• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
DOUGLAS MUTUA: Nenda salama Magufuli

DOUGLAS MUTUA: Nenda salama Magufuli

Na DOUGLAS MUTUA

NAKUMBUKA mwanzoni mwa janga la corona, yapata mwaka mmoja uliopita, nikipiga gumzo na jamaa na marafiki walionitembelea nyumbani.

Tulielezana hofu kwamba ugonjwa huo usipodhibitiwa kwa wakati, huenda ungewatwaa watu mashuhuri kwa jinsi ambayo haikuwahi kushuhudiwa duniani.

Nina masikitiko nikiandika haya kwa kuwa mmoja wa marais wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) – Dkt John Joseph Pombe Magufuli wa Tanzania – hayuko nasi duniani.

Naungana na Watanzania, Jumuiya ya EAC na bara la Afrika kwa jumla kumuaga kiongozi ambaye, japo alikuwa na mapungufu tele tu ya kibinadamu, aliipenda nchi yake.

Ijapokuwa si rasmi kuwa Dkt Magufuli alifariki kutokana na corona, duru za kuaminika zinasema alipata matatizo ya kupumua, yaliyoungana na ya moyo na kuleta matokeo chanya – kifo.

Dkt Magufuli ni kiongozi wa pili wa taifa la Afrika Mashariki kufariki katika hali ya kutatanisha katika muda wa mwaka mmoja uliopita.

Pierre Nkurunziza wa Burundi alituaga mwaka jana mwishoni mwa urais wake kwa kile kilichosemekana rasmi kuwa matatizo ya moyo, lakini dalili zilikuwa zilezile za corona – kushindwa kupumua.

Iwe marais wawili hao walifariki kwa corona au la, tunapaswa kuchukulia misiba hiyo kama tahadhari kwetu sisi binafsi na kwa watunga sera kote duniani kwamba mapuuza si tiba.

Dkt Magufuli na Bw Nkurunziza walikana uwepo wa corona nchini kwao, wakawahimiza watu watumie mitishamba kujikinga nao badala ya kutafuta suluhu za kisayansi.

Wote wawili waliwahadaa waumini wa dini zote – Waislamu, Wakristo, Wahindi na Dini za Kiasili za Afrika – kwamba maombi yangewakinga na janga hilo lakini wapi!

Wasichoelewa ni kwamba hata utaalamu wa sayansi ni uwezo tuliopewa na Mungu, hivyo anayeupinga kwa misingi ya ukinzani na imani yake anatangaza hadharani amepungukiwa na uwezo wa kutumia akili!

Biblia takatifu yenyewe inamnukuu Mungu akisema ‘watu wangu huangamia kwa kukosa hekima’, hivyo kukataa msaada wa wataalamu na kuishia kufa alivyokufa Magufuli ni ushahidi wa kukosa hekima.

Ikiwa kwa hakika Magufuli alifariki kutokana na korona, kifo chake ni ithibati kwamba kiongozi anayefanya mambo bila kutafakari matokeo anaweza kujinasa kwa mtego wake mwenyewe.

Naamini Magufuli angetangaza wazi kwamba anaumwa ama angesafirishwa ng’ambo kutibiwa hospitalini bora zaidi duniani au matabibu bora duniani washuke Tanzania kwa fujo kumganga!

Huu haupaswi tu kuwa wakati wa maombolezi bali pia fursa ya watawala wapya wa Tanzania kutafakari na kujichungua vilivyo ili waamue wanataka kuipeleka nchi wapi.

Rais Samia Suluhu Hassan anapaswa kuzitupilia mbali sera za Magufuli za kukana corona, aalike jamii ya kimataifa kuikwamua Tanzania ilikokwamishwa na janga hili.

Hatua ya kwanza ni kuwaamuru Watanzania watumie barakoa na njia nyingine za kujikinga, kisha aagize chanjo kwa mamilioni ili awasaidie kusalia hai.

Rais Hassan anapaswa kuiponya nchi kwa kurejesha undugu na kushusha joto la kisiasa, awasihi Watanzania waliokimbilia uhamishoni wakimwogopa marehemu warejee.

Buriani Magufuli, nenda salama.

[email protected]

You can share this post!

FRANCIS MUTEGI: Suluhu awe mwanga mpya Tanzania...

Kizaazaa Jaji kulalama faili ya kesi ya Bobi Wine imetoweka