• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
BAHARI YA MAPENZI: Ni sawa mkeo kustarehe na marafiki?

BAHARI YA MAPENZI: Ni sawa mkeo kustarehe na marafiki?

SIZARINA HAMISI Na BENSON MATHEKA

UBORA wa uhusiano wa kimapenzi unahusiana na jinsi wapenzi ama wanandoa wanavyowasiliana wakiwa pamoja.

Inategemea na yale wanayosema, jinsi wanavyosema na muhimu zaidi yale tunayotenda na malengo ya kutenda hayo tunayotenda. Haya huwa yanachangia kwa kiwango kikubwa mawasiliano yetu na kudumisha ama kuzorotesha uhusiano.

Wakati wanandoa wanaoshirikishwa pamoja sababu ya upendo, heshima na haja ya kupatiana faraja, mara nyingi mawasiliano huwa ni ya moja kwa moja na kuelezea hisia za mume, mke ama wapenzi.

Mwanamume anapomuoa mwanamke, mara nyingi huwa ni kwa sababu amevutiwa naye, labda akaona uwezekano wa yeye kuwa mama wa watoto wake.

Wanawake ni walezi kwa asili, ‘waumbaji’ wa vitu, wasimamizi wazuri na wabunifu wa mambo mengi katika familia.

Wanaweza kwa urahisi sana kuelezea kitu kilichopo kwenye akili likija suala la biashara kama kununua au kuuza. Hivyo unapomuona mwanamke ambaye tayari anao mtandao wa marafiki, ni muhimu kuwekana sawa tangu mwanzoni, kile ambacho kinakubalika na kile ambacho hakiwezi kukubalika. Kuwa kwenye ndoa hakukuzuii mke kuwa na marafiki. Kwani pia mara nyingi wanandoa huunganisha vikundi vya marafiki na ndoa zao na kushirikiana katika mambo ya kujenga ndoa na uhusiano. Lakini hata uwe karibu sana na wanandoa wengine, kuna uwezekano wa kuwa na marafiki ambao hawajaolewa na ambao wanaendelea kuishi maisha ya useja.

Katika mchanganyiko kama huu inawezekana kuleta tofauti kati ya wanandoa. Kwani mara nyingi, mtizamo, mipango na vipaumbele vya mwanamke ama hata mwanamume ambaye hayuko kwenye ndoa ni tofauti na yule ambaye yuko katika ndoa.

Pamoja na maisha ya ndoa, ni vyema pia kuwa na uhusiano na watu wengine, marafiki ambao mnaweza kushirikiana kimawazo katika kujenga yaliyo bora na sio vinginevyo.

Hata hivyo uhusiano huu na kutumia muda nje ya marafiki ni vyema ukubalike na wanandoa wote wawili. Kwani iwapo unatumia muda mwingi zaidi ukiwa na marafiki badala ya kuwa na mumeo ama familia yako, hapo kunaweza kuwa na dosari.

Unaweza kuwa unatoka mara kwa mara na marafiki zako kwenda katika starehe ama burudani na mwenzako ashindwe kukuelewa ama iwe ni chanzo cha mvutano, hapo kuna umuhimu wa kutathmini hatua zako. Panga ipasavyo na weka kando muda wako muhimu kwa mtu unayempenda, badala ya marafiki wako. Watu unaotumia wakati mwingi kuwa nao ndio wenye ushawishi mkubwa.

Ingawa pia kuwa na marafiki ni muhimu kwa maendeleo ya kibinafsi na ukuaji, inaweza kutoa sauti na maoni tofauti.

Kwa upande mwingine marafiki wengi na sauti nyingi zinaweza kuwa hatari kwa ndoa yako. Jifunze kwa busara na hekima kujua nini kinaendelea katika maisha ya mume wako na pia onyesha kwamba unamjali sana na kwa njia hiyo naye atakupenda zaidi na ndoa yenu itakuwa imara zadi.

[email protected]

JUKUMU moja kuu la mume kwa mkewe ni kumhakikishia ulinzi na usalama wake. Jukumu jingine muhimu la mwanamume ni kuhakikisha mkewe ana furaha ili aweze kuchangia katika ufanisi wa ndoa na familia.

Hakuna sheria inayoweka mipaka ya jinsi mume anafaa kuhakikisha mkewe ana furaha. Katika kuhakikisha mke ana raha, wanaume huwa wanatumia mbinu tofauti ikiwa ni pamoja na kuwapa wake zao muda wa kustarehe na marafiki zao.

Starehe hizi zinaweza kuwa katika maeneo tofauti ikiwemo ni kwenye vilabu ambako wengi wanasema ni hatari mume kuruhusu mke kwenda kivyake.

Ni kweli vilabuni huwa kuna mambo mengi hasa ikiwa umeoa au kuolewa. Kuna vituko vya kila aina na watu wakilewa huwa wanaweka uungwana kando na kuvaa uhayawani ambao hakuna mwanamume angetaka mkewe ajihusishe nao. Hii inaamanisha kuwa ili mtu kuruhusu mkewe kwenda kujivinjari na marafiki vilabuni lazima afahamu hatari na madhara yake.

Kama nilivyotangulia kusema, ni jukumu la mume kuhakikishia mkewe usalama wake.

Hivyo basi, kwa mume kuruhusu mke kuandamana na marafiki vilabuni bila kuhakikisha yuko salama ni kutelekeza jukumu hili muhimu.

Ikiwa mwanamke ameolewa na anafahamu kwamba ni jukumu la mumewe kumlinda na anamtambua kama mlinzi wake nambari moja, anafaa kuhakikisha kwamba anajua anakokutana na marafiki wake kila wakati.

Ikiwa ni katika vilabu ambako watu wakilewa huwa wanavua utu na kujivika ufisi, basi mke anapaswa kuhakikisha mumewe yuko karibu.

Kwa mke kusisitizia mumewe kwamba anahitaji uhuru wa kujivinjari na mashogake ni ishara kuna mambo anayoficha. Mambo ya siri daima huwa ni tishio na sumu kwa ndoa.

Kila mwanamume anajua mkewe anachopenda. Ikiwa mtu anajua mkewe anapenda kucheza densi vilabuni na kuteremsha chupa kadhaa za pombe, sidhani itakuwa haki kumnyima ruhusa ya kufanya hivyo wakioana mradi tu ajue marafiki anaondamana nao na wanakoenda kujivinjari.

Hata hivyo, nasisitiza kuwa uhuru huo unafaa kuwa na mipaka. Makosa wanayofanya wanawake wengi ni kutoa vitisho kuwashinikiza waume zao wawape ruhusa ya kwenda kujumuika na marafiki vilabuni.

Baadhi huwa wanajikumbusha waliyokuwa wakifanya kabla ya kuolewa ikiwa ni pamoja na kushiriki ufuska. Hii ndiyo inayofanya wanaume wengi kuchelea au kuwakazia wake zao raha na starehe vilabuni na marafiki wao.

Inasemwa sio rahisi kufuta mazoea ya mtu mzima na ikiwa ulioa mtu mliyekutana vilabuni, itabidi uvumilie hulka zake huku ukibeba mzigo zaidi wa kumhakikishia usalama wake kwa sababu hilo ni jukumu usiloweza kuepuka kama mume.

Hii inahitaji mwanamume mwenye moyo wa chuma anayeweza kuachwa nyumbani mkewe akiponda raha na na kisha kumfungulia mlango akirudi usiku wa manane au kwenda kumchukua akiwa chopi bila kujali wanayosema watu.

Ni vyema kuambiana ukweli kwa kuwa hulka hii inaongezeka siku hizi na jinsi kizazi cha sasa kinavyochukulia taasisi ya ndoa kwa mzaha, sioni ikiyeyuka.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Madai ya ‘mradi wa Joho’ yamtia doa...

HUKU USWAHILINI: Si ajabu mwanamume kutoroka kwake, kisa...

T L