• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Gachagua ashambulia Raila akimtaja kuwa mwelekezi wa mawaziri wa utawala wa Kenyatta 

Gachagua ashambulia Raila akimtaja kuwa mwelekezi wa mawaziri wa utawala wa Kenyatta 

NA SAMMY WAWERU 

NAIBU wa Rais Rigathi Gachagua amezidi kukosoa utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, akisema awamu yake ya pili “alikuwa akipata amri kutoka kwa upinzani”. 

Katika matamshi yaliyoonekana kuelekezewa kinara wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, Bw Gachagua alidai Baraza la Mawaziri la Rais Kenyatta lilikuwa chini ya uangalizi wa Bw Odinga.

Gachagua aidha alimtaja kiongozi huyo wa upinzani kama “raia binafsi aliyekuwa na mamlaka makuu katika serikali ambayo hakushiriki kuunda”.

“Utawala wa Uhuru Kenyatta, mawaziri na makatibu walikuwa wakielekezwa na raia binafsi,” Naibu Rais alisema.

Alitoa tetesi hizo Ijumaa, Agosti 18, 2023 wakati akifunga rasmi Kongamano la Ugatuzi 2023 lililofanyika katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Machi 2018, Rais Kenyatta na Bw Odinga walizika tofauti zao za kisiasa kupitia salamu za maridhiano maarufu kama Handisheki.

Mapatano hayo yalionekana kutoridhisha Rais wa sasa, William Ruto.

Dkt Ruto alihudumu kama Naibu Rais katika serikali ya Jubilee, na pamoja na wandani wake walilalamikia kutengwa kwenye serikali waliyoshiriki kuunda.

Bw Kenyatta aliunga mkono Raila Odinga wa Azimio kumenyana na Ruto – Kenya Kwanza katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022 kumrithi kuingia Ikulu, japo aliangushwa na Dkt Ruto.

Waziri Mkuu huyo wa zamani akiendelea kukosoa utawala wa Kenya Kwanza, Bw Gachagua amemtaka kuchukua jukumu lake kama mpinzani na mkosoaji wa serikali.

“Uchaguzi ulifanyika na Wakenya wakatoa maamuzi, hivyo basi, wewe endeleza wajibu wako kama mkosoaji wa serikali,” Naibu Rais akamwambia Raila Odinga.

Bw Odinga aidha alipinga matokeo ya kura za urais 2022, katika mahakama ya juu zaidi nchini akilalamikia udanganyifu na wizi wa kura.

Kesi yake, hata hivyo, ilifutiliwa mbali na korti, kwa kile mahakama ilisema ni kukosa ushahidi wa kutosha.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Luciano Spalletti achukua mikoba ya kudhibiti Azzurri

Taswira ya Tamasha za Kitaifa za Muziki 2023 zinazofanyika...

T L