• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Hatima ya uchaguzi mdogo kujulikana leo

Hatima ya uchaguzi mdogo kujulikana leo

Na MWANDISHI WETU

MAHAKAMA Kuu ya Meru leo Alhamisi inatarajiwa kuamua hatima ya uchaguzi mdogo wa Wadi ya Kiagu, Kaunti ya Meru katika kesi iliyowasilishwa na Chama cha Kazi (CCK).

Chama hicho kinachohusishwa na mbunge wa Gatundu Moses Kuria, kilikimbilia mahakamani baada ya mwaniaji wake, Milton Mwenda, kuondolewa kwenye kinyang’anyiro na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

IEBC ilitupilia mbali jina la Bw Mwenda kutokana na kigezo kwamba alichelewa kujiuzulu kutoka kwenye utumishi wa umma.

Bw Nathan Gitonga wa chama cha National Ordinary Peoples Empowerment Union (Nopeu), pia alizuiwa kuwania kiti hicho.

Wawili hao walikuwa wafanyakazi katika Bunge la Kaunti ya Meru kwenye afisi ya diwani aliyefariki, Eunice Karegi.

Jaji Anthony Mrima aliagiza kusimamishwa kwa uchaguzi huo uliofaa kufanyika Oktoba 14, 2021.

Aliagiza pande zote kufika kortini leo.Bw Mwenda aliondolewa kwenye orodha ya wawaniaji baada afisa wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), Imenti Kusini, Salesio Thuranira, kuwasilisha malalamishi kwa IEBC.

Baada ya kuondoa jina la Bw Mwenda, IEBC iliagiza chama cha CCK kuwasilisha jina la mwaniaji mwingine kwa afisa wa IEBC, Imenti ya Kati. Lakini chama cha CCK kilipeleka jina la Jacob Mugambi Muriithi kwa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati jijini Nairobi.

“Mlikosa kuwasilisha jina la mwaniaji mbadala kwa afisa wa IEBC Imenti ya Kati kufikia Septemba 27, hivyo tunachukulia kuwa CCK haina mwaniaji,” ikasema barua ya IEBC kwa chama hicho cha Bw Kuria.

Mahakama inatarajiwa kuamua ikiwa uchaguzi huo mdogo utafanyika bila mwaniaji wa CCK kushiriki au Bw Muriithi ataruhusiwa kushiriki.

You can share this post!

Chuo chachunguza ‘wadudu’ wawe mlo

Kenya kuadhimisha Siku ya Utamaduni