• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Gachagua: Kumeza ODM kama Jubilee kutatufanya tuumwe na tumbo

Gachagua: Kumeza ODM kama Jubilee kutatufanya tuumwe na tumbo

NA SAMMY WAWERU

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameendeleza mashambulizi yake kwa chama kikuu cha upinzani, Orange Democratic Movement (ODM), akidai kuwa kukiingiza ndani ya serikali ya Kenya Kwanza kutasababisha matatizo zaidi.

Katika video inayosambaa mitandaoni, Naibu Rais anaskika akisuta chama hicho kinachoongozwa na Bw Raila Odinga, akikirejelea kama “chama sumbufu”.

Bw Gachagua alitoa kauli hiyo akiwahutubia wakazi wa Eldoret, kufatia ziara yake ya majuzi Bonde la Ufa.

“Unajua tulikubali chama cha Jubilee tukakimeza…Lakini kujaribu hivyo hivyo na ODM kutasababisha maumivu ya tumbo,” Naibu Rais alitangaza.

Maoni ya Gachagua yalihusiana na mazungumzo yanayoendelea kati ya Azimio la Umoja-One Kenya na Kenya Kwanza, yanayolenga kupunguza joto la kisiasa linalozidi kuongezeka nchini.

Mrengo wa Kenya Kwanza inaongozwa na Rais William Ruto, huku upande wa Azimio ukiwa chini ya Bw Raila Odinga.

Upinzani umesitisha kwa muda maandamano yake kwa heshima ya waathirika wa ukatili wa polisi na kuwezesha mchakato wa mazungumzo.

Mazungumzo hayo ya mapatano yanaongozwa na Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Kimani Ichung’wa (Kenya Kwanza) na Bw Kalonzo Musyoka (Azimio), pamoja na wajumbe wengine wa timu za kiufundi kutoka pande zote mbili.

“Tumetoa maagizo kuwaruhusu kushiriki mazungumzo, lakini hatupaswi kusikia kuhusu Handisheki,” Naibu Rais akasema.

Rais William Ruto pia ameelezea msimamo wake kuhusu suala hilo, akikataa uwezekano wa Handisheki kati yake na upinzani.

Hata hivyo, kiongozi wa Azimio, Bw Raila Odinga, amepuuzilia mbali madai ya kutaka Handisheki na kushirikishwa kwenye serikali ya Ruto, akisisitiza kwamba lengo lake ni kuhakikisha gharama ya maisha inashushwa.

Odinga pia anataka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kufanyiwa marekebisho, ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kwa sava kubaini aliyeibuka mshindi katika uchaguzi mkuu Agosti 9, 2023 kiti cha urais.

Maandamano ya upinzani yaliyolenga kushinikiza serikali inayoongozwa na Dkt Ruto kupunguza gharama ya maisha, yalipigwa marufuku.

Idadi kadha ya vifo na majeruhi kutokana na ukatili wa polisi iliandikishwa wakati wa maandamano.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Aliyejiteketeza kwa ugumu wa maisha akimbizwa Coast General

Man-City waangusha Sevilla na kuongeza taji la UEFA Super...

T L