• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
GWIJI WA WIKI: Mathias Momanyi

GWIJI WA WIKI: Mathias Momanyi

Na CHRIS ADUNGO

MATHIAS Momanyi alikulia katika familia ya wanahabari na walimu.

Mbali na binamu yake, Walter ‘Nyambane’ Mong’are, wawili kati ya nduguze sita pia ni wanahabari – Lilian Moraa (Sauti Ya Rehema FM) na Vincent Nyambariga aliyekuwa Radio One Tanzania.

Momanyi alizaliwa kijijini Ikuruma, Kaunti ya Kisii na akalelewa Tanzania. Ndiye wa pili katika familia ya watoto saba wa Bw Omar Odari Kienge almaarufu Zephaniah Nyarunda na Bi Rachael Nyatundo – mwalimu na mwimbaji maarufu mzaliwa wa Mbezi, Tanzania.

Momanyi alianza safari ya elimu katika shule ya msingi ya Fez, Dar es Salaam, Tanzania, kabla ya kurejea Kisii mnamo 1986 kujiunga na shule ya msingi ya Ngokoro kisha Motonto, Manga Chache.

Alisomea katika shule ya upili ya Feza, Dar es Salaam, mwanzoni mwa 1993 kabla ya kurudi Kenya kujiunga na shule ya upili ya Musingu, Kaunti ya Kakamega.

Huko ndiko alikofanyia KCSE mwaka wa 1997.

Baada ya kuhitimu ualimu kutoka Chuo cha Asumbi, Kaunti ya Homa Bay mnamo 2002, alielekea Nairobi kufundisha katika shule ya msingi ya Marion (Kahawa West) kisha Makini (Lavington) na Consolata (Westlands).

Ana shahada ya Sayansi ya Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Moi (2005-2008), amesomea masuala ya usimamizi wa biashara katika Chuo Kikuu cha Oxford (2010-2012) na kwa sasa ni mwanafunzi wa uzamili katika Chuo Kikuu cha Moi.

Momanyi alipata mshawasha wa kujitosa katika uanahabari mnamo 2005 baada ya kualikwa Radio Citizen kuchanganua masuala ya Kiswahili.

Alikuwa shabiki mkubwa wa vipindi ‘Kamusi ya Changamka’ na ‘Ukarabati wa Lugha’ vilivyokuwa vikiendeshwa QFM na KBC Radio Taifa mtawalia.

Alianza kushirikishwa katika uendeshaji wa kipindi ‘Bahari ya Lugha’ katika Radio Citizen (2010-2013) na akaajiriwa kuwa mwanahabari wa Taifa Leo.

Baada ya kuagana na Radio Citizen na kukatiza mkataba wake Nation Media Group (NMG), alijiunga na KBC Radio Taifa kuwa mtayarishaji mwandamizi wa vipindi mnamo 2013.

Mbali na kusimamia mtandao wa Kiswahili wa KBC Radio Taifa na kuendesha kipindi ‘Sauti ya Mkenya’ kwa ushirikiano na Dorah Manya, Momanyi pia ni nahodha wa kipindi ‘Ramani ya Kiswahili’.

Anashirikiana na Rashid Mwamkondo kutayarisha kipindi ‘Sanaa ya Kiswahili’ katika KBC Channel 1 na alianza kusimamia Kitengo cha Kiswahili mnamo Januari 2022.

Uandishi wa vitabu ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Momanyi tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Kwa pamoja na mwalimu Tom Nyambeka, ni wakurugenzi wa Tarihi Educational Publishers (TEP) tangu Septemba 2021.

Baadhi ya vitabu vya Momanyi kutoka TEP ni ‘Sarafina na Hadithi Nyingine’, ‘Hidaya na Wenzake’ na ‘Haki Yao’.

Baada ya Faulu Publishers kumchapishia ‘Nyota ya Ufasaha’ (2003), aliandika ‘ Lisani za Lufufu’ (2006), ‘Ngoma’ (2007) , ‘Kurunzi ya Marejeleo Halahala (2009) na Kiswahili katika ‘On Point Encyclopedia’ (2015).

EAEP ilimtolea ‘Shujaa ya Mateso’, ‘Hazina na Abdul’ na ‘Taabu za Tabu’ kabla ya Phoenix Publishers kumfyatulia msururu wa ‘Kilele cha Insha’ na ‘Hatua za Kiswahili Rasmi.

Momanyi pia huimba kwa mtindo wa kufokafoka. Jina lake kisanii ni ‘Kamusi Inayotembea’ na kufikia sasa, amecharaza vibao vinne – ‘Wimbi Takatifu’, ‘Mama’, ‘Usidunde’ na ‘Nipo Radhi’.

‘Wimbi Takatifu’ ni wimbo aliotunga baada ya Mong’are aliyepania kuwania urais wa Kenya mnamo Agosti 2022 kurekodi kibao ‘Sweet Banana’.

“Amini kwamba unaweza na usichoke kutafuta. Ruhusu mawazo yako yatawaliwe na fikira za ushindi. Weka Mungu mbele, vumilia, ujitume na usifanye mambo kama wengine. Tenda mema, lakini kumbuka manabii si watu kwao, huchukiwa na watu wao,” anashauri.

  • Tags

You can share this post!

Mbakaji aliyenajisi kanisani asukumwa jela miaka 45

Mwanatenisi Okutoyi aanza kuona matunda ya jasho lake,...

T L