ndoa japo ni muhimu na haufai kupuuzwa, hawafai kuwa waamuzi wa mwelekeo au mipango ya ndoa yenu. Na sisemi watu wasitii wazazi wao, ila kunafaa kuwa na mipaka ili wasibadilike kuwa wamiliki wa ndoa ya wana wao.

Wazazi wanafaa kukumbatia hekima na kuacha wanao kujenga familia zao kwa njia wanayodhani ni bora kwao na kuingilia kati wanapoombwa kufanya hivyo. Vinginevyo, utaharibu ndoa ya binti au bin wako.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Kuwa mjanja, sishindane na mtu wako!

MALEZI KIDIJITALI: Chagulia mtoto wako teknolojia inayomfaa

T L