• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Wito serikali, mashirika yamnyanyue mwanahabari Kimani Mbugua

Wito serikali, mashirika yamnyanyue mwanahabari Kimani Mbugua

NA WANDERI KAMAU

MNAMO Oktoba 2023, mamia ya Wakenya waliungana pamoja kumsaidia mwanahabari Kimani Mbugua, baada ya kukumbwa na msururu wa masaibu, yakiwemo matatizo ya kiakili.

Mwanahabari huyo mchanga kitaaluma lakini mwenye uzoefu, alikuwa amekaa karibu miaka miwili katika Hospitali ya Watu Wenye Matatizo ya Kiakili ya Mathari, jijini Nairobi.

Baada ya kuruhusiwa kuondoka hospitalini, Bw Kimani alikiri kwamba hakuwa na lolote wala chochote, hivyo alihitaji msaada wa Wakenya.

“Nimefanikiwa kutoka hospitalini, ila sina chochote kwa sasa. Sina hata mahali pa kulala. Marafiki wangu kadhaa niliokuwa nikikaa kwao wameniambia nitafute mahali pangu binafsi,” akasema Bw Kimani.

Ikizingatiwa alikuwa amejijengea ufuasi mkubwa alipohudumu katika vituo vya televisheni vya NTV na Citizen, mashabiki wake hawakumuacha jangwani.

Akihudumu katika vituo hivyo vya televisheni, aliwachangamsha wengi kwa kusimulia masuala ya burudani kwa njia ya kipekee kwa hadhira yake.

Pia, wale waliokuwa wakimtazama nyakati za asubuhi katika runinga ya Citizen, walifuatilia kwa umakini habari kuhusu misongamano ya magari barabarani, hivyo kuwasaidia sana kujipanga walipokuwa wakielekea kazini au kwa shughuli zao za kawaida.

Mashabiki wake waliungana kupitia mitandao tofauti ya kijamii kama vile Facebook, Instagram, na Tiktok kuchanga fedha za kumsaidia.

Kwenye mtandao wa Tiktok, harakati za kumchangia fedha ziliongozwa na mwanamitandao Nyako, anayeishi nchini Ujerumani.

“Nawarai Wakenya wenzangu kuungana tumsaidie mmoja wetu,” alisema mwanamitandao huyo.

Kutokana na juhudi hizo, Wakenya walifanikiwa kuchanga zaidi ya Sh400,000.

Bw Kimani aliwashukuru Wakenya na mashabiki wake kwa ujumla, akisema kuwa mapenzi yao yatamruhusu kujisimamia tena kama mwanahabari huru.

“Sasa nimeanza safari ya kurejea tena kwenye ulingo wa uanahabari bila kikwazo wala kisingizio chochote,” alisema mwanahabari huyo.

Licha ya ‘kufufuka’ tena kutoka kwa uraibu wa mihadarati na matatizo ya kiakili, vumi zimeibuka kuwa kuna uwezekano mwanahabari huyo asharejea kwenye njia isiyo.

Mnamo Alhamisi, Bw Kimani alifanya video moja ndefu kupitia mtandao wa Tiktok akiwa ndani ya matatu moja akielekea jijini Nairobi, ambapo alisikika akitoa sauti na kauli zilizotia wengi hofu.

Kwenye video hiyo, ambayo ilidumu kwa zaidi ya saa mbili na kutazamwa na karibu watu 3,000 mwanahabari huyo alisema mengi huku akipuuzilia mbali msaada wa kifedha aliopewa na Wakenya kama vile haukuwa na maana yoyote.

“Hamkunisaidia hata kidogo!” akafoka.

Hata hivyo, mwanahabari huyo alisema mnamo Ijumaa kwamba alikuwa amepoteza fahamu, hivyo Wakenya hawafai kumlaumu.

Hayo yakiendelea, maswali yameibuka kuhusu kimya cha taasisi muhimu kama mashirika ya kuwasaidia watu wanaokumbwa na matatizo ya kiakili, huku mwanahabari huyo mahiri akiendelea kuzama.

“Ni wakati taasisi hizo zijitokeze ili kumsaidia mwanahabari huyu stadi kutorejea tena kwenye uraibu wa mihadarati,” akasema Bi Triza Rehema.

  • Tags

You can share this post!

‘Mgeni njoo wachuuzi Pirates Beach tuvune’

Siasa za atakayemrithi Ruto Bonde la Ufa zashika kasi    

T L