• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:01 PM
GWIJI WA WIKI: Dotto Rangimoto

GWIJI WA WIKI: Dotto Rangimoto

MWANDISHI asiye na ujuzi wa kutumia lugha kwa ufundi hukosa uhuru wa kusema anachokitaka kwa jinsi anavyotamani kifikie hadhira lengwa.

Ingawa uhuru wa mwandishi umo katika utashi na falsafa, lugha ndicho kitovu cha fasihi na kamba inayovuta hadhira kwa dhamira ya sanaa yenyewe.

Dotto Daudi Rangimoto anaamini kuwa kigezo cha kubaini mwandishi bora wa fasihi ni uwezo wake wa kutumia fani kusuka na kuwasilisha maudhui.

“Mwandishi hawezi kuweka mipaka baina ya fani na maudhui wala kutawala vyema sanaa ikiwa msingi wa lugha yake ni mbovu,” anatanguliza.

“Uandishi ni kipaji kinachoibuliwa, kunolewa na kukuzwa wala si taaluma inayofundishwa shuleni. Huwezi ukamfunza mtu kuwa msanii!”

“Iwapo unaandika riwaya kwa mfano, na hujui misingi ya sanaa ya aina hiyo, basi utatatizika sana. Unaweza kujaribu, lakini kazi utakayoitoa itakuwa duni mno.”

“Anavyoshikilia Prof Fikeni E.M.K. Senkoro, itakuwa ‘riwaya mahubiri’ au ‘riwaya maelezo’ isiyo na simulizi zenye visa, matukio, migogoro, wahusika na mandhari,” anasema Dotto kwa kusisitiza kuwa kazi nzuri ya fasihi ni ile inayounganisha vyema ubunifu na uhalisia.

Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Dotto katika umri mdogo. Akiwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, aliwahi kutunga shairi la kuomboleza kifo cha mamake mzazi na kazi hiyo ikamchochea kuandika hata zaidi.

Kufikia sasa, amechapisha jumla ya vitabu vitatu, ikiwemo diwani ‘Mwanangu Rudi Nyumbani’ iliyoshinda Tuzo ya Kiswahili ya Safal (Mabati)-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika 2017. Alifyatua ‘Wivu Bustani ya Edeni’ mnamo Septemba 2022 na akatoa riwaya nyingine ‘Nakupenda Jini Maimuna’ mwanzoni mwa Februari 2023.

Utunzi wa mashairi na kazi bunilizi umemzolea Dotto tuzo nyingi za haiba kubwa. Alishinda Tuzo ya Meya wa Dar es Salaam (Ushairi) mnamo 2016 na shairi lake ‘Mjomba Nataka Kusoma’ likaingia ndani ya orodha ya 10-bora kwenye Tuzo ya Ushairi ya Ebrahim Hussein 2017.

Hadithi yake ‘Mama Yuko Wapi?’ iliambulia nafasi ya pili kwenye Tuzo za Kimataifa za Kalahari mnamo 2020 na riwaya ‘Ujanajike’ ikaibuka ya kwanza katika Safal-Cornell Fasihi ya Kiafrika 2022 na kumfanya Dotto kuweka rekodi ya kuwa mwandishi wa kwanza kuwahi kushinda tuzo hiyo mara mbili, tena katika vitengo viwili tofauti.

Dotto alizaliwa Agosti 2, 1986 katika eneo la Morogoro nchini Tanzania. Ndiye kitinda mimba katika familia ya watoto tisa wa marehemu Bi Rehema Chamchua na marehemu Bw Daudi Cyprian Rangimoto.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Chamwino iliyoko Morogoro Mjini kabla ya kujiunga na shule ya upili ya Morogoro mnamo 2000.

Ingawa alikuwa na ndoto ya kuwa mtaalamu wa masuala ya uchumi, maradhi yalizima ghafla mshumaa wake wa masomo na akajitosa katika biashara na kilimo baada ya kupona. Mbali na shughuli hizo za ujasiriamali, Dotto kwa sasa ndiye afisa wa mitandao ya kijamii katika chama cha kisiasa cha ACT Wazalendo, Tanzania.

“Msingi wa kuandika ni kusoma. Asomaye sana huwa mwandishi mzuri sana. Mwandishi bora sharti ajisukume kujifunza mambo mapya. Lazima afanye utafiti wa kina, aulize wajuao zaidi yake na asome kazi za taaluma mbalimbali,” anashauri.

“Waandishi tushiriki tuzo kila zinapotokea kwa sababu huandaliwa kwa ajili yetu. Usijinyime fursa iwapo unatimiza vigezo vya kushiriki. Tutawavunja moyo waandalizi wa mashindano ya sampuli mbalimbali tukikosa kuyachangamkia,” anaongezea.

  • Tags

You can share this post!

Watoto 7 milioni wameathiriwa na tetemeko, UN

Salernitana wamtimua kocha kwa mara ya pili baada ya siku...

T L