• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Hali ya maisha ilivyo katika ‘Bethlehemu’ ya Shakahola

Hali ya maisha ilivyo katika ‘Bethlehemu’ ya Shakahola

ALEX KALAMA Na FARHIYA HUSSEIN

KIJIJI cha Shakahola, ambacho kimepata umaarufu kwa wiki kadha sasa kwa sababu ya dhehebu la ajabu linalosemekana kuambia waumini wafunge kula na kunywa hadi kufa, ni kijiji kisicho cha kawaida.

Safari ya kufika huko kutoka Malindi inachukua takriban saa moja kwa barabara zinazopitia ndani ya vichaka na misitu.

Mwanamke akiokolewa. Picha / WACHIRA MWANGI

Usalama huko si wa hakika, kwani unapojiandaa kuenda, utaonywa kuhusu waumini sugu wa dhehebu linalohusishwa na mhubiri Paul Mackenzie, aliyekuwa mwanzilishi wa Kanisa la Good News International, ambao wanasemekana wanaweza kushambulia yeyote anayepinga dhehebu lao.

Kituo cha polisi kilicho karibu ni kile cha Langobaya, ambacho hakina magari ya kuwezesha polisi kusafiri.

Kunapotokea dharura, maafisa wa kituo hicho hutatizika kusafiri zaidi ya kilomita 50 hadi Shakahola.

Mwanamke akiokolewa. Picha / WACHIRA MWANGI

Ili wafanye hivyo, gari lazima liombwe kutoka Kituo kikuu cha Polisi cha mji wa Malindi ambacho kiko zaidi ya kilomita 60.

Ndani ya shamba kubwa la Chakama lililozingirwa na vichaka vya miiba ndipo kuna ishara za watu ambao huja hapa kwa mfungo wa kula na kunywa.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa, nyumba ya mhubiri huyo iko kwa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa ekari 10.

Sehemu ambayo nyumba yake imejengwa kumebandikwa jina ‘Bethlehemu’.

Kila eneo ndani ya shamba hilo kubwa limepewa majina ya Kibiblia.

Nyumba ya mmoja wa wafuasi wa mchungaji Paul Mackenzie ambaye amekuwa akiishi msitu wa Shakahola. Picha / ALEX KALAMA

Nyumba zote hapa zimejengwa kwa udongo na nyasi au makuti.

Kijiji cha Shakahola ni mahali tupu sana, na safu za nyumba zilizotelekezwa zimesimama kama walinzi kimya.

Njia ni tulivu, hazina dalili za maisha au shughuli zozote. Ni kana kwamba wakazi wote wa kijiji walitoweka, na kuacha tu vitu vichache vya nyumbani kama vile Biblia zao kama ushahidi wa kuondoka kwao haraka.

Mazingira ni ya wasiwasi na ya kutisha, kana kwamba kuna jambo baya limetokea hapo.

Mazingira ya makazi ya baadhi ya wafuasi wa Paul Mackenzie Shakahola. Picha / ALEX KALAMA

Katika nyumba mbalimbali, hakuna dalili ya mapishi ambayo yamefanywa hivi karibuni.

Vyombo vilivyopo vina vumbi, ishara kuwa wenyeji walikuwa kwa mfungo kwa muda mrefu.

Mita chache kutoka kwa kila nyumba, kuna vichaka.

Mle vichakani pia kuna magodoro na vitambaa, kuashiria baadhi ya wenyeji wamekuwa wakilala huko mwituni.

Mmoja wa maafisa wa polisi aliyendamana nasi alituarifu kuwa, hapa ndipo wafuasi zaidi ya 10 wa dhehebu hilo tatanishi waliokolewa wakiwa hai, huku wengine wanne wakifa njiani kuelekea hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi wiki iliyopita.

Baadhi ya mizigo ya wafuasi wa Paul Mackenzie ambayo walikuwa wamefungasha ili kuondoka ila waliiacha na kutorokea msituni baada ya wanahabari kuzuru ghafla wakiwa wameandamana a polisi. Picha /ALEX KALAMA

Ni kufuatia tukio hilo ambapo Bw Mackenzie alifikishwa mahakamani pamoja na wasaidizi wake kadha, polisi wakapewa siku 14 kuendeleza uchunguzi wao washukiwa wakifungwa seli.

Kila hatua tuliyofanya tulipokuwa tukichunguza kijiji ilikuwa ikifuatiliwa, na kwa wakati huo tulielewa kwa nini ilikuwa muhimu kuwa na maafisa wa usalama kutusindikiza.

Takriban mita 100 kutoka kwa nyumba ya Mackenzie, kuna bwawa la takriban mita za ujazo 10,000, lakini lilikuwa limekauka.

Bwawa kubwa la ujazo wa maji ambalo lilichimbwa ndani ya msitu wa Shakahola na mchungaji tata Paul Mackenzie. Picha /ALEX KALAMA

Baadhi ya watu waliookolewa kutoka kwa dhehebu hilo walikuwa wametoka maeneo ya mbali, Magharibi ya Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Ufukuaji makaburi Shakahola waanza

Miili ya watoto 2 kati ya 3 iliyofukuliwa Shakahola

T L