• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Fahamu jinsi unavyoweza kuhifadhi mazingira kwa kutumia jiko linalotegemea nishati ya miale ya jua

Fahamu jinsi unavyoweza kuhifadhi mazingira kwa kutumia jiko linalotegemea nishati ya miale ya jua

NA MAGDALENE WANJA

UTOTONI, Justine Abuga alitaka kuwa daktari kwani alipenda sana masomo ya sayansi na alitaka kusaidia jamii zinazoishi katika kaunti ya Nyamira alikozaliwa.

Alihisi kwamba jamii katika eneo hilo zilikuwa zimetengwa katika shughuli za maendeleo na aliona angeweza kusaidia katika kuinua hali zao za kiafya.

“Katika mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne, nilikosa nafasi ya kujiunga na masomo ya udaktari kwa kukosa alama moja tu. Niliamua kufanya kozi ya Microbiology katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, ili kusaidia katika utafiti na kurahisisha kazi ya madaktari,” akasema Bw Abuga.

Alipokuwa katika mwaka wa pili katika msomo, alijiunga na marafiki ambao pamoja walianzisha shirika la kutoa hisani (foundation)

Kazi yao kuu ilikuwa ni kuwasaidia wasiojiweza haswa katika mitaa duni.

Siku moja walipokuwa wakitembelea makao ya watoto ya Watu Wa Maana Children’s Home, watoto walitumwa kutafuta kuni za kupika. Ulikuwa msimu wa mvua na watoto hao walinyeshewa.

“Hii ilinikumbusha changamoto kama hizi ambazo nilipitia utotoni mwangu, na nilianza kuwaza jinsi ninavyoweza kubadilisha hali hii,” akasema Abuga.

Tuliporudi chuoni, nilianza kufanya utafiti wa jinsi ambavyo ningeweza kutafuta njia mbadala ya kupata nishati ya kupikia,” anasema.

Mnamo mwaka 2016, walishirikiana na marafiki zake na kuanzisha kampuni ya Ecobora ambapo ilianza kutengeneza makaa aina ya bryquettes.

“Tulianza kwa kusambaza makaa hayo kwenye makao ya watoto jijini Nairobi, na baadaye kwenye sehemu za vijijini,” anasema Abuga.

Justine Abuga (wa pili kulia) ambaye alifanya utafiti na wenzake hadi wakatengeneza jiko la kipekee ambalo hutumia nishati itokanayo na miale ya jua. Limerahisisha shughuli ya upishi na lina manufaa mengi kama vile kuokoa muda na kuhifadhi MAZINGIRA kwani halina moshi. PICHA | MAGDALENE WANJA

Baada ya muda, aligundua kwamba, japokuwa wanafunzi nyumbani hawakutumwa kutafuta kuni, shuleni walihitajika kubeba vipande vya kuni kila siku.

Mnamo mwaka 2018, serikali ilipiga marufuku ukataji wa miti, bila kutoa mwelekezo wa nishati mbadala ambayo ingetumika shuleni.

Justine Abuga (kulia) ambaye alifanya utafiti na wenzake hadi wakatengeneza jiko la kipekee ambalo hutumia nishati itokanayo na miale ya jua. Limerahisisha shughuli ya upishi na lina manufaa mengi kama vile kuokoa muda na kuhifadhi MAZINGIRA kwani halina moshi. PICHA | MAGDALENE WANJA

Baada ya kushauriana, walifanikiwa kuunda aina ya jiko ambalo linatumia nishati ya jua.

“Jiko hili la kipekee hutumia nishati itokanayo na miale ya jua na limerahisisha shughuli ya upishi na lina manufaa mengi kama vile kuokoa muda na hewa safi kwani halina moshi,” akasema Bw Abuga.

Kwa idadi ya wanafunzi kati ya 400 na 1000 ambao hutumia tani 96 za kuni kwa mwaka, jiko hili la nishati ya jua limesaidia katika kuokoa hadi Sh1.5 milioni kwa mwaka.

Jiko hilo pia limetengenezwa kwa kuwekwa “sensors” za kutoa onyo kunapokuwa na hitilafu wakati wa matumizi yake.

Anaongeza kuwa shule zinaweza kulipia jiko hilo kwa muda wa hadi miaka mitatu.

  • Tags

You can share this post!

Kotut, Wanjiru waingia mbio za Tokyo Marathon, kivumbi...

Jared Mwanduka: Mwanzilishi wa programu ya LearnsoftERP...

T L