• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Buda Murang’a alivyosherehekea Krismasi kwa bajeti ya Sh100  

Buda Murang’a alivyosherehekea Krismasi kwa bajeti ya Sh100  

NA MWANGI MUIRURI 

KRISMASI, ni sherehe inayofanyika kila mwaka kote duniani kuadhimisha siku maalum ya kuzaliwa kwa Yesu Kristu na ambayo wengi huihusisha na ulaji na unywaji hasa vileo.

Kwa Wakristu, wapo wanaokongamana makanisani kwa minajili ya ukumbusho wa Yesu.

Nchini Kenya, idadi kubwa ya wakazi wa maeneo ya mijini Desemba 25 huwapata wakiwa mashambani.

Sijui wewe uliiadhimisha vipi?

Kwa John Mburu, mkazi wa Murang’a aliisherehekea kwa njia ya kipekee, bajeti aliyoitengea ikivutia zaidi.

Bw Mburu anaamini Sikukuu ya Krismasi huandaliwa nyumbani ila si kwenye baa kinyume na mtazamo wa wengi.

Mzee huyu anaanza kwa kufichua kiwango cha pesa alichotumia kusherehekea Krismasi 2023.

“Bajeti yangu mtaani ilikuwa Sh100 na sikutatizika kamwe kujihesabu na wengine waliosherehekea kivyao.

John Mburu akisherehekea Krismasi 2023 kwenye bucha. Alitumia bajeti ya Sh100 pekee kununua nyama, supu, nyama na glasi ya mvinyo. PICHA|MWANGI MUIRURI

Nilifululiza hadi mkahawa uitwao Green Park, Murang’a unaosifika kwa upishi wa supu na nyama ya kichwa, ngozi, miguu na matumbo ya ng’ombe.

Wengi watatilia shaka jinsi Sh100 zilinitosha kusherehekea, ila huu ndio ukweli wa mambo; Niliagiza supu ya Sh20 na nyama ya kichwa ya Sh30.

Mapeni yaliyosalia, niligonga glasi moja ya mvinyo na kamwe silalamiki kwamba sikukuu ilinipita.

Baadaye, jua lilipotua (jioni) nilirejea kwangu nikasherehekea kile ambacho familia yangu ilikuwa imeandandaa.”

Hiyo ndiyo ilikuwa taswira ya jinsi Mzee Mburu aliadhimisha Krismasi 2023.

Mwaka Mpya 2024, mwenyeji huyu wa Murang’a anasema bajeti ya kuulaki haitakuwa tofauti na ya Krismasi iliyokamilika.

“Nitatekeleza bajeti nyingine ya Sh100 kuukaribisha,” Mburu anasisitiza.

Anadokeza kwamba nyumbani kwake kulikuwa na bajeti ya Sh5, 000, japo ilidhibitiwa na wengine.

“Na sio eti pesa hizo zina upungufu eti ningepata Sh200 au hata Sh1, 000 ningetumia vinginevyo. Hiyo ndiyo ilikuwa bajeti yangu na uraibu wangu ni huo, kwa kuwa sio eti nilikuwa naingia kwa supu na nyama nile nishibe bali ni kwa raha tu zangu,” anasema.

Anaongeza: “Kwa ulevi, hata uniume kitovu changu, siwezi kamwe nikazidisha glasi moja kwa kuwa silewi ili niwe hoi, bali ni kuchangamsha akili tu.”

Na kwa wenye mazoea ya kuponda raha msimu wa Krismasi na kusahau kesho yaja, anawashauri: “Kifupi, ninakusihi uwe na adabu za matumizi mtaani hasa katika safu ya raha. Sikukuu huandaliwa nyumbani wala sio kwenye baa”.

 

  • Tags

You can share this post!

Ninaenda ‘break’ mashabiki mnisubiri – Akothee

Wanandoa wanaojitafutia riziki kwa kuchimba vyoo, makaburi

T L