• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 3:16 PM
DINI: Tusemezane kwani hakuna yasiyotatulika

DINI: Tusemezane kwani hakuna yasiyotatulika

NA PADRE FAUSTINE KAMUGISHA

LISEME, usikae nalo. Hakuna yasiyotatulika. Hakuna yasiyo na suluhisho. Elewa upande wa mwingine.

Kusemezana ni kufikiria pamoja, kusemezana ni kujadiliana, kusemezana ni kusikilizana. Ni kusikiliza na kusikilizwa. Kusemezana ni kuzungumza. Kusemezana ni kuvunja ukimya.

Wito wa kusemezana ni wito wa kiBiblia, “Njoo tusemezane” (Isaya 1:18). Kusemezana ni kuwasiliana.

“Mawasiliano katika mahusiano ni kama oksijeni ilivyo kwa uhai. Bila mawasiliano mahusiano yanakufa,” alisema Tony A. askins Jr.

Bila kusemazana kuna kuumizana. Mawasiliano ni lugha ya amani. Mawasiliano ni lugha ya uongozi.

“Ufundi wa kuwasiliana ni lugha ya uongozi,” alisema James Humes.

Kusemezana ni niseme nawe useme. Ni kuzungumza.

Kuna wanandoa wawili ambao kwa muda wa miezi miwili walikuwa hawaongei. Siku moja mwanaume aliamua kuvunja ukimya. Alivuruga vitu kwenye nyumba. Aliweka mashuka na blanketi sebuleni. Alitoa vyombo kwenye kabati na kuweka sebuleni. Alitoa nguo masandukuni na kuweka sebuleni kana kwamba anatafuta kitu. Alifanya shughuli hiyo kwa muda wa saa mbili.

Mke wake alimuuliza, “Unatafuta nini muda wote huu?”

Alijibu, “Natafuta sauti yako.”

Kusemezana ni kuitafuta sauti ya mwenzako. Ni kupata maoni yake. Kusemezana ni kusikilizana. Nisikilize, nikusikilize. Nikusikilize, unisikilize.

“Kujibu kabla ya kusikiliza ni upumbavu na jambo la aibu” (Mithali 18: 13).

Sikiliza hadithi yake. Sikiliza hadithi yake yote.

Kuna baba mmoja aitwaye Musa aliyekuwa na mtoto wake ambaye alihitajika kufanyiwa operesheni. Siku ya operesheni daktari John alichelewa.

Baba huyo alilalamika sana. Daktari alikuja akikimbia.

Mzee Musa alianza kulalamika akisema, “Ulikuwa wapi? Unapata mshahara bila kuufanyia kazi. Unasepa tu toka kazini. Mtoto akikumbwa na jambo baya ni mimi na wewe.”

Daktari John aliingia chumba cha operesheni na kufanya kazi nzuri. Baada ya hapo alitoka nje. Alimwambia mzee Musa, “Mtoto wako anaendelea vizuri. Kila kitu atakueleza nesi.”

Daktari John aliondoka.

Mzee Musa alisema, “Unaondoka tena kwenda kwenye shughuli zako.”

Baadaye mzee Musa alimuuliza nesi, “Mbona dakatari huyu yuko hivi leo.”

Nesi alimwelezea kuwa amefiwa na mtoto wake. Alikuwa kwenye mazishi. Aliacha wanaendelea na mazishi na kuja hospitalini kumfanyia mtoto wako operesheni.

Mzee Musa alijihisi vibaya. Shida ni kutosikiliza hadithi ya mwingine.

Kuna methali ya Wahaya isemayo, “Tiwakuramura kwa nyakaisiki, otakauririze kwa nyakojo” (Huwezi kuamua kesi ya msichana, bila kusikiliza upande wa mvulana). Sikiliza upande wake pia.

Kuna aliyesema, “Tatizo kubwa sana katika mawasiliano ni kuwa hatusikilizi kuelewa bali tunasikiliza ili tupate kujibu.”

Sikiliza ukiwa na nia ya kumwelewa mwenzako. Sikiliza mwili wa mwenzako. Sikiliza na lile ambalo halikusemwa au liko katikati ya mistari.

Kusemeza ni kufikiria pamoja kimantiki.

Biblia inasema mume anapaswa kumfikiria mke wake na kumuelewa.

“Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili” (1 Petro 3:7).

Bila kufikiria pamoja ni kushindwa kukaa pamoja kwa akili. Sikiliza hoja zake. Sikiliza sababu zake. Sikiliza upande wake.

Kusemezana ni muhimu katika kuleta maridhiano, amani, maelewano na utulivu. Kusemezana ni muhimu katika familia, katika taasisi, katika nyanja za kisiasa na kidini.

Kusemezana ni tiba.

“Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza lakini si mwepesi wa kusema wala mwepesi wa kukasirika” (Yakobo 1:19). Yatafakari kabla ya kusema au kujibu.

Wahaya wana methali isemayo, “Nkagamba akira nkesiza” (Nilisema anamzidi nilinyamaza). Sema naye usinyamaze. Ongea usinyamaze. Sikiliza, usifumbe masikio.

You can share this post!

Aliyedaiwa kukuza bangi nyumbani ajisalimisha

Kampuni yaanza kukarabati vifaa katika kiwanda

T L