• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
KILIMO NA MAZAO: Pato la nduma kwake si kubwa lakini analiongeza kwa kuwekeza vikundini

KILIMO NA MAZAO: Pato la nduma kwake si kubwa lakini analiongeza kwa kuwekeza vikundini

Na JOHN NJOROGE

BAADA ya kutolewa kwenye makao yake yaliyokuwa sehemu za Olpusimoru katika mpaka wa Kaunti za Nakuru na Narok kufuatia vita vya kikabila zaidi ya miaka 20 iliyopita, Hannah Nyambura, 60, alihamia katika kijiji cha Kasarani mjini Elburgon ambapo alikodisha nyumba na kuanza kutafuta kazi ya vibarua ili aweze kulea watoto wake waliomtegemea.

Baada ya miaka kadha ya kuhangaika huku akitafuta kazi ili apate riziki ya kila siku, Nyambura alipata sehemu ndogo ya shamba lililoko karibu na chemichemi ya maji ambapo alikodisha kutoka kwa shirika la reli kwa Sh2,000 ambapo alilipa na kuanza matayarisho ya upanzi wa nduma alizozinunua kutoka kwa ofisi za kilimo mjini Molo.

“Baada ya kununua mizizi/ miche ya nduma iliyoidhinishwa, nilichimba mashimo na kuyatenganisha kwa mita moja ili kuzipa nafasi nzuri ya kukua. Kwa kuwa fedha nilizipata kwa shida, nilitafuta mbolea ya wanyama,” akasema Nyambura na kuongeza kuwa alitumia Sh3,000 kununua miche 200 mmoja akinunua kwa Sh15.

Mkulima huyu ambaye amekuwa kwa ukulima huu kwa zaidi ya miaka kumi, alisema kuwa kutoka kwa robo hiyo ya shamba, hawezi kuwa na majuto kwa sababu amewasomesha watoto wake ambapo mmoja wa wanawe alihitimu mwaka uliopita.

Baada ya miezi sita, Nyambura alianza kuvuna mazao yake na kuwauzia majirani huku akitafuta soko. Kwa siku nzuri, aliweza kupata zaidi ya Sh1,000 huku wanabiashara wa hoteli wakimtembelea shambani mwake na kununua bidhaa zake.

Kwa wakati huo, rafiki yake alimtembelea na kumwomba ajiunge na kikundi ili awe anawekeza fedha kidogo kutoka kwa mauzo yake ya siku akisema baada ya majuma kadha, atapata fedha nzuri kwa pamoja na aweze kujimudu kimaisha.

“Niliona ikiwa vigumu kwangu kujiunga na kikundi hicho kwa sababu baadhi ya siku ambapo nilipata Sh200 pekee na hazingetosha matumizi yangu nyumbani na kuwekeza kwenye kikundi. Baada ya kuwaza na kuwazua, nilijawa na imani na kujiunga na kikundi hicho cha akina mama wasiopungua 20 ambapo nilianza kuwekeza Sh200 kila siku,” akasema Nyambura na kuongeza kuwa, kwa siku ambazo mauzo yalikuwa mazuri, aliwekeza hadi Sh500 alipogundua kuwa ni njia moja ya kuweka na kuongeza mapato.

Kufuatia ukosefu wa ajira na kupigwa marufuku kwa ukataji miti nchini, Nyambura alisema kuwa licha ya sehemu hii ya shamba kuwa ndogo imemfaidi pakubwa. Amekuwa akipata mauzo haba na kuwekeza kidogo ambacho kimemsaidia sana kutekeleza wajibu wa kuwasomesha watoto wake akijivunia kuwa hawajawahi kutumwa nyumbani kwa ukosefu wa karo.

Akiongea na Akilimali hivi majuzi, Nyambura anakumbuka siku moja ambapo alipata mauzo ya Sh5,000 kwa siku moja ambapo fedha hizo zilimwezesha kuwekeza Sh2,500 akizingatia kuna siku zingine ambapo mauzo huwa chini sana. Fedha zingine alizitumia kwa matumizi ya nyumbani.

Alisema ukulima huu hauna hasara akieleza kuwa hakuna wadudu wanauvamia. Tangu alipoanza kulima nduma, alisema hajawai kuona wadudu wakivamia zao lake.

“Nduma huhitaji maji mengi ndio ziweze kunawiri vizuri. Kwa bahati nzuri, mmea huu hunawiri hata wakati wa kiangazi, matawi yake hayakauki,” akasema na kuongeza kuwa ana mpango wa kuongeza sehemu hiyo hadi ekari moja ili apata mauzo tele na fedha zaidi za kuwekeza.

Nyambura alisema kuwa ukulima wa vyakula vya miezi michache huwa na faida ikilinganishwa na ile ya miezi mingi kama vile mahindi ambapo mkulima huvuna baada ya mwaka mmoja huku akitumia gharama nyingi na bei kuwa ya chini mno.

Kwa wakati huu, mkulima huyu ana zaidi ya miche 6,000 ambapo matarajio yake ni 10,000 ifikapo mwezi wa Aprili wakati kuna mvua nyingi. Kulingana na mkulima huyu, nduma hazina hasara, wakulima wanapovuna huwa wanakata sehemu za shina na kupanda tena ambapo huchukua pia miezi sita kukua na kukomaa.

Nyambura alikiri kuwa hajawai tembea katika maonyesho ya kilimo kupata ujuzi na maarifa zaidi ya ukulima huu. Alisema kuwa yeye hufuatilia maelezo ya ukulima kwa kupitia redio na televisheni ambapo ameelemishwa zaidi. Kwa mkulima anayepanga kupanda nduma kwa mara ya kwanza, Nyambura alisema kuwa cha muhimu ni kutambua sehemu ambayo ina maji mengi, udongo wenye rutuba na mbolea ili mazao yake yanawiri ipasavyo.

Alfrend Waithaka, afisa wa kilimo katika kaunti ndogo ya Molo amewahimiza wakulima kujaribu kupanda vyakula tofauti tofauti akisema sehemu hii ina rutuba ya kutosha.

You can share this post!

KILIMO NA MAZAO: Sumu kwenye nafaka, mbegu bandia zimeumiza...

BIASHARA MASHINANI: Ubunifu wa upanzi wa maua umemzolea sifa