• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Justina Syokau afunga mwaka na drama zake

Justina Syokau afunga mwaka na drama zake

NA WANDERI KAMAU

MWANAMUZIKI Justina Syokau almaarufu kama ‘Madam 2020’ anamaliza mwaka 2023 kwa drama zake za kawaida.

Ingawa yeye ni mwanamuziki anayeimba nyimbo za Injili, Bi Syokau amekuwa akigonga vichwa vya habari kwa vitendo ambavyo wakati mwingine vimekuwa vikizua utata na midahalo isiyoisha miongoni mwa mashabiki wake.

Mwaka 2023, kama ilivyo kawaida yake kila mwisho wa mwaka, ashatoa wimbo ‘2024’ kuukaribisha Mwaka Mpya.

Bi Syokau amekuwa akitoa wimbo kuukaribisha na kutoa ‘tabiri’ kuhusu kila mwaka, tangu 2020.

Kufikia sasa, ametoa nyimbo kuhusu miaka ya 2021, 2022, na 2023.

Ikizingatiwa kuwa lazima aonyeshe mbwembwe fulani anapojitayarisha kutoa kila wimbo, hali haikuwa tofauti mwaka 2023.

Wiki iliyopita, Bi Syokau alidai kuwa ana mimba.

Kwenye mahojiano na wanahabari, Bi Syokau hata alionyesha dalili za mwanamke mwenye ujauzito.

“Hebu nitulie kidogo kutokana na hali yangu ya ujauzito,” akawaeleza wanahabari, ambao walilazimika kukatiza mahojiano yake kwa dakika chache.

Kama hilo halikutosha, Bi Syokau mnamo Jumatano alisema anataka kuolewa na mwanamuziki wa nyimbo za injili Alex Apoko almaarufu kama ‘Ringtone’.

Bi Syokau alizua vurugu katika makazi ya mwanamuziki huyo katika mtaa wa kifahari wa Runda jijini Nairobi, aliposisitiza kuwa lazima amwone kwa nguvu.

“Nimekuwa nikimtaka Ringtone. Mbona ananikataza kuingia kwake? Nimekuwa nikitamani anioe. Niko tayari kuolewa naye,” akasema Bi Syokau, huku akiingia kwa nguvu kwenye makazi ya mwanamuziki huyo.

Mwanamuziki Ringtone alikuwa amewaalika wanamuziki wenzake kusherehekea Sikukuu ya Krisimasi.

Baada ya sakata hiyo, Bi Syokau aliiambia Taifa Leo mnamo Alhamisi kwamba huwa vitendo vyake si mzaha, bali humaanisha anachosema.

“Kusema kweli, nina mimba na nimekuwa nikimtamani mwanamuziki Ringtone kwa muda mrefu. Hii si kiki. Si mzaha ninaowafanyia mashabiki wangu,” akasema Bi Syokau.

Hata hivyo, mwanamuziki mmoja ambaye ni mshirika wake wa karibu alisema kuwa vitendo tata vya Bi Syokau ni njia ya kuzipa umaarufu nyimbo zake. Kwenye mahojiano na Taifa Leo, mwanamuziki huyo alifichua kwamba vitendo hivyo vyote vilikuwa mbinu za kuupa umaarufu wimbo wake ‘2024’.

“Bi Syokau ni mwanamuziki anayefahamu kuwa nyimbo zake zitapata umaarufu ikiwa atazua utata fulani. Hiyo ni njia tu ya kujipa umaarufu, ambayo inakubalika katika burudani,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Kuzubaa kwa sababu ya mihadarati kunasababisha ajali

Kandanda: Gundi ya mshikamano, silaha dhidi ya mihadarati

T L