• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Chuo chachunguza ‘wadudu’ wawe mlo

Chuo chachunguza ‘wadudu’ wawe mlo

Na MAUREEN ONGALA

UTAFITI umeanzishwa kuchunguza ikiwa aina ya lishe ya samaki inaweza kutumiwa kama chakula cha binadamu katika Kaunti ya Kilifi.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Egerton wameungana na wenzao kutoka Chuo Kikuu cha Maseno na Taasisi ya Utafiti wa Baharini (Kemfri), kwa utafiti huo.

Wanalenga kubainisha kama ‘wadudu’ wa baharini wanaofahamika kama Artemia ambao huliwa na samaki, wanaweza kuwa na virutubisho vinavyofaa binadamu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Egerton, Dkt Maureen Cheserek, alisema viumbe hivyo vidogo vya baharini huwa havijatiliwa maanani humu nchini ikilinganishwa na baadhi ya mataifa ya nje.

“Artemia hawatumiwi ipasavyo katika nchi yetu kuhusu hitaji ya kuongeza virutubisho, lakini tunaposoma vitabu, tunapata kuwa hutumiwa kama chakula cha binadamu katika mataifa ya Asia,” akasema, akiwa Kilifi, Jumatano.

Kulingana na Dkt Cheserek, utafiti utalenga kutafuta mbinu zinazoweza kutumiwa ili viumbe hao wasaidie kupunguza ukosefu wa virutubisho kwa watoto na wanawake katika jamii kitaifa.

Alikuwa akizungumza katika eneo la Kadzuhoni, Kaunti ya Kilifi wakati wa hafla ya kuhamasisha wenyeji kuhusu manufaa ya kufuga Artemia.

Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa Kadzuhoni, Bw John Sulubu, alisema walianza kufuga viumbe hao wa baharini katika mwaka wa 2011 kwa lengo la kuuzia viwanda vya kutengeneza lishe ya samaki wanaofugwa.

“Wakulima walifunzwa wakahamasishwa na tukapokea vyema mradi huu. Sasa tumeanza kufaidika kifedha na mambo yakiendelea hivi tutafanikiwa kuondoa umasikini katika eneo letu,” akasema.

Mpango huo ulifadhiliwa na Western Indian Ocean Marine Science Association (WIOMSA).

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Maseno, Dkt Erick Ogello, alisema ingawa baadhi ya wakazi wamekuwa wakijihusisha na ufugaji wa Artemia, mapato yao hayajakuwa ya juu jinsi inavyostahili kwa sababu wanatumia mbinu zilizopitwa na wakati katika shughuli zao.

Wafugaji hao sasa wamefunzwa kuhusu mbinu mpya ya ufugaji inayofahamika kama Bionfloc ambayo inatarajiwa kuwaongeza mapato.

“Wenyeji walikuwa wanafuga Artemia, ndio, lakini walikuwa wakifa kwa kukosa kulishwa. Teknolojia hii mpya itasaidia kuongeza bakteria katika vidimbwi vya ufugaji, ambazo viumbe hao watakula,” akaeleza.

Dkt Ogello alisema wafugaji wa samaki nchini kwa sasa wanakumbwa na uhaba wa lishe ya samaki wao na hivyo kuhatarisha uzalishaji nchini.

“Katika soko la kimataifa, kilo moja ya Artemia huuzwa kwa Dola 70 (takriban Sh7,000). Kuna nafasi kubadilisha hali mbaya ya uchumi inayoshuhudiwa katika eneo hili ambapo wakazi huwa hawategemei kilimo bali hujitafutia riziki katika uchimbaji madini ya kutengeneza chumvi,” akasema.

Mtafiti kutoka Kemfri, Bi Maureen Mukami alisema wenyeji walianza kushirikishwa katika ufugaji wa Artemia katika mwaka wa 2010 kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa viumbe hao wa baharini.

Kemfri hununua kilo moja ya Artemia kwa Sh800, na kuzitumia kutengeneza lishe ya samaki ambayo huuzwa kwa wafugaji wa samaki katika maeneo mbalimbali nchini.

You can share this post!

Jamii ya Sengwer yalia viongozi kusahau eneo lao kimaendeleo

Hatima ya uchaguzi mdogo kujulikana leo