• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 5:30 PM
Biashara ya siagi yafaidi walemavu

Biashara ya siagi yafaidi walemavu

NA BRIAN OCHARO

WAKATI kundi la wanawake wanaoishi na ulemavu katika eneo la VoK, Kaunti ya Mombasa lilipokusanyika ili kusaidiana kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayowakabili, hawakujua kwamba umoja wao ungezaa mradi ambao umewapa sababu za kutabasamu.

Mradi wa kutengeneza siagi ndio umekuwa kitega uchumi kwa zaidi ya wanawake 15 ambao wako katika kundi hilo linalojiita Tunaweza PWD.

Wanawake hao wamekodisha nyumba katika eneo la VOK wanakofanyia mradi huo.

Kundi hilo pia linawasaidia wazazi wa watoto wanaoishi na ulemavu kupitia mradi huo wa kutengeza siagi.

Siku ya kawaida, mkurugenzi wa mradi huo Charity Chahasi husimamia shughuli za kutengeneza siagi.

Mwandishi huyu alipotembelea mradi huo wiki iliyopita, Bi Chahasi na wafanyakazi wengine walieleza utaratibu wao wa kuongeza thamani na maana ya mradi huu kwa kikundi chao na wanajamii walio katika mazingira magumu katika eneo hilo.

“Tulianzisha kiwanda hiki cha jamii cha siagi kama njia ya kuhakikisha kuwa wanawake na watoto wanaoishi na ulemavu wanapata msaada wa kiuchumi na hawaathiriwi na hali zao za kimaumbile,” alisema Chahasi.

Mradi huo ulianza mwaka wa 2016 kwa kuuza siagi iliyochakatwa hapa nchini na kuwalipa wanachama waliofanya mauzo asilimia ya faida.

Walianza na mashine yao ya kwanza iliyokuwa na uwezo wa kusindika kilo mbili kabla ya kununua mpya ambayo inaweza kusindika hadi kilo hamsini kwa siku.

Mchakato wa kutengeneza siagi katika kiwanda kidogo cha kuongeza thamani kama hii ya Tunaweza CBO ni cha makini na cha kushangaza kwani unaanza kutoka shambani.

Njugu huvunwa vizuri wakati udongo umekauka vya kutosha hivyo hautashikamana na mashina na maganda.

Kisha hatua ya pili ni kuwa, zinaondolewa kwenye magamba na wachumaji na kusafirishwa kwa ajili ya kukaushwa.

Mimea hiyo hupelekwa kwenye vyumba vya kuhifadhia kwa ajili ya kusafish – wa. Shirika hilo hupata njugu zao kutoka kwa wakulima wakubwa katika Kaunti ya Busia.

Katika kiwanda hicho kidogo, kikundi hicho huchoma na kupoeza njugu hizo.

“Baada ya kuzichoma na kupozwa, njugu hizo huondolewa ngozi kwa kutiwa joto au maji,” alifafanua Bi Chahasi.

Kulingana naye, njia ya joto ina faida ya kuondoa sehemu kali ya njugu. Anasema wao pia huongeza chumvi katika hatua hii ili kuboresha ulaini na ladha.

Mwaka wa 2018 ulikuwa wa mafanikio kwa biashara yao kwani mahitaji yaliongezeka baada ya kupata kandarasi kadhaa ya usambazaji kwa maduka makubwa ya ndani ambayo yaliidhinisha siagi kwenye rafu zao.

“Hii ilitupa fursa ya kutengeneza bidhaa zaidi ili kuboresha mapato yetu. Tuliongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji yetu,” alieleza.

Huku baadhi yao wakibakia kwenye eno hilo kushugulikia mambo mengine, wengine wao huondoka kuenda kufanya mauzo sehemu mbali mbali wa mji wa Mombasa.

“Lazima tuwatafute wateja ambao wanahitaji bidhaa hizi. Mara nyingi lazima tuwatafute wateja kwani wengine wanaweza kuwa na uvivu wa kufika hapa kwetu kununua,” alisema.

Hata hivyo, kama biashara nyingine yoyote, chama hicho kimekumbwa na changamoto mbalimbali.

Mojawapo ya changamoto hizo ni baadhi ya maduka makubwa kushindwa kulipa licha ya kupewa bidhaa.

Alieleza kuwa duka kubwa ambalo chama hicho kiliuzia bidhaa hizo lilizama na deni ya zaidi ya Sh50,000 baada ya kushindwa kulipia bidhaa.

Bi Chahasi anasema licha ya mafanikio waliyoyapata katika mradi huo, wanahitaji mashine nzuri na yenye ufanisi ili kuimarisha uzalishaji.

Anasema kuwa mashine waliyonayo kwa sasa ni ndogo hivyo huwa vigumu kuongeza uzalishaji.

  • Tags

You can share this post!

Nina tajriba ya kufufua uchumi, Wanjigi asema

Timu ya Zetech Rugby yaonyesha ubingwa wake

T L