• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Farm shield: Kifaa kinachorejelewa kama ubongo wa shamba

Farm shield: Kifaa kinachorejelewa kama ubongo wa shamba

NA SAMMY WAWERU

MATAIFA yaliyoimarika kiteknolojia kuendeleza shughuli za kilimo, kwa kiasi kikuu yamefanikiwa kukabiliana na kero ya njaa na usalama wa chakula.

Yataje; Marekani, Uingereza, India, China, Israili… Haya yakiwa machache tu kuorodhesha.

Israili kwa mfano, ni jangwa ila ni mzalishaji mkuu wa nafaka kama vile ngano, mtama na mahindi.

Isitoshe, nchi hiyo ni guru katika kilimo cha zabibu, maparachichi maarufu kama avokado, kiwi, na maembe, kati ya matunda mengineyo.

Ufanisi wa Israili unatokana na ukumbatiaji wa mifumo na teknolojia za kisasa katika zaraa.

Licha ya kuwa taifa kame, hakuna tone la maji ya mvua linalopotea.

Huteka na kuvuna maji, wanayatumia kunyinyizia mimea na mashamba.

Kampuni ya Synnefa, ni miongoni mwa wadauhusika katika sekta ya kilimo wanaojaribu kuleta suluhu kwa wakulima hapa nchini.

Huunda vifaa na zana za kilimo, hasa za kisasa.

Mojawapo ni kifaa maalum aina ya Farm shield, ambacho majukumu yake ni kufuatilia na kudhibiti shughuli za kilimo cha mvungulio – greenhouse farming.

Almaarufu ubongo wa shamba, Shalom Mbugua ambaye ni mtaalamu wa masuala ya ukuaji wa biashara katika kampuni hiyo anasema kina sensa zinazowekwa kwenye udongo.

Mtaalamu wa masuala ya ukuaji wa biashara Synnefa, Shalom Mbugua akionyesha sensa za Farm shield zinazowekwa udongoni kukusanya data. PICHA | SAMMY WAWERU

Sensa aidha zinakusanya data kama vile kiwango cha maji na joto udongoni, madini; Nitrojini, Potassium na Calcium, levo ya asidi na alikali (pH), na hadhi ya miale ya jua, kisha zinatuma jumbe kwa kifaa hicho cha kiteknolojia.

“Farm shield ina kadi ya kumbukumbu (memory card), na utendakazi wake unaunganishwa na simu. Jumbe zinasambazwa kwa mkulima kwa njia ya mawimbi, achukue hatua,” Shalom afafanua.

Cha kustaajabisha na kuridhisha ni kwamba, mkulima anapoarifiwa popote pale alipo anaweza kuchukua hatua kwa kubofya ushauri na hatua za dharura.

“Kwa mfano, ikiwa ni kiwango cha maji kimepungua au kuwa kingi, joto, na mahitaji mengineyo, anadhibiti hali akiwa mahali alipo,” mtaalamu huyo aelezea.

Hali kadhalika, Farm shield inafungua na kufunga tapu kusambaza maji.

Shalom anasema, jumbe zinatumwa kwa njia ya arafa fupi ya simu au barua pepe.

“Matumizi ya maji na mbolea, yanadhibitiwa,” asema.

Synnefa ilikuwa kati ya kampuni na mashirika yaliyohudhuria Maonyesho ya Kimataifa ya Agritech Africa, yaliyofanyika katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi.

Maonyesho hayo ya makala ya saba, wakulima na wafugaji hususan wa ng’ombe wa maziwa na kuku, walipata fursa kujifunza mifumo na teknolojia za kisasa.

Shalom aliambia Akilimali kwamba Farm shield inagharimu Sh55,000.

“Kando na kutumika kwenye vivungulio, kifaa hicho pia kinaweza kukumbatiwa na wanaoendeleza shughuli za kilimo maeneo tambarare,” akasema.

Alidokeza kwamba, kwa sasa Synnefa ina jumla ya wakulima 10 nchini waliokumbatia matumizi ya kifaa hicho kuendeleza zaraa.

 

  • Tags

You can share this post!

Kenya Kwanza yadai bandari zote nchini zimeuzwa kwa Dubai

Nitajenga kwangu kasri la kula na kunywa – Rigathi

T L