• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
Binti ajitunza kwa kuosha magari na pikipiki mjini, Nairobi

Binti ajitunza kwa kuosha magari na pikipiki mjini, Nairobi

Na WINNIE ONYANDO

AKIWA amevalia nguo nyeupe ya kuyazuia maji yasimmwagikie mwilini, Nancy Wanjiku almaarufu Shiko, 30, anaonekana akiosha gari nyeupe aina ya Toyota katika karakana yake mtaa wa Mlango Kubwa,  Nairobi.

Alipotembelewa na Akili Mali, Wanjiku alisema alichoshwa na harakati za mara kwa mara za kutafuta ajira bila mafanikio.

“Japo nimesoma, nilichoshwa na kazi ya kutafuta ajira mjini. Nina watoto wawili wanaonitegemea hivyo nikaamua kuanzisha biashara ya kuosha magari,” akaeleza Wanjiku.

Tangu aanzishe biashara yake, mrembo huyo hajawahi kujuta. Analipa kodi ya nyumba, kuwalipia watoto karo na kuwakimu.

“Kupitia biashara hii, nimetimiza baadhi ya malengo yangu maishani. Kila mara nikiwaona wateja wakija ili niwahudumie, huwa najawa na furaha,” akaeleza Wanjiku.

Kwa siku, Wanjiku anaweza kuyaosha magari zaidi ya 10 huku idadi ya pikipiki kuzidi 20.

Ili kupata huduma ya kuoshewa gari, Wanjiku hutoza kati ya Sh250 na Sh500 kutegemea ukubwa wa gari lenyewe. Kwa upande mwingine, kuosha pikipiki hugharimu Sh50.

Kwa siku, Wanjiku hupata faida zaidi ya Sh5000. Anaeleza yeye huwekeza idadi fulani ya pesa kwa matumizi ya baadaye na kwa nia ya kujiendeleza kimasomo.

Katika biashara hiyo, Wanjiku amewaajiri vijana watatu kutoka katika mtaa wa Madhare ambao humsaidia katika kuwatolea wateja huduma.

Utaratibu wa kuliosha gari

Ili kuosha gari, Wanjiku huhitaji maji, mashine ya kuosha na kumimina maji, sabuni, brashi ngumu ya kusugulia magari, besheni au ndoo na sponji.

Kwanza kabisa, gari au pikipiki humwagiliwa maji safi kabla ya kuanza kusuguliwa.

Gari au pikipiki hunyunyiziwa maji yaliyo na sabuni na kusuguliwa na sponji na kisha baadaye kusuguliwa na brashi. Mwishowe, maji safi hutumika ili kulisuuza gari.

Ili kulifanya lingare zaidi, taulo nyeupe iliyotiliwa marashi hutumika kupangusia maji yaliyobaki baada ya kuoshwa.

Changamoto

Wanjiku alivyoianzisha biashara yake miaka miwili iliyopita, aliugua kwa muda wa wiki moja baada ya kupatikana na nimonia kwa sababu ya kutumia maji kila mara.

“Kwa kuwa mwili haukuwa umeyazoea maji wa mara kwa mara, nilipatikana na nimonia na kukaa nyumbani kwa muda wa wiki mbili kabla ya kurejea kazini,” Wanjiku aliambia Akili Mali.

Kadhalika, kazi yake humlazimu kushika maji kila mara, jambo analoeleza humdhuru hasa wakati wa baridi.

Hata hivyo, anasema anaienzi biashara yake kutokana na faida chemchem anazozizoa kutokana na bidii yake.

Anawahimiza vijana wasikae tu na kutegemea serikali bali wajitume ili kuboresha maisha yao.

You can share this post!

Kuongeza bei ya mafuta kunaongezea umaskini Kenya –...

Kijana aunda Sh150,000 kutokana na magurudumu