• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Gachagua: Wakenya wasio na kazi hawatatozwa ushuru

Gachagua: Wakenya wasio na kazi hawatatozwa ushuru

Na WANGU KANURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amewaahidi Wakenya wasio na kazi kuwa hawatatozwa ushuru.

Huku mjadala wa Mswada wa Fedha 2023 ukishika kasi, Bw Gachagua akitetea mswada huo alisema kuwa lengo kuu ni kuwasaidia vijana kupata kazi.

Akizungumza katika hafla ya mageuzi ya sera za kahawa Meru, Bw Gachagua aliwauliza wabunge wanaonuia kuupinga mswada huo kuangazia lengo la kuwapatia vijana ajira.

“Mswada wa nyumba umegawanywa mara mbili. Asilimia 30 ni kuwasaidia Wakenya kupata nyumba ili wawache kuishi kwenye mitaa ya mabanda. Asilimia 70 ni kusaidia vijana kupata ajira mbalimbali,” akasema.

Aliongeza: “Hao vijana hakuna mtu anawaambia kuwa watakatwa chochote kwa sababu hawana mshahara. Tunawaambia Wakenya wasio na ajira kutoshughulika na kelele zinazopigwa kuhusu mswada huu kwani hakuna anayewakata mshahara. Mtakapopata kazi, na muanze kukatwa basi mtapiga kelele wakati huo.”

Akiwanyooshea kidole cha lawama viongozi, Bw Gachagua alisema kuwa wao ndio wanaokataa kulipa ushuru akisisitiza kuwa sharti watalipa.

“Nawaambia hivi, uchochezi huu utafikia kikomo. Wakati tutapitisha mswada huu utafanywa sheria, na hawa mahasla wote hakuna mtu atakayekuwa na shughuli na wao. Hao watu wasio na jukumu lolote kwa Wakenya ndio wanaopiga kelele sana na watakuwa wakizungumzia miti,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Itumbi aachiliwa katika kesi ya kudai kulikuwa na njama ya...

Viongozi wahimizwa kupiga jeki wanamichezo

T L