• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Wahuni wanaohangaisha walevi kwa pingu 

Wahuni wanaohangaisha walevi kwa pingu 

NA SAMMY WAWERU 

WALEVI wanaotoka kwenye baa na klabu majira ya usiku mitaa kadha Nairobi, wamegeuka kuwa kitoweo cha wahuni wanaowahangaisha kwa kutumia pingu.

Wahalifu hao, wanajifanya kuwa maafisa wa polisi wanaoshika doria.

Mitaa ya Githurai 44, Zimmerman, Githurai 45, Kahawa West na hata Kasarani, ni kati ya inayoshuhudia visa vya aina hiyo.

Maeneo ya burudani yaliyo Thika Road (barabara kuu inayounganisha Jiji la Nairobi na Thika) na Kamiti Road, wanaotoka kujivinjari wanaandamwa na wahalifu hao.

Mwendo wa saa tano hivi za usiku, katika mtaa wa Githurai 44 tunakutana na jamaa wawili; mwanamume na mwanamke.

Tuko kwenye kundi la watu wanne, na ghafla tunasimamishwa na jamaa hao wanaojitambulisha kama maafisa wa polisi.

“Nyinyi ndio mnakiuka sheria za unywaji pombe?” wanauliza.

Mwanamume anaongeza, “Sisi ni askari, mna makosa.”

Akijitambulisha, anatoa pingu huku akitutishia kwamba atatuchukulia hatua ‘za kisheria’.

Tunamshinikiza atoe kitambulisho cha kazi, cha askari na ndipo inabainika kuwa ni polisi bandia.

Cha kushangaza zaidi, wanaonekana wakitafuna miraa.

Ni kutokana na ukakamavu na ujasiri wetu wanatoweka, wakihofia drama kuzuka kwani eneo tulilokutana nao ni karibu na mojawapo ya maeneo ya burudani Githurai 44.

Mmoja wa wahudumu wa baa kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali alidokeza kwamba majambazi wanatumia ujanja wa pingu kuhangaisha wanaotoka kujivinjari.

“Hicho si kisa cha kwanza. Vimeripotiwa visa kadhaa vya wahuni kuhangaisha walevi, hasa wanapotoka kujienjoi. Huwa na pingu tusizojua wanakozitoa,” mhudumu Neema (si jina lake halisi kwa sababu za kiusalama) anaelezea.

Kando na mtaa wa Githurai 44, visanga vya aina hiyo, vinashuhudiwa Zimmerman, Githurai 45, Kahawa West na Kasarani.

“Wanaandama wanaonekana kulemewa na makali ya pombe, wanawatia pingu kisha wanawaporea gizani,” anasema Kevin, si jina lake kamili, ambaye amewahi kuwa mwathiriwa.

Anadokeza kwamba alipojipata katika tukio na wahuni hao, aliporwa simu na Sh30 alizokuwa amesalia nazo.

“Hakunipeleka kwa kituo chochote cha polisi, na isitoshe hawasemi wanakofanyia kazi (kituo wanachohudumu),” asimulia.

Kevin anashukuru Mungu kwani hawakumdhuru.

Kituo cha Polisi cha Kiamumbi, Kahawa West, Githurai 44, na cha Kasarani, ndivyo vinajukumika kuimarisha usalama maeneo yanayotajwa kuathirika.

  • Tags

You can share this post!

Wanawake wahalifu walivyomgeuza kiwete

Fisi wasifiwa kwa kutuliza walevi 

T L