• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
GWIJI WA WIKI: Kelvin Nyakundi

GWIJI WA WIKI: Kelvin Nyakundi

NA CHRIS ADUNGO

BAADA ya kukamilisha KCSE mnamo 2019, Kelvin Nyakundi alitamani sana kusomea uanahabari. Hiyo ni taaluma aliyovutiwa nayo tangu akiwa mtoto wa umri mdogo.

Alikuwa na mazoea ya kuiga wanahabari nguli wa humu nchini huku akijirekodi kwenye kanda. Alikuwa maarufu miongoni mwa wanafunzi wenzake na ‘sauti yake ya utangazaji’ ikamfanya ateuliwe mwenyekiti wa chama cha uanahabari katika shule ya upili ya Nyambaria iliyoko Kaunti ya Nyamira.Hata hivyo, ndoto hiyo ya kuwa mtangazaji wa taarifa za habari runingani ilikatika ghafla mnamo 2020 na akahiari kujiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kusomea ualimu (Hisabati/Bayolojia).

Akiwa huko, alikutana na mhubiri Christopher Munene aliyetambua kipaji chake cha uimbaji na akamhimiza ajitose kikamilifu katika uinjilisti na fani ya uanamuziki.

Ingawa mazingira alimokulia yalichangia pakubwa umilisi wake wa Kiswahili, upekee wake katika ulingo wa muziki ni upevu wa masimulizi, ukwasi wa msamiati na ujuzi wa kuita na kusana maneno kwa ufundi wa kuajabiwa.

“Mbali na kuwa chanzo cha kujifunzia utamaduni na kuhifadhi historia, muziki ni namna ya kujieleza kwa ubunifu. Nyimbo za injili zinastahili kuipa jamii mwelekeo na kusawiri uhusiano wa karibu kati ya binadamu na Mungu,” anasema.

Nyakundi amejikuza sana kisanaa tangu Bw Best Bard amsaidie kurekodi wimbo wake wa kwanza, ‘Unifunze Kuvumilia’, mnamo Septemba 2020. Kibao hicho kilimchochea kufyatua wimbo ‘Uinuliwe Yesu’ mnamo Aprili 2021 kabla ya kutoa ‘Nahitaji Bwana’, ‘Linda Imani’, ‘Yuko Hapa Mungu’ na ‘Ainua Yesu’ kati ya Januari na Julai 2022.

Weledi wake katika uimbaji ulimwezesha kutamalaki tuzo za MKUSA Awards zilizotolewa na MKU mnamo Julai 1, 2022. Baada ya kushirikiana na msanii chipukizi Diana Mutile kucharaza kibao ‘Overcomer’ mwanzoni mwa Septemba, Nyakundi anatazamia sasa kuachilia wimbo ‘Heri Mungu’ mnamo Oktoba 2022.Anajivunia nyimbo saba ambazo amezihifadhi katika albamu, ‘Unifunze’, aliyoizindua wikendi iliyopita katika ukumbi wa MKU Indoor Arena mjini Thika.

Hafla hiyo iliyonogeshwa na baadhi ya waimbaji wabobevu wa nyimbo za injili, ilihudhuriwa na maelfu ya watu akiwemo Bw Robert Burale.

Zaidi ya kuchomoa kibao kipya kila mwezi, Nyakundi anapania pia kushirikiana na baadhi ya wasanii wazoefu kutoka Kenya na Tanzania kueneza Ukristo kwa kutumia nyimbo.

Yeye hutumia ujuzi wake wa ualimu kuwaelekeza vijana katika masuala ya maadili, namna ya kujikuza kisanaa na jinsi ya kujitegemea na kukabili changamoto mbalimbali maishani.

Amekuwa akifanya hivyo tangu Machi 2021 kupitia kipindi ‘The Kelvin Duo Show’ anachokiendesha kwa pamoja na Kelvin Baraka, Geoffrey Manasseh na James Katana kupitia mtandao wa Instagram.

Nyakundi alizaliwa na kulelewa katika kijiji cha Kehancha, eneo la Kuria, Kaunti ya Migori. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watano wa Bi Eucabeth Nyaboke na mwalimu Shem Bogonko.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Kehancha Educational Centre (2007-2014) kabla ya kujiunga na Nyambaria High (2015-2018).

Alifanya KCSE kwa mara ya pili katika shule ya upili ya Riokindo, Kaunti ya Kisii mnamo 2019 baada ya kutofaulu vyema katika jaribio la kwanza mwaka wa 2018. Atahitimu ualimu chuoni MKU mnamo Disemba 2023.

  • Tags

You can share this post!

Kenya kuandaa handiboli ya Zone 5 ya U18 na U20 Oktoba

Hisia mseto za wabunge kuhusu hotuba ya Rais Ruto

T L