• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
MALEZI KIDIJITALI: Chagulia mtoto wako teknolojia inayomfaa

MALEZI KIDIJITALI: Chagulia mtoto wako teknolojia inayomfaa

NI kweli kuwa teknolojia imenyima wazazi muda wa kuwa na watoto wao nao watoto wamegeukia dijitali kujaza pengo lililoachwa na wazazi wao licha ya kuwa wengi wao wanafanyia kazi zao nyumbani.

Kwa baadhi ya wazazi, wanalazimika kufanya kazi ili kukidhi mahitaji ya familia zao. Wanaume huwa wanashinda wakichunguza barua pepe zao kuona iwapo wamejibiwa ombi la kandarasi wanayonuia kupata pesa za kulipia wanao karo ya shule nao akina mama wanashinda wakifuatilia bidhaa wanazouza kupitia mtandao.

Wataalamu wa malezi dijitali wanasema kwamba ili wazazi wasionekane kuwapuuza watoto wao wanapojipata katika hali kama hii, wanafaa kuwachagulia teknolojia ya kuwafaidi ili kuwaepusha na hatari zinazoongezeka za kuzama katika mtandao.

“Ikiwa unalazimika kufanyia kazi nyumbani na kukosa muda wa kuwa na mtoto wako, usimuache awanie kila aina ya bidhaa za dijitali, tovuti au mitandao ya kijamii. Mchagulie mtoto wako teknolojia, tovuti na mitandao ya kushughulika nayo wakati unapoendelea kufanya kazi ukiwa nyumbani,” asema mtaalamu wa malezi dijitali Salma Salim.

Salma asema katika hali hii, hakuna atakayepoteza kati ya mzazi na mtoto.

“Utakuwa ushindi kwa kila upande. Mzazi atafanya kazi yake bila kuwa na hofu ya mwanawe kutumbukia katika hatari za teknolojia naye mtoto atakafaidika na busara ya mzazi wake na hatahisi ametelekezwa,” aongeza.

Hata hivyo, anasisitiza wazazi wanafaa kutenga muda japo mfupi wa kuwasikiliza watoto wao licha ya mageuzi ya teknolojia yanayofanya nyumba kuwa afisi na vituo vya kufanya biashara mtandaoni.

“Kuchagulia mtoto anachopaswa kufanya na kufuatilia kwenye mtandao ni jukumu ambalo mzazi anapaswa kupatia kipaumbele. Sio chaguo, ni jambo la lazima kwa wazazi wanaojali wanao enzi hizi za dijitali,” asisitiza.

  • Tags

You can share this post!

BAHARI YA MAPENZI: Nafasi ya wazazi katika ndoa ya wanao

JAMVI LA SIASA: Ruto angemtumia Kalonzo kuatika mbegu ya...

T L