• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
BBI YAINGIA ICU

BBI YAINGIA ICU

NA MWANGI MUIRURI

MCHAKATO wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga kubadilisha Katiba kupitia BBI umo kwenye hatari ya kufeli. Hii ni kutokana na mivutano ya kisiasa baina ya wawili hao, pamoja kukosa kuchangamkiwa na wananchi na vizingiti vya kisheria.

Iwapo itafeli, BBI itakuwa imeletea Kenya hasara ya zaidi ya Sh20 bilioni ambazo zimetumika hadi sasa katika kampeni, wakati mamilioni ya Wakenya wanaposhindwa kupata chakula na matibabu, gharama ya maisha kupanda kutokana na ushuru wa juu kupindukia pamoja na madeni ya kigeni, biashara kuporomoka na wengi kukosa ajira.

Pesa hizi ni pamoja na Sh200 Milioni ambazo zilitumika katika awamu ya kwanza ya kuandaa ripoti ya BBI, ikarejeshwa tena kwa jopo hilo kuandaa ripoti ya pili iliyogharimu Sh55 milioni.

Mamilioni mengine yametumiwa katika kampeni za rais, Bw Odinga na washirika wao za kupigia ripoti hiyo debe.Pia kuna Sh4.5 bilioni za kuwapa madiwani marupurupu ya magari waliyopewa na Rais Kenyatta ili kuwashawishi waunge mkono BBI.

“Tunakadiria kuwa Sh20 bilioni zimetumika kufikia sasa katika BBI. Hii ni pamoja na uchapishaji na usambazaji wa nakala, matangazo kwa vyombo vya habari, kampeni za viongozi wakuu, pesa ambazo zimekuwa zikipewa viongozi na wananchi mashinani, magari ya madiwani miongoni mwa matumizi mengine,” asema Bw Wanjumbi Mwangi, ambaye ni mwenyekiti wa taasisi ya ushauri wa masuala ya kifedha ya NewTime.

Duru za kijasusi nazo zilieleza Taifa Leo kuwa kufeli kwa BBI pia kunatishia kuzua msukosuko wa kisiasa nchini, kutokana na taswira kuwa Rais Kenyatta alikubali BBI na handisheki kwa nia ya kumtuliza Bw Odinga baada ya uchaguzi wa 2017, mbali sio kuunganisha nchi.

Wandani wa Bw Odinga wakiwemo Seneta wa Siaya, James Orengo na Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohammed, wanasema kuna juhudi za kumhujumu Bw Odinga kisiasa licha yake kuwa mwaminifu kwa Rais Kenyatta tangu 2018.

Jana Bw Odinga alisema kuna njama ya kujaribu kupitisha BBI kupitia kwa wabunge, akisisitiza kuwa lazima iende kwa kwa wananchi kupigiwa kura.

BBI pia inakabiliwa na changamoto za kisheria baada ya Mahakama Kuu kuagiza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) isipange referenda ya BBI hadi kesi zinazoipinga zisikizwe na kuamuliwa.Bungeni nako kumezuka pingamizi tele kuhusu mchakato huo huku Naibu Mwenyekiti wa ODM, Wycliffe Oparanya akisema kuwa referenda kwa sasa sio wazo la busara.

“Sasa ni wakati wa kushughulikia masuala nyeti kama Covid-19 na madeni ambayo yanazidi kupanda. Referenda inaweza ikangoja,” akasema Bw Oparanya.

Kauli hii ya ODM ni kinyume na msimamo wake wa awali ambapo Bw Odinga alisisitiza kuwa referenda lazima ifanyike mwaka huu.Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki, Jeremiah Kioni anasema kuwa mchakato wa BBI sasa umekosa mwelekeo baada ya kuingizwa siasa.

Pia kamati kuu ya kushirikisha BBI inayoongozwa na mbunge wa zamani wa Dagoretti Dennis Waweru na Bw Junet imeripotiwa kusambaratika.

Masuala ambayo yanatishia kuvuruga BBI bungeni ni kuhusu kubuniwa kwa maeneo bunge mapya, ambapo 70 yamependekezwa, suala ambalo limepingwa na wabunge kutoka maeneo ambayo hayapati maeneo mapya.Pia kuna mvutano kuhusu iwapo ripoti ya BBI iliyo bungeni ifanyiwe marekebisho.

Duru za kambi ya Bw Odinga zimeeleza Taifa Leo kuwa kuna manung’uniko makubwa miongoni mwa wafuasi wake, na wanamikakati wake wanapanga kuhakikisha kuwa utengano baina yake na Rais Kenyatta utakuwa na dhoruba kali.

“Njama katika mrengo wa Bw Odinga ni kumsukumia Rais Kenyatta kashfa kuwa aliidhinisha mabilioni ya pesa za umma zitumike kufadhili BBI wakati nchi inapokabiliwa na changamoto tele za Covid-19, umaskini na madeni ya kiholela,” akadokeza afisa mmoja wa ODM.

Kinara wa Narc Kenya, Martha Karua anahoji kuwa mawimbi yanayotisha kuzamisha BBI yameibuka baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuzinduka kuwa jaribio lao la kubadilisha Katiba halina mwelekeo wa kisheria wala uungwaji mkono wa wananchi wengi.

You can share this post!

‘Sauti ya Mnyonge’ anayeendeleza ndoto ya kutetea...

Daraja la Liwatoni lazidisha hatari ya kuenea kwa corona