• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Posti za ‘kichokozi’ kwa Christina Shusho

Posti za ‘kichokozi’ kwa Christina Shusho

NA LABAAN SHABAAN

WANAUME wenye mazoea ya kumezea mate kila mwanadada mrembo, wamejitoma mitandaoni kuelezea namna wanavyomsubiria mwanamuziki wa nyimbo za injili kutoka nchini Tanzania, Christina Shusho.

Ni bayana kuwa wamemzimikia kichizi Shusho mwenye sauti ya ninga.

Haya yanadhihirika tukifuatilia jumbe zilizoelekezwa kwake katika mitandao ya kijamii.

“Kweli nawe unahitaji make-up kweli?  Wewe ukijipaka mafuta ya kupikia bado utapendeza,” aliandika Dionis Germain akijibu posti ya Shusho aliyopachika katika akaunti ya mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) mnamo Jumapili, Desemba 24, 2023.

Mtumiaji mwingine wa X, Stalon Memer aliweka posti ya kichokozi, kudhihirisha ni kwa jinsi gani anavyokoshwa na mwimbaji huyo.

Naye Zee la Mshale akasema kwamba anampenda Shusho kinoma.

“Wewe mama nakupenda hatari,” aliandika Zee la Mshale.

Wengi wa mashabiki wanaosema na Christina Shusho mitandaoni wanarejelea kibao chake kinachotamba kwa jina ‘Shusha Nyavu’.

Ni wimbo wa kumtumainia Mungu kuwa ukiamini Neno lake na kufanya kazi, utafaulu.

Fidelis Lavu na Kelvin Aluku wamestaajabia urembo wa Shusho wenye ulimbo wa kumnata mwanamume yeyote na wakamuita malkia wa Afrika mwenye urembo kupindukia.

Haya yanajiri siku chache kabla ya kuandaliwa kwa shoo ya Shusho Live Concert ya kuruka mwaka Desemba 31, 2023, jijini Nairobi.

Unatarajiwa kuwa usiku wa kucheza na kuabudu ambapo wasanii mbalimbali watatumbuiza.

Wasanii hao ni pamoja na mchekeshaji Daniel Ndambuki almaarufu ‘Churchill’, na waimbaji wa nyimbo za injili Mercy Masika na Solomon Mkubwa.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Shusho kutumbuiza mkesha wa kuukaribisha mwaka mpya.

Mnamo Desemba 31, 2016, Shusho alipanda jukwaani katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta (KICC) ambapo aliwatumbuiza mashabiki waliokuwa wakikesha kukaribisha mwaka 2017.

  • Tags

You can share this post!

Mwanajeshi, mpenziwe ndani kwa wizi wa bastola

Krismasi: Mfugaji ateremsha bei majirani wale samaki

T L