• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
Watoto 7 milioni wameathiriwa na tetemeko, UN

Watoto 7 milioni wameathiriwa na tetemeko, UN

NA MASHIRIKA

NEW YORK CITY, AMERIKA

UMOJA wa Mataifa umesema zaidi ya watoto 7 milioni waliathiriwa na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea wiki jana Uturuki na Syria.

Umoja huo umesema hayo huku shughuli za kuwatafuta waliokwama kwenye vifusi vya majengo zikikaribia kukamilika.
Tetemeko hilo liliitikisa sehemu ya katikati mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria alfajiri Jumatatu wiki jana, na kufuatiwa na jingine dakika 10 baadaye, likiharibu vibaya miundombinu katika miji 12.

Hata hivyo, kuna wasiwasi mkubwa kuwa huennda maelfu ya watoto waliangamia kwenye janga hilo.

Msemaji wa shirika la Umoja wa huo la kuwahudumia watoto (UNICEF), James Elder, alisema nchini Uturuki pekee jumla ya watoto walioathirika katika mikoa 10 iliyokumbwa na tetemeko hilo kubwa ilifikia milioni 4.6 huku Syria ikiwa na watoto milioni 2.5 walioathiriwa na janga hilo.

“Nchini Uturuki, jumla ya watoto wanaoishi katika majimbo 10 yaliyokumbwa na mitetemeko miwili ya ardhi ilikuwa watoto milioni 4.6. Nchini Syria, watoto milioni 2.5 wameathirika,” akasema Elder.

“UNICEF inahofu kwamba huenda watoto wengi waliangamia,” akasema Elder, akiongeza kwamba huenda ni jambo la kusikitisha.

Tetemeko hilo lilibomoa majengo katika maeneo hayo, huku uharibifu huo ukizidisha uharibifu ambao umekuwa ukishuhudiwa katika miji mingi nchini Syria kutokana na vita ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa miaka mingi.
Tetemeko hilo lilikuwa la na uzito wa 7.8 kwenye vipimo vya Ritcher.

Kadhalika, tetemeko hilo limetajwa kuwa baya zaidi kukumba Uturuki na Syria katika karne hii.

Wataalamu walisema ukubwa wake ulihisiwa pia katika mataifa jirani kama Cyprus na Lebanon.

Kulingana na Umoja wa Mataifa na serikali ya Syria, watu zaidi ya 40,000 waliangamia kwenye tetemeko hilo hatari.

Mamlaka ya Uturuki ilisema watu 35,418 walipoteza maisha yao nchini humo, huku zaidi ya watu 5,800 wakiuawa nchini Syria.

Kadhalika, iliripotiwa kwamba mbwa wawili waliokolewa siku sita baada ya tetemeko hilo kutokea.

Kufuatia maafa makubwa yaliyotokana na tetemeko hilo, mataifa mbalimbali duniani yanaendelea kupeleka misaada katika maeneo mbalimbali.

  • Tags

You can share this post!

Kocha Aussems awaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi...

GWIJI WA WIKI: Dotto Rangimoto

T L