• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Hatujaona hicho chakula cha Sakaja, shule zalia kuhusu mradi wa Dishi na Kaunti

Hatujaona hicho chakula cha Sakaja, shule zalia kuhusu mradi wa Dishi na Kaunti

Na FRIDAH OKACHI

SHULE za msingi za umma, katika Kaunti ya Nairobi, zinasubiri kujumuishwa katika mpango maalumu wa chakula almaarufu ‘feeding programme’ katika awamu ya pili.

Kaunti ya Nairobi ina shule 225 za umma. Katika awamu ya kwanza ni shule 45 zilizopokea mpango huu wa chakula kwa wanafunzi kutoka kwa serikali ya Kaunti.

Mtaa wa Korogocho, eneo bunge la Ruaraka, mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Daniel Comboni, Bi Dorcus Musila, ana matumaini ya kufikiwa na mpango huu wa chakula kwa wanafunzi.

Bi Musila alielezea Taifa Leo kuwa, kwa miaka mitatu akiwa shuleni humo, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakikosa kufika shuleni kwa kukosa chakula na kusababisha matokeo duni.

“Mradi huo ni wa manufaa iwapo Gavana Johnson Sakaja ataweza kutekeleza. Tumesubiri kwa muda. Nina uhakika wanafunzi wangu wakipata chakula hicho watafanya vizuri zaidi. Pia ni afueni kwa mzazi kwa kuwa atakuwa akitumia Sh5 kila siku,”alisema huku akitabasamu.

Rose Muthoni ambaye ni mzazi katika shule hiyo, anaomba Bw Sakaja kuendeleza mradi huo kwa haraka.

“Gavana ajumuishe shule zote. Mimi naona watoto wa jirani wakija na chakula nyumbani, kama mama wa watoto watatu, wawili wakija nacho nitakuwa nimesaidika. Nitajua nina jukumu la kutafuta kiamsha kinywa peke. Maisha ni magumu,”alisema Bi Muthoni.

Katika Shule ya Msingi ya Ngong Forest, mwalimu mkuu alisema Bw Sakaja amekuwa akitoa ahadi kuwa wanafunzi wa shule hiyo watahusishwa kwenye mpango wa chakula kwa wanafunzi.

Mwalimu Mkuu huyo alisema tumaini lake ni kuona shule hiyo inajengewa eneo la mapishi, jambo ambalo halijatekelezwa.

Beker Clarence ambaye ni mzazi wa watoto wanne, katika shule hiyo, amesikitishwa na jinsi muda unavyosonga kabla ya wanawe kupata chakula huku muhula wa tatu ukielekea kutamatika.

“Wacha shule zote za umma zipewe kwa wakati mmoja. Na sisi kama wazazi tumsaidie Gavana kwa kulipa Sh5 kila siku. Kuna shule zinalipa Sh15, kwa mradi kama huo wa mbunge,” alisema Bw Clarence.

Septemba 26, 2023, Mwakilishi wa Wadi ya Gatina Kennedy Sakwa, alimuandikia barua Spika wa Kaunti ya Nairobi akitaka kufahamishwa jinsi Sh5 zinazochukuliwa kutoka kwa mwanafunzi, zinaelekezwa kwenye akaunti gani.

Kaunti ya Nairobi ilipitisha bajeti ya 2023/2024 na kutenga Sh1 bilioni kushughulikia chakula cha wanafunzi.

Mwezi Septemba 2023, mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alitoa madai kuwa mradi wa Dish na County ni wa kufyonza pesa za umma. Mbunge huyo alidai kuwa mradi huo ulioazishwa Agosti 2023 haujanufaisha watoto wa Kaunti ya Nairobi.

“Kila shule inahitaji kuwa na mahala pake pa mapishi ambako kuna wafanyakazi. Vyumba 10 vya mapishi vilivyojengwa haviwezi kuwalisha mamia ya wanafunzi, lakini kwa mtu kama yeye hawezi kuelewa ukweli mdogo,” aliandika kwenye ukurasa wake wa X ambao zamani ulijulikana kama Twitter.

Kulingana na Babu Owino, kila mwezi Kaunti ya Nairobi itakuwa inapata zaidi ya Sh22 milioni.

“Shilingi tano kwa siku kwa wazazi 1,000 kwa kila shule ikiwa ni jumla ya Sh5,000 kila siku, kwa mara 22 katika shule ambazo zinapata chakula, ina maanisha kuwa kwa mwezi ni Sh110,000. Tuna shule 208 za umma Kaunti ya Nairobi kwa mara 110,000 utapata Sh22.8 millioni kila mwezi,” Babu aliendelea.

Ujumbe huo, ulimchochea Gavana wa Nairobi kuandika ujumbe wa kumjibu Bw Owino kuwa kwa sasa ni wanafunzi 80,000 wanaopata chakula kwa kutumia Sh5 baada ya kukamilisha awamu ya kwanza.

“Kuna watu wanapinga mradi wa chakula. Wanasambaza propaganda ambazo hazina manufaa. Tumezungumza na walimu wakuu ili waendelee na mipango yao hadi tutakapoanza tena awamu ya pili. Kuna mtu alisambaza video ya shule ya msingi ya Tumaini ambayo haina wanafunzi wala walimu,” aliandika Gavana Sakaja.

Mradi wa Dish na County unatarajiwa kuwalisha wanafunzi 250,000 katika shule zote za umma mjini Nairobi.

  • Tags

You can share this post!

Kisura wa pembeni anataka nigharamie mahitaji eti hana kazi

Naondoka Wizara ya Biashara baada ya kufufua uzalishaji wa...

T L