• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Kijana aunda Sh150,000 kutokana na magurudumu

Kijana aunda Sh150,000 kutokana na magurudumu

Na WINNIE ONYANDO

BAADHI ya watu huyatupa magurudumu baada ya matumizi ya muda ila kwake Joseph Mwaniki, 33, gurudumu zee ni manufaa kwake.

Kazi ya kuchakata magurudumu alianza mwaka wa 2012 na imemkimu pamoja na familia yake.

Alipotembelewa na Akili Mali katika karakana yake iliyoko Sokoni Kariokor, mjini Nairobi, Mwaniki alisema baada ya kuacha kazi kama agenti wa kampuni ya kutoa huduma za bima, alizamia bishara ya kuunda bidhaa mbalimbali kwa kutumia magurudumu.

“Mimi huyasanya magurudumu nzee, kuyaosha na kutengeza bidhaa tofauti tofauti. Pesa ninazopata kutoka kwayo haziaminiki,” akasema Mwaniki.

Kutoka kwa magurudumu, yeye hutengeza viatu, ukanda, kamba za kufungua mizigo na viti.

Kando na magurudumu, Mwaniki hutumia ngozi ya ng’ombe au ngamia, kitambaa, gundi aina ya Crowmax, Quickboard ama Tuffstick, mashine spesheli aina ya gunder, mashine ya kushona na ya kurembesha, kisu spesheli ya kukata kiatu na makasi.

Namna ya uundaji (Viatu)

Baada ya kuoshwa, gurudumu hukatwa katika umbo mbalimbali ili kutengeza kiatu.

Ngozi ya ngamia pia hukatwa katika umbo tofauti tofauti. Baada ya hapo, ngozi ya ngamia huunganishwa na gundi aina ya Crowmix.

Ngozi hiyo hushikanishwa na rexin kutumia gundi aina ya tuffstick ili kuepuka kutokana. Baada ya hapo, ngozi pamoja na rexin zilizounganishwa huwekwa katika mashine ya kushona ili ziunganishwe kabisa.

Baada ya kushonwa, huunganishwa na gurudumu lililokatwa tayari ili kutengeza kiatu kitakachodumu kwa muda mrefu.

Mwishowe kabisa, viatu kilichotengezwa huwekwa katika mashine ya kutia madoido ili kumvutia mteja zaidi. Kwa siku, Mwaniki anawezaviunda viatu zaidi ya 50.

Bw Mwaniki akiwa katika karakana yake, Kariokor, Nairobi. Picha/Winnie Onyando

“Mara nyingi mimi huviuza viatu kwa jumla hasa kwa Wamaasai ambao huvinunua viatu vingi. Hata hivyo nawauzia wateja rejareja ambao hutembelea karakana yangu,” Mwaniki akaambia Akili Mali.

Kwa siku, mwanabiashara huyo mashuhuri hupata faida zaidi ya Sh5000 kutoka kwa biashara yake.

Kila kiatu yeye hukiuza kati ya Sh200 na Sh400 kutegemea ubora na mfuko wa mteja mwenye.

“Ikiwa mteja anaonekena ana pesa, mimi nitamwambia bei ya juu. Ikiwa amevaa hivi hivi, nitampunguzia bei,” akasema Mwaniki.

Kati ya viatu zaidi ya 50 anavyoviunda kila siku, Mwaniki anawezaviuza karibu viatu vyote.

Kando na viatu, Mwaniki huyatumia gurudumu kutengeza viti vya kiasili vinavyoashiriana na mila na desturi za jamii mbalimbali nchini.

Mara nyingi yeye huviuza viti hivyo katika masoko ya vijijini kwa kuwa amewaajiri wafanyikazi aliowafunza kuviunda.

Kwa upande mwingine, anatekengeza kamba zinazotumika mara nyingi na waendeshaji pikipiki kufungia mizigo.

Biashara yake imemwezesha kujenga nyumba ya kifahari mashambani na kuwasomeshea wana wake wawili. Changamoto zinazomkumba sana katika baishara yake ni kiwango cha juu cha ushindani.

Hata hivyo, anajitahidi kila mara kuwa tofauti na washindani wake kwa kuunda bidhaa za kipekee. Anawashauri vijana kuwa wabunifu katika kila jambo wanalolitenda ili kuongeza mapato yao.

“Ubunifu ndio uti wa mgongo katika biashara yoyote. Hii itakuwezesha kuwashinda washindani wako,” akashauri Mwaniki.

You can share this post!

Binti ajitunza kwa kuosha magari na pikipiki mjini, Nairobi

Kocha wa Ingwe atarajiwa kuwasili Ijumaa