• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Fisi wasifiwa kwa kutuliza walevi 

Fisi wasifiwa kwa kutuliza walevi 

NA RICHARD MAOSI

WARAIBU wa pombe katika barabara ya Naivasha – Maai Mahiu wanalazimika kurejea makwao mapema kufuatia kero ya fisi wanaowahangaisha.

Fisi hao wanatoka katika Mbuga ya Wanyama ya Longonot.

Aidha, sehemu kubwa katika Shirika la Huduma za Wamyamapori Nchini (KWS) iliyoko karibu na mji wa Naivasha, ambayo vilevile inatumika kama hifadhi ya wanyama pori pia haijasazwa.

Ni jambo ambalo limewasukuma wakazi kujichukulia hatua mkononi mwao na mara nyingine kuua fisi ambao wamekuwa ni tishio kwa maisha yao na hata mifugo.

Licha ya hatari inayowakodolea macho wakazi, baadhi ya akina mama kutoka kijiji cha Kihoto wamejitokeza kusifu fisi kwa kile wanachodai kama huwafanya wanaume wao kurudi nyumbani mapema.

“Ingawa fisi wanafaa kudhibitiwa, wametusaidia kurekebisha mienendo ya waume zetu na hatusumbuani sana kama zamani kwa sababu ifikapo jioni, huwa wamefika nyumbani mapema kwa kuhofia kutafunwa na fisi,” anasema Loise Wangare mkazi wa Longonot.

Bi Loise anasema kimaumbile, fisi ni waoga sana lakini hupata windo rahisi pale wanapokumbana na walevi usiku.

Hata hivyo, sio rahisi kushambulia binadamu labda iwe ni watoto.

Anasema walevi wamekuwa wakivamiwa kwa urahisi na fisi kwa sababu hawana uwezo wa kutoroka pindi wanapokutana na wanyama hao njiani jambo ambalo vilevile limeharibu biashara ya wagema mitaani.

Anaomba KWS kuangazia suala hili, hasa muda huu ambapo visa vya wanyama kuzurura mitaani vimeongezeka.

Mfano, kuna viboko kutoka Ziwa Naivasha na Nyati wanaozurura karibu na eneo la Weigh Bridge barabara ya kuelekea Nakuru.

Alfred Kimutai mwendeshaji boda na mkaazi Karagita, anasema yeye hulazimika kufunga kazi kabla ya saa mbili mbili jioni kwa sababu barabara za kuelekea South Lake huwa hazipitiki nyakati za usiku.

“Hapa ni kama makazi ya wanyamapori hasa viboko, nyati na fisi,” akasema.

Kimutai anasema haiwezekani kwa wapita njia kutumia barabara za kuelekea South Gate, ikimaanisha kuwa ni pigo katika sekta ya utalii ikizingatiwa kwamba ni eneo ambalo hupokea idadi kubwa ya wageni.

Agosti 2022, wakazi wa Naivasha waliandamana kulalamikia dhidi ya wanyamapori hasa viboko ambao wamekuwa wakiharibu mazao katika mashamba yao hasa nyakati za usiku.

Aidha 2019, KWS ilipokea malalamishi kutoka kwa wakazi baada ya takriban simba wanane kuonekana wakizurura katika eneo la Moi Ndabi na Ndabibi viungani mwa mji wa Naivasha.

  • Tags

You can share this post!

Wahuni wanaohangaisha walevi kwa pingu 

Magwiji wa shindano la kunywa soda na kula boflo watuzwa  

T L