• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
GWIJI WA WIKI: Martin Munene

GWIJI WA WIKI: Martin Munene

NA CHRIS ADUNGO

INGAWA Martin Munene Micheni ni mwanahabari kitaaluma, kinachomlisha na kumvisha kwa sasa ni sanaa ya uigizaji ambayo imempa fursa ya kuvalia kofia nyingi katika ulingo wa filamu.

Kubwa zaidi katika maazimio yake ni kuwa miongoni mwa wasanii watakaotikisa ulimwengu wa uigizaji kwa kufyatua michezo ya runingani itakayokubalika kimataifa.

Analenga pia kupanua wigo wake wa ujasiriamali, kuwa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na kurejea katika tasnia ya uanahabari akiwa ripota na msomaji wa taarifa runingani huku akilea vipaji vya waigizaji chipukizi katika ngazi na viwango tofauti.

Baada ya kukamilisha KCSE mnamo 2012, Munene alipata kazi ya uripota katika idhaa ya Hero Radio 99.0 FM Nakuru kutokana na ukubwa wa uwezo wake katika Kiswahili.

Hata hivyo, kipawa cha uigizaji kilimteka baada ya muda mfupi na akajitosa katika fani ya filamu akiigiza mhusika Murume katika mchezo ‘Habibu’ (2014, Citizen TV) kisha akawa mwelekezi wa mchezo ‘Arosto’ (2014, K24 TV).

Ilikuwa hadi 2018 alipoajiriwa na kampuni ya Jiffy Pictures inayomilikiwa na wanahabari Lulu Hassan na Rashid Abdalla kuwa props master katika mchezo ‘Maza’ (Maisha Magic East – DStv).

Alidhihirisha kiwango cha juu cha ubunifu na akaridhisha mabosi wake waliomwaminia fursa ya kuwa prodyusa msimamizi wa michezo ‘Aziza’ (2019), ‘Maria’ (2020), ‘Zora’ (2021) na ‘Sultana’ (2022).

Munene alikulia na kulelewa katika mtaa wa London viungani mwa jiji la Nakuru.

Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto watatu wa Bw Fredrick Micheni na Bi Harriet Kainyu.

Alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Kimathi jijini Nakuru kabla ya kujiunga na Moi Primary Nakuru (2005-2007) kisha Moi Secondary Nakuru (2008-2012).

Alisomea uanahabari na mawasiliano ya umma katika Chuo cha Kiufundi cha Mombasa (TUM) kati ya 2014 na 2015.

“Baba alikuwa shabiki mkubwa wa vipindi na taarifa za NTV. Niliiga baadhi ya wanahabari wazoefu wa runinga hii katika juhudi za kupalilia kipaji cha utangazaji kilichoanza kujikuza ndani yangu utotoni,” anasema.

Akiwa sekondari, Munene aliteuliwa mwenyekiti wa chama cha uanahabari na kiranja mkuu wa shule.

Martin Munene wakati wa mahojiano. PICHA | CHRIS ADUNGO

Nyadhifa hizo zilimpa majukwaa tele ya kuwasilisha mbele ya hadhira, akanoa kipaji cha ulumbi na kuinua kiwango chake cha umilisi wa lugha.

“Kuhutubia wanafunzi na kusoma habari za matukio mbalimbali gwarideni kulinishajiisha sana. Nilikariri pia mashairi ya sampuli nyingi katika mashindano anuwai na kuwakilisha shule yangu ya upili katika tamasha za kitaifa za muziki na drama,” anaeleza.

Munene anamstahi sana mkewe Lilian Wanjeri anayezidi kuiwekea taaluma yake thamani na mshabaha.

“Kufaulu katika fani ya filamu na tasnia ya uanahabari ni zao la imani, bidii, stahamala na nidhamu. Usiogope kujaribu. Kuna kuweza katika kujaribu na kufeli katika kutojaribu. Kwa hivyo, jaribu,” anashauri.

  • Tags

You can share this post!

Ruto, Raila bega kwa bega

Huwezi ukang’olewa huku ukawania kule, DPP Haji...

T L