• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
KIGODA CHA PWANI: Madai ya ‘mradi wa Joho’ yamtia doa Abdulswamad

KIGODA CHA PWANI: Madai ya ‘mradi wa Joho’ yamtia doa Abdulswamad

NA PHILIP MUYANGA

JE uhusiano wa karibu wa kisiasa ambao mbuge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir anao na Gavana Ali Hassan Joho utaathiri azma yake ya kutwaa kiti cha ugavana wa Mombasa wakati wa uchaguzi wa Agosti 9?

Swali hili linaulizwa na watu wengi kwa kuwa baadhi ya wapinzani wa Bw Nassir wanalitumia kisiasa na kudai kuwa yeye ni mradi wa Bw Joho.

Wapinzani hao wanadai kuwa Bw Nassir ataendeleza uongozi wa Kaunti ya Mombasa jinsi ulivyo sasa iwapo atatwaa mamlaka na kuwa gavana.

Katika mojawapo ya mikutano ya kisiasa ya wananchama wa muungano wa Kenya Kwanza (KKA) eneo la Likoni, mgombea wa ugavana katika tikiti ya United Democratic Alliance (UDA), Bw Hassan Omar alisema kuwa Bw Joho anataka kuwawekea wakazi wa Mombasa mtu atakayeendeleza mambo yake.

Azimio la Umoja

“Watu wa Likoni wakatae, sisi hatuchaguliwi viongozi, (rais) Uhuru na Raila (Odinga aliye kinara wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya) walikaa chini na kumchagua Abdulswamad,” alisema Bw Omar.

Hata hivyo, katika mojawapo ya mahojiano na kituo kimoja cha televisheni hivi majuzi, Bw Nassir alipuuzilia mbali dhana ya kuwa yeye ni mradi wa Bw Joho.

Bw Nassir akijitetea, alisema kuwa wapinzani wake walijaribu kuzua dhana hiyo kwa wananchi kuanzia kitambo, ila akasema yeye ni mradi wa watu wa Mombasa.

“Mimi ni mradi wa watu, haikuanza jana au juzi, walijaribu kuitia lugha hiyo na sumu hiyo kitambo, watu wenyewe wakasema huu ni mradi wetu, mimi ni Abdulswamad Shariff Nassir, mtoto wa Mombasa, mradi wa watu wa Mombasa,” akasema Bw Nassir.

Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa, azma ya mbuge huyo wa Mvita kutwaa kiti cha ugavana Mombasa inaweza kuathiriwa na uhusiano wake na Bw Joho au pia kumjenga kisiasa kwani sio watu wote ambao hawapendi uongozi wa sasa wa kaunti hiyo.

Mombasa

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa pia wanadai kuwa iwapo Bw Nassir atachukua uongozi, basi ataendeleza sera za uongozi uliopo, suala ambalo baadhi ya wananchi hawatafurahia.

Prof Hassan Mwakimako ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Pwani, bewa la Kilifi, suala la Bw Nassir kudhaniwa kuwa mradi wa Bw Joho litamuathri kisiasa kwa njia moja ua nyingine.

“Bw Nassir amekuwa mtu wa karibu wa Bw Joho na kulikuwa na watu ambao walikuwa wamechoshwa na uongozi wa Bw Joho ambao utasababisha baadhi yao kuukikimbia,” asema Prof Mwakimako.

Hata hivyo, Prof Mwakimako anaongeza kuwa Gavana Joho pia anao wafuasi wengi ambao wanaweza kumpigia kura Bw Nassir na kupiga jeki azma yake ya kuwa gavana wa Kaunti ya Mombasa.

Kulingana na Prof Mwakimako, hata wabunge wa Mombasa ambao walikuwa wanamuunga mkono Bw Nassir, ni kwa kuwa walikuwa wanahusishwa na Bw Joho.

Mchanganuzi mwingine wa masuala ya siasa nchni, Bi Maimuna Mwidani anasema kuwa Bw Nassir kutajwa kama mradi wa Bw Joho kutamuathiri kisiasa.

Bw Mwidani anasema kuwa sababu moja ya Bw Nassir kuonekana kuwa mradi wa Bw Joho ni kwa kuwa kulikuwa na juhudi kubwa kuhakikisha kuwa yeye ndiye anayepeperusha bendera ya chama cha ODM katika uwaniaji wa kiti hicho.

“Iwapo kungekuwa na kura ya mchunjo ya chama cha ODM na Bw Nassir ashinde,basi ingekuwa vigumu sana kumwita au kusema kuwa yeye ni mradi wa mtu fulani kwa kuwa angekuwa amewashinda wapinzani wake,” akasema Bi Mwidau.

Bi Mwidau anasema kuwa dhana ya kuwa Bw Nassir ni mradi itamuathiri na inafaa afanye bidii sana kuhakikisha anajiondoa katika dhana hiyo na kujiweka huru na kwamba hategemei kiongozi yeyote kisiasa.

Kwa upande wake, mchanganuzi wa siasa za Mombasa, Bw Mndwamrombo Mwakera anasema kuwa kuhusishwa kwa Bw Nassir na Gavana Joho kutamwathiri kisiasa kwani tayari wapinzani wake wanamuona kama mradi wa gavana huyo.

Mgombea mwenza

“Pia uchaguzi wa mgombea mwenza unatilia mkazo sana dhana hiyo kwa sabababu mgombea huyo (Bw Francis Thoya) ashawahi kufanya kazi katika serikali ya Bw Joho kama katibu wa kaunti,” anasema Bw Mwakera.

Bw Mwakera anaongeza kuwa ingawa tangu kuanza kwa kampeni rasmi bado mbuge huyo wa Mvita hajaonekana na Gavana Joho katika shughuli zake za kampeni za kusaka kura, suala hilo halijatoa dhana ya kuwa Bw Nassir ni mradi katika uchaguzi ujao.

Kwa sasa inasubiriwa kuonekana iwapo dhana ya Bw Nassir kuwa mradi wa uongozi wa sasa wa Kaunti ya Mombasa, inayoendelezwa na baadhi ya wapinzani wake na wafuasi wao, itamwathiri katika azma yake ya kuwa gavana wa pili wa kaunti hiyo.

Baadhi ya wawaniaji wa ugavana wa Mombasa ni pamoja na Bw Omar, Daniel Kitsao (mgombea huru), naibu gavana wa Mombasa Dkt William Kingi (PAA), Hezron Awiti (Vibrant Democratic Party), Said Abdalla (Usawa Kwa Wote) na Shafi Makazi (United Party of Independent Alliance).

  • Tags

You can share this post!

WALIOBOBEA: Mudavadi ‘alilelewa’ na Moi...

BAHARI YA MAPENZI: Ni sawa mkeo kustarehe na marafiki?

T L