• Nairobi
  • Last Updated May 14th, 2024 1:09 PM
PENZI LA KIJANJA: Kuwa mjanja, sishindane na mtu wako!

PENZI LA KIJANJA: Kuwa mjanja, sishindane na mtu wako!

NA BENSON MATHEKA

“KUDUMISHA penzi kunahitaji ujanja kila siku, usihisi tu umetosheka kwa kuwa unapata kila kitu. Na ujanja huo unategemea unavyomjua mtu wako kwa hivyo siwezi kukushauri umfanyie Saimo ninavyomfanyia Ngugi,” Selina alimweleza Wambui alipomuuliza siri ya kuwa na Ngugi kwa miaka kumi bila kuvurugana.

Walipozama kwa mazungumzo, Wambui aligundua kwamba tatizo lake na Saimo lilikuwa kushindana na kutaka kutoshana naye.

“Ilikuwa ni kawaida yangu kushindana na Saimo na kutaka tuwe sawa. Hilo lilisabababisha mgogoro kati yetu ambao wakati mwingine ulilipuka na kuwa vita,” Wambui akafunguka.

Baada ya kutafakari maneno ya Selina, aliamua kubadilisha tabia ili kuokoa uhusiano wake na mwanamume anayesema ni wa ndoto yake na hangetaka kumpoteza.

Laula Andanyi, mtaalamu wa masuala ya mahusiano na mshauri wa wanandoa katika Live Solution Center, anasema ushindani unaharibu uhusiano wa kimapenzi hasa kati ya mke na mume.

“Inaibuka kuwa watu wengi hawatambui nafasi zao katika ndoa. Unapata mke anataka kuwa katika kiwango kimoja na mumewe kuhusiana na maamuzi. Nataka kuwaambia akina dada kuwa wana haki ya kuwapa wanaume zao maoni na kuwaachia uamuzi. Wanachoweza kukosoa ni matokeo au athari za uamuzi wao na kwa njia ya heshima,” asema Laula.

Mtaalamu huyu anasema kwamba hata wanaume wanafaa kushauri wake zao kuhusu masuala yanayowahusu na kuwaacha wafanye uamuzi bila kuwashinikiza.

“Kuna masuala ya wanawake ambayo wanaume wanapaswa kuwapa ushauri tu na kuwaacha wafanye maamuzi yao wenyewe,” asema.

Muhimu kabisa, aeleza Laula ni kila mmoja kuelewa jinsi ya kushughulika na mtu wake.

“Kuna mwanamume anayesaka maoni ya mkewe kabla ya kununua ploti na kukubaliana naye na kuna wengine ambao wakiamua hawaoni haja ya kushirikisha wake zao. Ukijua mtu wako ana tabia hii, kuwa mjanja ili usiguze waya moto na kuharibu uhusiano wenu kwa sababu ya kitu ambacho ungeepuka,” aeleza Laula.

Hata hivyo, Pasta Dominic Waswa wa kanisa la Ebenezar, jijini Nairobi anasema ujanja wa kudumisha uhusiano shwari ni kila mtu kujua nafasi yake katika ndoa.

“Ukijua nafasi yako, hautashindana na mwenzako. Utashika laini yako na kutekeleza majukumu yako inavyohitajika kuu likiwa ni kutambua kila mmoja ana haki zake,” asema huku akikubaliana na Laula kwamba kila mtu ni tofauti na mwingine.

  • Tags

You can share this post!

Sijachoka kupiga vita maadui wa nchi, asema Raila

BAHARI YA MAPENZI: Nafasi ya wazazi katika ndoa ya wanao

T L