• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 11:53 AM
HUKU USWAHILINI: Si ajabu mwanamume kutoroka kwake, kisa vituko vya mamkwe

HUKU USWAHILINI: Si ajabu mwanamume kutoroka kwake, kisa vituko vya mamkwe

NA SIZARINA HAMISI

KAMA ilivyo kwa wenzetu huko Uzunguni, huku kwetu Uswahilini pia tunakutana na changamoto za ndugu kutaka kujazana nyumbani bila utaratibu, wakati mwingine akiwemo mama mkwe.

Tena hawa akina mama mkwe wa huku wengi ni wa upande wa mwanamke. Kwamba mama mkwe anahamia kwa msichana wake akidai anahitaji matibabu ama anahitaji kupumzika. Hatajali kwamba binti yake anaishi chumba kimoja na maisha yake ni ya kuunga unga.

Shughuli inakuwa kwa mwanamume aliyeoa binti huku kwetu. Kwani kama ana kipato kiasi, anaweza kugeuzwa kuwa mradi wa kupata mahitaji na hata pesa kwa huyo mkwewe. Akiwa na bahati mbaya zaidi, hutafutiwa jinsi ya kudhibitiwa ikiwemo kuendewa kwa mganga ili asifurukute na atoe kila anachoombwa bila maswali wala ubishi.

Tumeona mwanamume akikosa amani na wakati mwingine kuikimbia nyumba yake sababu ya visa na vituko vya mama mkwe wake. Mmojawapo akiwemo barobaro mmoja ambaye tunasikia amehamia mtaa wa pili baada ya vibweka kuzidi nyumbani kwake.

Mama mkwe alijaribu njia za kienyeji kumdhibiti huyu mume wa binti yake na ziliposhindikana akahamia kwenye mbinu za kivita. Ikawa kila mwanamume akirudi kutoka kazini analakiwa na maswali chungu nzima zikiwemo lawama za jinsi binti yake alivyosinyaa na kukosa raha sababu anashindwa kumtunza vizuri.

Hilo halikumuudhi zaidi ya ile tabia ya mkwewe kuwagongea mlango usiku wa manane wakiwa katikati ya shughuli akidai anataka dawa kichwa kinamuuma.

Juhudi za mwanamume kuzungumza na mkewe kuhusu tabia na mwenendo wa mama yake hazikuzaa matunda kwani mkewe kasisitiza kwamba yule ni mama yake na hawezi kumfukuza ama kumuambia aondoke.

Alipoona hali imekuwa tete zaidi nyumbani kwake, yule kaka akaondoka bila kuaga. Siku alipoenda kazini hakurudi tena.

Sisi hapa mtaani tunayo habari kwamba kahamia mtaa wa jirani, kapanga chumba chake kingine na ameanza maisha yake peke yake.

Hivi sasa tunamuona binti alivyokosa raha na jinsi anavyohangaika kukidhi mahitaji, kwani hana kipato cha maana, shughuli zake ni kupika na kuuza vitumbua ambavyo havikidhi mahitaji yake na mama yake.

Mashambenga wa mtaa wakamfuata yule binti na kumshauri amuondoe mama yake pale nyumbani na amuombe radhi mumewe kabla hajarukiwa na wajanja wa mjini. Tunasubiri tuone matokeo, kwani bado mama mkwe anajivinjari kwa binti yake. Hatujui hadi lini.

[email protected]

You can share this post!

BAHARI YA MAPENZI: Ni sawa mkeo kustarehe na marafiki?

IEBC: Kilio cha Raila kinampa Ruto maksi

T L