• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 11:13 AM
JUNGU KUU: Ruto atarajie presha kali kutoka kwa Raila

JUNGU KUU: Ruto atarajie presha kali kutoka kwa Raila

NA WANDERI KAMAU

UREJEO wa kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, nchini unatarajiwa kuongeza shinikizo kwa Rais William Ruto kutekeleza ahadi alizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni yake ya urais mwaka 2022.

Mara tu baada ya kurejea nchini kutoka ziara ya wiki moja katika Milki ya Kiarabu (UAE) Ijumaa, Bw Odinga alifululiza hadi katika ngome yake ya Kibra, Nairobi, ambapo alitangaza kurejea kwa maandamano dhidi ya serikali kuanzia Jumanne.

Bw Odinga aliilaumu serikali kwa kukosa kutekeleza na kuzingatia masuala yaliyoibuliwa na mrengo huo kama kupunguza gharama ya juu ya maisha kwa Wakenya, kuwarejesha ofisini waliokuwa makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) maarufu kama “Cherera 4”, kuboresha usalama katika sehemu tofauti nchini kati ya mengine.

Mwelekeo wa Bw Odinga pia unafuatia kuvurugika kwa mazungumzo yaliyokuwa yamepangwa kuanza baina ya mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja, kujadiliana na kusuluhisha masuala tata.

Kenya Kwanza inasisitiza mazungumzo hayo kuendeshwa katika Bunge la Kitaifa, huku Azimio ikishikikia kuwa lazima yaendeshwe nje ya Bunge.
Suala jingine tata ni kujumuishwa kwa baadhi ya wabunge katika majopo hayo.

Azimio inapinga kujumuishwa kwa mbunge Adan Keynan (Eldas) katika jopo litakaloiwakilisha Kenya Kwanza, huku Kenya Kwanza nayo ikipinga kujumuishwa kwa mbunge David Pkosing (Pokot Kusini).

Ni hali inayotishia kuvuruga kabisa mazungumzo hayo, ikizingatiwa yalionekana na wengi kama hatua ya mwanzo katika kusuluhisha mvutano huo.

Kulingana na wadadisi wa siasa, urejeo wa Bw Odinga na uamuzi wake wa kurejesha maandamano utaishinikiza serikali kuanza kutekeleza ahadi ambazo imekuwa ikitoa—kwa mfano kupunguza bei ya unga.

Wiki mbili zilizopita, Rais Ruto aliwaahidi Wakenya kuwa bei ya unga ingepungua hadi Sh150 baada ya siku chache, lakini hilo bado halijaonekana kutimia kwani raia wengi bado wanalalamika kuwa bei hiyo haijashuka.

“Urejeo wa Bw Odinga bila shaka utaipa shinikizo serikali kutimiza ahadi zake kama vile kupunguza bei ya unga na umeme. Kwa muda ambao amekuwa nje ya nchi, serikali ya Rais Ruto imeonekana kulegea kuhusu utekelezaji wa masuala ambayo tayari yameibuliwa na Upinzani,” asema mdadisi wa siasa Wyclife Muga.

Rais Ruto amekuwa akilaumiwa na baadhi ya Wakenya kwa kutotimiza baadhi ya ahadi alizotoa kwao, kwani wengi wanaendelea kuhangaika kutokana na gharama ya juu ya maisha.

Rais pia amejipata lawamani kutokana na Serikali ya Kitaifa kuchelewa kutuma fedha kwa serikali za kaunti, hali ambayo imewalazimu baadhi ya magavana kutishia kusimamisha shughuli zote katika kaunti zao kwa siku 14 kutokana na ukosefu wa fedha.

Kadhalika, Rais Ruto anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kutokana na serikali kuchelewa kulipa mishahara ya watumishi wa umma—hilo likitajwa kutoshuhudiwa hata kidogo katika serikali za marais waliomtangulia kama Mzee Jomo Kenyatta, Daniel Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta.

Vile vile, pendekezo la Rais kuwatoza watumishi wa umma asilimia tatu ya mishahara yao kama ada maalum ya ujenzi pia limekosolewa vikali.

  • Tags

You can share this post!

BAHARI YA MAPENZI: Uvumilivu ni mzuri ila nao una mipaka

Uhuru alivyozamisha merikebu ya Jubilee

T L